Vihekalu vya fedha vya Artemi vilikuwaje? (Matendo 19:24).

by Admin | 10 July 2023 08:46 am07

Jibu: Turejee

Matendo 19:24 “Kwa maana mtu mmoja, jina lake Demetrio, mfua fedha, aliyekuwa akifanya vihekalu vya fedha vya Artemi, alikuwa akiwapatia mafundi faida nyingi”.

Mahekalu yalikuwa ni majengo maalumu kwaajili ya ibada za miungu.. Lilikuwepo hekalu moja tu duniani la Mungu wa kweli, ambalo lilitengenezwa Yerusalemu, hilo pekee ndilo Mungu wa kweli wa mbingu na nchi alikuwa akiabudiwa ndani yake kipindi cha agano la kale. Lakini mahekalu mengine yote yaliyojenga tofauti na hilo yalikuwa yanamuabudu shetani kupitia sanamu.

Sasa kipindi Mtume Paulo na wanafunzi wengine wamefika mji wa Efeso, walikuta jamii ya watu wa pale wanamwabudu mungu mke waliyemwita Artemi.

Na katika huo mji wa Efeso walikuwa wamemtengenezea Hekalu kubwa, na ndani ya hilo hekalu kulikuwa na sanamu ya huyo mungu mke, Artemi ambayo wanaamini haikutengenezwa na mtu bali ilishushwa/ilianguka kutoka mbinguni (jambo ambalo halikuwa la kweli). Na watu kutoka pande zote za dunia walikuwa wanakuja hapo Efeso lilipo hekalu la huyo Artemi kumwabudu..

Matendo 19:35 “Na karani wa mji alipokwisha kuwatuliza watu, akasema, Enyi wanaume wa Efeso, ni mtu gani asiyejua ya kuwa mji wa Efeso ni mtunzaji wa HEKALU LA ARTEMI, aliye mkuu, NA WA KITU KILE KILICHOANGUKA KUTOKA MBINGUNI?”.

Sasa kwasababu walikuwa wanamwamini huyo mungu waliyemwita Artemi kuwa ni mkuu na aliye na wafuasi wengi, wale wageni walikuja kutoka mataifa ya mbali walipata changamoto ya kumwabudu wakiwa makwao (huko katika mataifa yao ya mbali),

Hivyo ili kutatua hiyo changamoto..baadhi ya mafundi waliokuwepo pale Efeso wakaanza biashara ya kutengeneza vijihekalu vidogo vidogo vinavyobebeka vinavyofanana kabisa na lile hakalu lenye sanamu ya huyo Artemi, ili watu wanaotoka mbali wakiisha kumwabudu wakiwa Efeso waweze kuondoka na vijihekalu hivyo na kwenda navyo huko walikotokea na kuendeleza ibada zao, ambapo wengine waliviweka kwenye vyumba vyao, wengine katika vimilima na sehemu mbali mbali.

Vihekalu hivyo vilitengenezwa kwa madini ya “fedha”, ambapo mafundi wakiongozwa na fundi mkuu aliyeitwa Demetrio waliyeyusha madini hayo ya fedha na kuyatengeneza kwa muundo wa hilo hekalu.

Lakini Paulo pamoja na wanafunzi wengine wa Bwana walijua uongo huo wa shetani, na hivyo walipoingia huo mji wa Efeso waliupindua kwa injili ya kweli, na wengi wakamwamini Mungu wa kweli na kumpokea Yesu na kuacha ibada hizo za miungu, ambayo nyuma yake ni shetani anaabudiwa.

Ukisoma mistari ya juu utaona matokeo ya injili ile iliwafanya maelfu ya watu waache uchawi waliokuwa wanaufanya, na kumgeukia Mungu.

Matendo 19:18  “Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao.

19  Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu.

20  Hivyo ndivyo neno la Bwana lilivyozidi na kushinda kwa nguvu”.

Na hata sasa uweza wa Mungu upo,  Injili ya Kristo ina nguvu nguvu kuliko uchawi!. Sawasawa na Warumi 1:16 “Kwa maana siionei haya Injili kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia”.

1Wakorintho10:4-5 “(maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;)

5  tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo;

6  tena tukiwa tayari kupatiliza maasi yote, kutii kwenu kutakapotimia”

Usiionee haya (aibu) injili.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

NINI TOFAUTI KATI YA MATENDO YA SHERIA NA MATENDO YA IMANI?

Ni kwa namna gani Kristo analitakasa kanisa kwa Maji katika Neno? (Waefeso 5:26)

Nini maana ya Mhubiri 10:16, inaposema Ole wako, nchi, akiwa mfalme wako ni kijana?

NI NANI ALIYEKUPA MAMLAKA HII UYATENDE HAYA?

ALIPOKUWA ANGALI MBALI, BABA YAKE ALIMWONA.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/07/10/vihekalu-vya-fedha-vya-artemi-vilikuwaje-matendo-1924/