Kwanini Daudi achukue mawe matano, na malaini na sio vinginevyo?

by Admin | 4 August 2023 08:46 pm08

SWALI: Naomba kufahamu maana ya mawe matano ya kombeo na jiwe la kwanza maana yake nini na la pili hata la tano, na kwa nini mawe laini asingeokota jiwe ni jiwe tu?


JIBU: Daudi alipokutana na Goloathi maandiko yanatuambia akashuka katika kijito Cha maji akayaokota mawe matano malaini, kama silaha yake ya kumwangusha Goliathi.

1 Samweli 17:40

[40]Akaichukua fimbo yake mkononi, akajichagulia mawe laini matano katika kijito cha maji, akayatia katika mfuko wa kichungaji aliokuwa nao, maana ni mkoba wake, na kombeo lake alikuwa nalo mkononi mwake, akamkaribia yule Mfilisti.

Lakini Swali linakuja, Kwanini yawe matano, na je yanafunua Nini rohoni? Na pia Kwanini yawe malaini?

Baadhi ya watu wanaamini pengine Daudi hakuwa na Imani ya kutosha Kwa Mungu ya kuamini kuwa jiwe Moja tu lingetosha kumwangusha Goloathi, ndio maana akachukua matano. Lakini uhalisia ni kwamba Daudi alikuwa na Imani, hata kitendo tu Cha kukataa kubeba silaha za vita alizopewa na mfalme ilikuwa ni Imani kubwa.

Wengine wanaamini mawe Yale matano, yanafunua mambo matano ambayo Daudi alikuwa nayo yaani  1) Imani, 2) utiifu, 3)utumishi, 4)maombi na 5) Roho Mtakatifu.

Wengine wanaamini kuwa yanasimama kuwawakilisha wale watoto 5 wa Yule jitu aliyeitwa Refai, ambapo, Goliathi akiwa mmojawapo.(2Samweli 21:15-22). Hivyo Daudi alionyesha kuwa wote atawaangamiza.

Wengine wanaamini kuwa mawe yale matano yanafunua zile huduma tano (5), Waefeso 4:11. Ambazo hizo zinasimama kama msingi wa kumuangusha shetani  katika kanisa.

Lakini tukirudi  katika muktadha wa habari yenyewe, kiuhalisia ni kuwa Daudi alichukua mawe matano, akiamini kuwa la kwanza likimkosa bado la pili lipo atarusha tena, na kama la pili likimkosa basi bado lipo la tatu atarusha tena..Kufunua jinsi gani alivyokuwa na akiba ya imani. Bwana Yesu alisema, Imetupasa kuomba sikuzote bila kukata tamaa,  (Soma Luka 18:1-8), Upo wakati utaomba jambo kwa Bwana, halafu usijibiwe muda huo huo, je! Utakata tamaa kesho tena usiombe? Yesu anatuambia tuombe bila kukoma. Daudi aliamini hata ikitokea jiwe la kwanza limegonga dirii ya chuma, sio wakati wa kuvunjika moyo, ni kuvuta lingine, na kuendelea na mapambano. Vivyo hivyo na sisi yatupasa tuwe watu wenye akiba nyingi ya imani ndani yetu. Tunaomba tena na tena na tena, kwasababu hatujui ni jiwe lipi litaleta majibu, kama ni la kwanza au la katikati au la mwisho.

Lakini pia utaona hekima nyingine Daudi aliyoitumia ni kwenda kuyachukua mawe yake kwenye kijito cha maji. Jiulize ni kwanini iwe kwenye maji na sio penginepo? Kwasababu kimsingi mawe yapo kila mahali. angeweza kuokota tu ardhini.

Ni kufunua nini? Daudi alitambua VIJITO VYA MAJI YA UZIMA, ndipo wokovu ulipo. Ambavyo ni Yesu Kristo (Yohana 7:28). Usalama wa imani yake uliegemea kwa Mungu.  Hata sasa Bwana anataka imani yetu iegemee kwa Yesu Kristo, huko ndiko asili ya nguvu zetu ilipo, Kama mkristo usipolitambua hili ukawekeza imani yako kwenye elimu, au mali, au vitu vya ulimwengu huu, tambua kuwa huwezi mpiga adui yako ibilisi, kwa lolote.

Na mwisho kabisa Daudi aliyatwaa mawe laini kwanini yawe malaini.  Hata katika maji, yapo mawe ya maumbile mbalimbali, yapo makubwa yapo madogo, yapo yenye ncha, yapo malaini. Lakini alitambua kuwa jiwe litakalokaa katika kombeo lake, na litakalopaa vizuri na kumwangusha adui yake, sio kubwa, wala lenye ncha, wala zito sana. Bali laini, la mviringo. Kufunua nini.. Hauhitaji imani kubwa ya kuhamisha milima ili kumwangusha ibilisi. Bali kipimo cha imani yako, ukikitumia vema kinatosha kabisa kumdondosha Shetani.

Warumi 12:3  Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani. 4  Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja; 5  Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake.

Ukitumia vema nafasi yako uliyopewa na Mungu. Katika udogo wako, unyonge wako, umaskini wako, utamwangusha adui. Kila mmoja wetu amepewa nguvu hizo na Mungu. Hivyo usisubiri uwe Fulani ndio udhani utauangusha ufalme wa shetani. Hapo hapo ulipo ikiwa umeokoka, jiwe lako Kristo amekutolea. Litumie vizuri, lirushe vema, Goliathi atalala chini.

Bwana akubariki

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Je! aliyemwua Goliathi ni Daudi au Elhanani.

WALA HAKUACHA MTU ACHUKUE CHOMBO KATI YA HEKALU.

LIONDOE JIWE.

YESU NDIYE ATAKAYEKURUSHIA MAWE, USIPOTUBU.

YESU NDIYE ATAKAYEKURUSHIA MAWE, USIPOTUBU.

JIWE LILILO HAI.

TEMBEA NDANI YA SUKOTHI YAKO.-Maafundisho maalumu kwa watumishi

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/08/04/kwanini-daudi-achukue-mawe-matano-na-malaini/