Maziara ni nini? Je! Na Tunaruhusiwa kuyajenga kwenye makaburi yetu?

by Admin | 5 September 2023 08:46 pm09

Kwa utamaduni wa sasa mtu anapokufa, huwa anafukiwa chini ardhini, na juu huwekewa  kiashirio Fulani cha kawaida kuonesha eneo hilo lipo kaburi. Lakini  watu wengine hupenda kuyapa thamani makaburi ya watu wao, hivyo kwa juu hujengea, kichumba Fulani kinachopambwa kwa vito au mawe ya thamani , wengine wanaweka mnara Fulani n.k. Sasa vitu hivi vyote vinavyojengewa juu ndio huitwa Maziara.

Kwamfano katika picha hii, ni mfano wa Ziara ambalo lilijengwa na wenyeji wa Marekani kama kumuenzi raisi wao wa kwanza wa taifa hilo aliyeitwa George Washington.

Hata katika agano la kale, enzi za biblia, yapo makaburi yaliyokuwa ya kawaida, lakini pia yapo yaliyokuwa yamejengewa maziara. Na hayo yalikuwa hususani ya wafalme na manabii wakubwa waliotokea Israeli, ambao waliuliwa kikatili mfano wa hao  ni Zekaria, Hagai na Malaki.  Na waliohusika sana kutengeneza maziara haya walikuwa ni hawa waandishi na mafarisayo(Watu wa kidini). Wakidai kuwa wanawa-enzi manabii wao, lakini tunaona Yesu akiwakemea kwa dhambi ya unafki waliyokuwa wanaifanya kwa tendo hilo.

Tusome.

Mathayo 23:29  Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnayajenga makaburi ya manabii, na kuyapamba maziara ya wenye haki, 30  na kusema, Kama sisi tungalikuwako zamani za baba zetu, hatungalishirikiana nao katika damu ya manabii. 31  Hivi mwajishuhudia wenyewe, ya kwamba ninyi ni wana wao waliowaua manabii. 32  Kijazeni basi kipimo cha baba zenu. 33  Enyi nyoka, wana wa majoka, mtaikimbiaje hukumu ya jehanum? 34  Kwa sababu hiyo, angalieni, mimi natuma kwenu manabii na wenye hekima na waandishi; na wengine wao ninyi mtawaua na kuwasulibisha, na wengine wao mtawapiga katika masinagogi yenu, na kuwafukuza mji kwa mji; 35  hivyo ije juu yenu damu yote ya haki iliyomwagika juu ya nchi, tangu damu ya Habili, yule mwenye haki, hata damu ya Zakaria bin Barakia, mliyemwua kati ya patakatifu na madhabahu. 36  Amin, nawaambieni, Mambo hayo yote yatakuja juu ya kizazi hiki.

Soma pia (Luka 11:47-48).

Swali ni je! Walikuwa wanafanya makosa kutenda jambo lile?

Jibu ni hapana, Bali walichokuwa wanakifanya nje, hakikuendana na kile kilichokuwa mioyoni mwao na ndio maana akawaita wanafiki. Kwasababu walikuwepo pia manabii wa Mungu na watu wenye haki wakati wao, mfano wa Yohana, pamoja na yeye mwenyewe lakini walikuwa wanataka kuwaua. Na ndivyo walivyokuja kufanya kwa Bwana, pamoja na mitume wako na watakatifu wa kanisa la kwanza kama vile wakina Stefano.

Je! Sisi tujengapo maziara kama heshima  kwa wafu wetu tunatenda dhambi?

Jibu ni la, Endapo tu hatutashirikisha ibada yoyote ya wafu mahali pale. Lakini kama ni kwa kumbukumbu, au kumu-enzi marehemu wako, hakuna shida kuweka ziara (kupamba kaburi lako kwa jinsi upendavyo). Lakini fahamu tu hilo halitakuongezea jambo lolote rohoni. Wala halimfaidii kwa lolote Yule marehemu kule alipo.

Je! Ni sawa kwa Mkristo kusafisha kaburi la mfiwa wako, na kufanya ibada mahali pale?

Kutunza kaburi lolote, yaani kulisafisha, kulirepea, kulipandia bustani, kulilinda.. Si kosa kibiblia, kwasababu tunaona katika biblia makaburi yalitunzwa kwa bustani, soma (Yohana 20:15), pia yalilindwa, Na zaidi yalihifadhiwa yasiharibiwe. Soma

2Wafalme 23:16 Naye Yosia alipogeuka, aliyaona makaburi yale yaliyokuwako huko, juu ya mlima; akatuma watu, akaitoa ile mifupa katika yale makaburi, akaiteketeza juu ya madhabahu, akainajisi, sawasawa na lile neno la Bwana, alilolinena yule mtu wa Mungu, aliyetamka mambo hayo.  17 Kisha akasema, Ni kumbukumbu la nani, hili ninaloliona? Na watu wa mji wakamwambia, Ni kaburi la yule mtu wa Mungu, aliyetoka Yuda, akayanena mambo hayo uliyoyatenda wewe juu ya madhabahu ya Betheli.  18 Akasema, Mwacheni; mtu awaye yote asiiondoe mifupa yake. Basi wakaiacha mifupa yake, pamoja na mifupa ya yule nabii aliyetoka Samaria.

Hivyo, upendapo kutunza kaburi la mpendwa wako, aliyefariki hufanyi kosa.

Vipi katika kufanya ibada?

Zipo ibada za wafu, ambazo ndizo zinazofanyika mara nyingi katika makaburi ya marehemu, ibadani hizo, zinahusianisha kuwaombea wafu hao, n.k. Ibada hizi ni za kipagani, na mkristo hapaswi kuzifanya ni  ibada za miungu. Au wengine wanakwenda kuzungumza na kaburi wakiamini Yule mtu yupo pale makaburini anawasikia. Huo ni uchawi.

Hivyo hakuna mahusiano yoyote ya kiibada katika makaburi. Endapo imetokea unakwenda kufanya maziara (yaani kukarabati au kupamba), basi unachofanya ni kufungua kwa maombi na kufunga kwa maombi, kisha mnaendelea na kazi yenu, ili kutimiza hili andiko

Wakolosai 3:17  “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye”.

Na kama mmeguswa kutafakari maneno ya Mungu mahali pale, kama mfanyapo sehemu nyingine zozote, mfano kazini, shuleni, chini ya mwembe n.k..  Basi iwe ni kwa Mungu na sio kwasababu ya makaburi. Epuka Ibada za wafu.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Pango la Makpela ni lipi, je lina umuhimu wowote kwetu?

MAKABURI YAKAFUNUKA; IKAINUKA MIILI MINGI YA WATAKATIFU WALIOLALA;

MAUTI NA KUZIMU ZIKAWATOA WAFU WALIOKUWAMO NDANI YAKE.

Nini maana ya kuabudu?

Wenye kubatizwa kwa ajili ya wafu ni wakina nani?

Praitorio ni nini? Na Kwanini ilikuwa ni najisi kwa wayahudi kuingia humo? (Yohana 18:28)

Nini maana ya Ukuta uliopakwa chokaa (Matendo23:3)?

Makanda ni nini?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/09/05/maziara-ni-nini/