AKAPITA KATIKA LILE SHAMBA AMBALO YAKOBO ALIMPA YUSUFU MWANAWE

by Admin | 23 January 2023 08:46 pm01

Kuna wakati Bwana Yesu alianza safari ya kuchosha ya kutembea kutoka Yerusalemu kuelekea Galilaya..lakini maandiko yanatuonyesha katika safari yake yote hiyo hakuona mahali popote pa kupumzika, japo alikatiza katika vijiji na miji midogo midogo.

Lakini alipofika Samaria mahali ambapo hapakai wayahudi, aliingia katika eneo ambalo, huwenda alihisi amani  nyingi ya Mungu ikibubujika ndani yake, na hapo hapo akaona kisima cha maji akatulia apumzike kidogo.

Lakini maandiko yanatupa uelewa eneo hilo lilikuwa ni la namna gani mpaka likamfanya Yesu avutiwe nalo…yanasema..mahali pale palikuwa ni karibu na Shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu mwanawe..

Yohana 4:3-8

[3]aliacha Uyahudi, akaenda zake tena mpaka Galilaya.

[4]Naye alikuwa hana budi kupita katikati ya Samaria.

[5]Basi akafika kunako mji wa Samaria, uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu mwanawe.

[6]Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu amechoka kwa safari yake, akaketi vivi hivi kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita.

[7]Akaja mwanamke Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe.

[8]Kwa maana wanafunzi wake wamekwenda mjini kununua chakula.

Yesu aliiiona ardhi ile katika roho, aliona mbaraka ule wa Yakobo kwa mwanawe Yusufu unavyomkaribisha pale, hivyo hakuweza kupita hivi hivi bila kutenda jambo…aliiona haki ya Yusufu inamlilia shambani kwake.. Kumbuka Israeli yote ilikuwa ni Milki ya wana wote wa 12 wa Yakobo, lakini si kila shamba la mwana wa Yakobo Yesu alipumzika.

Hivyo kitendo cha Yesu tu kutulia pale, kama tunavyojua habari watu wengi wa Samaria wakapokea wokovu akawaokoa watu ambao hawakustahili wokovu kabisa (yaani wasamaria).

Unaweza kujiuliza ni wakati gani Yakobo alimpa Yusufu shamba hilo? Waweza kusoma habari hiyo katika..Mwanzo 48:21-22

Utaona akipewa sehemu mara dufu ya wenzake.. Na hiyo yote ni kwasababu Yakobo alimpenda Yusufu kwa tabia zake njema.

Ile Tabia ya Yusufu ya kumcha Bwana alipokea thawabu sio tu za wakati ule alipofanyika kuwa waziri mkuu wa Misri.. Lakini tunaona pia hadi kipindi cha Bwana Yesu baraka zake bado zilitembea.

Leo hii ukimcha Mungu wewe kama kijana, utawasababishia wengine kupokea neema ya wokovu  hata wakati ambapo haupo hapa duniani.. Kumcha Mungu ni uwekezaji mkubwa sana zaidi ya mali.

Bwana akikubariki uzao, basi huwenda vitukuu vyako vikawa majeshi hodari ya Kristo, kwasababu Yesu anapita kuangalia ni wapi mbaraka wa Yusufu upo  ili apumzike?akakuona wewe.

Akikubariki mashamba au mali, siku za mbeleni aidha uwapo hai au ufapo, Kristo atapita hapo na patakuwa kitovu cha madhabahu nyingi za Mungu.

Chochote kile ukiachacho duniani, kama sio mali, kama sio shamba, kama sio vitu..basi Mungu atatumia hata mifupa yako kuwaponya wengine.. Ndivyo Mungu alivyovyafanya kwa Elisha baada ya kufa na miaka mingi kupita ameshasahaulika, amebakia tu mifupa,kaburini, lakini maiti ilipoangukia mifupa yake, ile maiti ikafufuka.

Je ni tabia gani unaionyesha kwa Mungu sasa, hadi akupe shamba lake spesheli ambalo Kristo atakuja kupumzikia hapo siku za mbeleni? Watoto wako, vijukuu vyako, vitabrikiwaje kama wewe hutamcha Mungu sasa?

Tafakari maisha ya Yusufu, kisha fananisha na yako utapata majibu. Yatupasa tuichukie dhambi, tuchukie uasherati, tuchukie wizi, tuwe waaminifu, tuishi maisha yanayompendeza Mungu sikuzote. 

Na hatimaye na sisi tutakuwa wokovu kwa vizazi vyijavyo. 

Bwana atuponye..Bwana atusaidie.

Shalom

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

WALA HAKUSIMAMA MTU PAMOJA NAYE, YUSUFU ALIPOJITAMBULISHA KWA NDUGUZE

Je! habari ya Yusufu, inabeba ujumbe gani kwa agano jipya?

UVUMILIVU NA MIKAKATI YA ABSALOMU, INA FUNZA NYUMA YAKE.

Kuiaua Nchi ni kufanya nini? (Waamuzi 18:2).

Injili iliyopo kwa Samaki aina ya Eeli.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/01/23/akapita-katika-lile-shamba-ambalo-yakobo-alimpa-yusufu-mwanawe/