IPENDE BUSTANI YAKO.(Ilime, itunze)

by Admin | 22 May 2023 08:46 pm05

Nakusalimu katika jina la mwokozi wetu Yesu Kristo. Karibu tujifunze maneno ya uzima.

Ipo tabia ambayo tunapaswa tujifunze kuhusu Mungu. Kama tunavyojua, alipomaliza kuumba vitu vyote ndani ya zile siku saba, zoezi la mwisho kabisa lilikuwa ni Mungu kupanda bustani mashariki mwa Edeni. Tengeneza picha, bustani hiyo ilikuwaje! Bila shaka ilikuwa ni nzuri sana. Mungu alifanya kazi ya kuchukua Ua hili, Ua lile, ukoka huu, ukoka ule, mti huu wa kivuli, mti ule wa matunda kila moja mahali pake stahiki.. Yaani kwa ufupi Edeni ni bustani ambayo iliundwa kwa kila aina ya mmea, lakini katika mpangilio bora. Jambo lililoifanya bustani ile kuwa tofauti na maeneo mengine yote duniani.

Kwani huko kwingine kulijiotea otea, bila mpangilio maalumu. Japo pia napo kulikuwa pazuri lakini sio kama Edeni, kwasababu ile ni bustani iliyopandwa sio kujiotea. Lakini tunaona, asili ya ile Bustani. Ni kwamba ilihitaji kulimwa na matunzo baada ya pale ili iendelee kuwepo vilevile katika ubora wake. Hii ikiwa na maana kama isingetunzwa na kulimwa, ingepotea kabisa, na kufanana tu na sehemu nyingine yoyote ya dunia.

Mwanzo 2:8 “Bwana Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya…15 Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.

Watunza bustani wanaelewa jambo hili, mahali ambapo wanazipanda, huwa ni lazima mara kwa mara, wawepo kung’oa majani-shambulizi yanayojitokeza, wanafyeka ukoka unapozidi kimo, wanatia mbolea panaposua sua, na wanainyeshea bustani kila siku, na wakati mwingine kuiwekea uvuli. Hivyo ni kazi ambayo inamgharimu mtunza bustani kuwepo pale wakati mwingi.

Ndivyo ambavyo Mungu alimpa jukumu hilo Adamu, kwamba aitunze bustani na kuilima, kwasababu hilo halikuwa jukumu lake tena. Tafsiri yake ni kwamba ili aendelee kukaa katika mahali pazuri pa nchi. Hana budi kupalima na kupatunza. Asipofanya hivyo pataendelea kuwa kama sehemu nyingine tu ya dunia.

Lakini Adamu, hakuweza kudumu katika bustani ile kwasababu aliyakaidi maagizo ya Mungu.

Hii ikifunua nini?

Kila mtu ameandaliwa Edeni yake hapa duniani, ambayo atamfurahia Mungu wake katika hiyo. Si kila mazingira Mungu amekuwekea wewe kumfurahia yeye, si kila mahali ni Edeni yako. Ipo sehemu maalumu, ambapo hapo Mungu anakuundia kisha wewe unapatunza baada ya hapo.

Na sehemu yenyewe ni ndani ya Kristo.

 Maana yake ni kuwa ukishaokoka, tayari Mungu amekuwekea mema yako mbeleni. Hivyo kuanzia huo wakati huna budi kuanza kuistawisha bustani yako kwa kuitilia mbolea mara kwa mara, kuinyeshea maji, kuipalilia, kuichonga n.k.. Ndio hapo, linakuja suala la Maombi ya mara kwa mara, mikesha, mifungo, kutafakari Neno, kufanya ibada za sifa,  kutoa sadaka, kujitenga na dhambi, na kushuhudia.

Unapokuwa mtu wa namna hii ndivyo unavyoifanya bustani yako kupendeza siku baada ya siku rohoni, ndivyo inavyojitofautisha na sehemu nyingine za dunia, kwa uzuri wake. Matokeo yake ni kuwa Dunia yako itakuwa ya neema sikuzote yenye furaha, Amani na mafanikio, yenye kububujika maziwa na asali. Lakini ukikaa tu ukasubiri, ukasema Mungu atatenda, huku huyatunzi  maneno ya Mungu ndani yako, sahau kuona mabadaliko yoyote maisha yako yatakuwa hayana tofauti na yale ya kale, kwasababu kazi ya utunzaji sio ya Mungu bali ni yako. Wewe umemsubiria Mungu, wakati Mungu alishamaliza kazi yake.

Litunze sana Neno la Mungu, kwa kuliishi sio kulisikia tu. Kwani wanaofanya hivyo wanafungua milango mingi sana ya kiroho, Kanisa la Filadelfia ndio kanisa pekee lililopendwa na Kristo kwasababu liliyatunza maneno yake, na matokeo yake likafunguliwa mlango wa mafanikio mbele yake.

Ufunuo 3:8  “Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe UMELITUNZA NENO LANGU, wala hukulikana jina langu”.

Hivyo anza sasa kujibidiisha kulitendea kazi Neno la Mungu. Kwa jinsi unavyolitunza ndivyo utakavyoona mabadiliko yako.

Bwana akubariki.

Je! Umeokoka? Je, unatambua kuwa hizi ni nyakati za mwisho? Tunaishi katika dakika za nyongeza tu? Dalili zote zilizotabiriwa kuhusiana na kurudi kwa pili kwa Yesu zimeshatimia?. Wasubiri nini? Ukifa leo utajibu nini mbele ya kiti cha enzi cha Mungu?  Tubu sasa ukabatizwe, upokee ondoleo la dhambi zako. Ikiwa bado hujafanya hivyo, basi wasiliana nasi kwa namba zetu hizi kwa msaada huo; +255693036618/+255789001312

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Kuna tofauti gani kati ya  “Edeni” na “Adeni”?

UNAWAZA NINI SASA, JUU YA UFALME WA MBINGUNI?

EDENI YA SHETANI.

SISI TU MANUKATO YA KRISTO.

MBINGU MPYA NA NCHI MPYA. (Sehemu ya 1)

Kwanini Mungu hakumuua Nyoka, akamwacha Hawa ajaribiwe katika bustani ya Edeni?

Kwa jina lake Ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa.

AKAPITA KATIKA LILE SHAMBA AMBALO YAKOBO ALIMPA YUSUFU MWANAWE

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/05/22/ipende-bustani-yako-ilime-itunze/