by Admin | 26 December 2022 08:46 pm12
2Timotheo 1:6 “Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu”.
Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo.
Neno la Mungu linatufundisha kuzichochea KARAMA tulizopewa,.. Ikiwa na maana kuwa “Kuwa na karamaa pekee haitoshi kuifanya kazi ya Mungu vizuri”..bali inahitajika Karama iliyochochewa. Na anayeichochoea si Mungu, bali ni sisi ndio tunaoichochea.
Mtu anapomgeukia Kristo na kuokoka, tayari Mungu anakuwa ameiweka karama ndani yake, kama mbegu ndogo sana.. Lakini karama ile isipochochewa inaweza kufa ndani ya mtu, na hatimaye mtu yule akabaki kama mtu asiye na karama kabisa.
Hata wanaoshiriki michezo ya kidunia, ijapokuwa wanavyo vipaji vya michezo hiyo, lakini wasipovifanya mazoezi ya kutosha, haijalishi wana vipaji vikubwa kiasi gani, bado vipaji vyao hivyo vitakuwa si kitu. Na vipaji vina muda wake, mwanamichezo akifikia umri Fulani kama hajakitumia vizuri kipaji chake, basi kinapungua nguvu chenyewe, kwasababu tayari umri umeshaenda!.
Na karama za rohoni au vipaji vya rohoni ni ivyo hivyo.. visipochochewa vinakufa na visipotumika katika muda fulani, vinaisha thamani nguvu ndani yake..Ndio maana maandiko yanasema..
Mhubiri 12:1 “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo.
2 Kabla jua, na nuru, na mwezi, Na nyota, havijatiwa giza; Kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua”
Na pia inasema..
1Yohana 2:14 “…..Nimewaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu”
Sasa maandiko yanasema Bwana alitoa wengine kuwa mitume, wengine manabii, wachungaji, waalimu, wainjilisti, karama za kuponya, matendo ya miujiza, karama za lugha, karama za masaidiano, imani, hekima, maarifa n.k (kasome Waefeso 4:11-12, 1Wakorintho 12). Lakini wengi hawajijui kama wanazo hizo karama.. kwasababu wanadhani zinaanza katika ukubwa wanaotugemea wao.
Wengi sana leo hii ni wainjilisti tangu siku ile wanapookoka, lakini kwasababu hawajijui kama wao ni wainjlisti, pale wanapojiona kuwa hawafanani na mwinjilisti mmoja maarufu, basi moto unazima ndani yao, pasipo kujua kama wanamzimisha roho, wengi ni waalimu tangu siku ile wanapookoka, lakini kwasababu hawajui namna ya kuzitumia karama zao na wanapoona wao si kama waalimu Fulani maarufu wanaowajua basi moto unazima ndani yao, wanabaki kusubiria muujiza siku moja wajikute wamekuwa wahubiri wenye uwezo wa kuhubiri kama watu Fulani maarufu.
Wengi wamepewa karama za kumwimbia Mungu, tangu siku walipookoka lakini kwasababu wanajiona kama sauti zao bado zinakwaruza, kwa kujilinganisha na wengine ambao tayari wanamwimbia Mungu kwa muda mrefu, basi wanatulia huku wakisubiri muujiza mwingine uwashukie utakaowafanya wawe kama hao wengine.
Kungoja huko ndiko kunakuua karama za watu wengi ndani yao.
Leo tutatazama njia 3, za namna ya kuzichochea karama zetu ili zifanye kazi katika viwango ambavyo Mungu amevikusudia.
1.KUJIFUNZA NENO.
Msingi wa karama zote ni Neno la Mungu, mtu aliyepungukiwa Neno la Mungu ndani yake, tayari karama yake inazima yenyewe tu ndani yake.. Kwanini Neno la Mungu??… kwasababu Neno la Mungu linatia hamasa, linatia moyo, linatupa sababu ya kuzitumia karama zetu, linafundisha jinsi ya kuzitumia kupitia mifano mbali mbali ya watumishi wa Mungu ndani ya biblia, na pia linatuonya madhara ya kutozitumia karama zetu. Hivyo Mtu mwenye Neno la Mungu la kutosha ni lazima tu karama yake itanyanyuka.
2. MAOMBI.
Hii ni njia ya pili ya kuchochoe karama zetu, Maandiko yanasesema tuombe bila kukoma (1Wathesalonike 5:17), Na kuomba kunajumuisha pia na kufunga, vitu hivi viwili vinaenda pamoja..tunapoomba Bwana anatuongezea uwezo na upako katika karama zetu.
Mathayo 17:21 “Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.”
3. MAZOEZI.
Hii ni njia ya tatu na ya muhimu sana, chochote kisichofanyiwa mazoezi hakiwezi kuwa bora.. hata karama isipofanyiwa mazoezi haiwezi kuwa bora, maana yake ni kwamba kama wewe una karama ya kuimba, kamwe usitegemee utakuwa bora, bila kuifanyia mazoezi karama hiyo, ni lazima uwe na vipindi vya kuinoa sauti yako, kutafuta na kujifunza jinsi ya kuzipangilia sauti kupitia waliokutangulia au waalimu, huku wewe mwenyewe ukifanya mazoezi ya kurudia rudia mara kadhaa… hivyo ndivyo karama yako itakavyoongezeka nguvu, lakini ukiiacha tu na kujiona tayari unajua kila kitu, basi hutaweza kupiga hatua..
Vile vile kama umepewa karama ya kiualimu, au kiinjiilisti..kama utaketi tu kusubiri kufundishwa, basi kamwe hutaweza kufundisha wengine..unapaswa utenge muda wa wewe kwenda kufundisha wengine, hata kama bado hujui vitu vingi,.. wewe kafundishe hivyo hivyo, Bwana atakufundisha huko mbele ya safari, makosa utakayoyafanya ndiyo yatakuwa darasa lako la kufanya vizuri katika matukio ya mbele..hivyo usiogope, nenda kahubiri..
Vile vile kama umepewa karama ya matendo ya imani, au karama za kuponya, usingoje ngoje.. nenda mahospitalini, nenda sehemu mbali mbali kafanye maombezi huku ukiwahubiria habari za njema za wokovu, usiogope wala kuvunjika moyo, unapoona umeombea watu 10, na hakuna aliyepona hata mmoja.. wewe endelea mbele, hizo ni hatua za awali, katika matukio yanayokuja Bwana atakutumia kwa maajabu mengi.
Na karama nyingine zote ni hivyo hivyo, ni lazima UZICHOCHEE!!..kama vile moto unavyochochewa.
Na ulingo mzuri wa kuiona karama yako ikifanya kazi ni ndani ya KANISA, yaani unapokuwa katika kusanyiko la Kristo ni kipindi kizuri cha kuiona karama yako kuliko unapokuwa nje ya kusanyiko, kwasababu Biblia inasema karama hizi lengo lake la kwanza ni kuujenga mwili wa Kristo, maana yake kulijenga kanisa (Waefeso 4:11).
Ichochee karama yako!
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Nini tofauti kati ya Kipawa na Karama?
Karama ya pili inayozungumziwa katika 2Wakorintho 1:15 ndio ipi?
NA VIUNGO VYETU VISIVYO NA UZURI VINA UZURI ZAIDI SANA.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/12/26/ichochee-karama-yako/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.