MAKABURI YAKAFUNUKA; IKAINUKA MIILI MINGI YA WATAKATIFU WALIOLALA;

MAKABURI YAKAFUNUKA; IKAINUKA MIILI MINGI YA WATAKATIFU WALIOLALA;

Nakusalimu katika jina kuu sana la Bwana wetu na mwokozi wetu Yesu Kristo, Mfalme wetu, Karibu tujifunze maneno ya uzima.

Utakumbuka huduma ya Bwana wetu iligawanyika katika sehemu kuu tatu,

Ya kwanza, ilikuwa ni hapa duniani,

Ya pili ni Kuzimu

Na ya tatu ni mbinguni.

Lakini wengi wetu tunafahamu ile ya duniani na mbinguni, Lakini kwa sehemu ndogo sana tunaielewa ile ya kuzimu. Ni vema pia tukaifahamu hiyo ili tujue ni nini tutakutana nacho baada ya kifo.

Siku tukiifahamu kwa mapana, hatutaacha kumshukuru Bwana Yesu kwa kifo chake pale msalabani.

Kama tunavyosoma siku ile Bwana aliyokufa, kuna matukio kadha wa kadha yaliyotokea, mojawapo ni lile la pazia la hekalu kupasuka, lakini tukio lingine ambalo lilitokea la kustaajabisha sana, ni lile la kuonekana  kwa watu ulimwenguni ambao walikuwa tayari wameshakufa zamani. Na watu hao walikuwa ni watakatifu wa zamani.

Biblia inatuonyesha baada ya kufufuka kwao walianza kutembea tembea na kuingia mpaka mji mtakatifu  wa Mungu (Yerusalemu.)

Mathayo 27:50 “Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake.

51 Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;

52 makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala;

53 nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi”.

Sasa swali unaweza kujiuliza ni kwanini uwe ni wakati ule na si mwingine, kwanini waonekane wanatoka makaburini, na kutembea tembea duniani, huku wakiwatokea watu? Kwanini iwe hivyo? Na hao watu sasahivi wapo wapi?

Hii ni kutuonyesha kuwa zamani mtu alipokufa, hakuwa huru hata kidogo, alikuwa anakwenda   moja kwa moja kaburini haijalishi ni mtakatifu au mwovu. Huko kaburini ndio sasa kuliganyika katika  sehemu ya waovu na wema.

Na kama tunavyojua sikuzote kaburi ni kama gereza, huwezi kwenda popote, au kufanya lolote, ndivyo ilivyokuwa kwa watu wote waliokuwa wanakufa zamani, walikuwa sehemu fulani tu, wamekaa wanasubiria siku moja masihi aje awaondoe huko.  (Waebrania 2:14-15)

Lakini Bwana Yesu alipokuja, alifanya kazi ya kuyapasua makaburi hayo yaliyokuwa yamewashikilia kwa nguvu ya dhambi kwa muda mrefu . Lakini biblia inatuonyesha hakupasua makaburi ya wote, bali ya wale watakatifu tu. Na matokeo yake  wakatoka huko, wakawa huru kama vile wanaishi tena duniani, na ndio maana wakawatokea wengi, wakatembea tembea huu na huko mpaka mji mtakatifu (Yerusalemu) n.k. kuonyesha ni jinsi gani wafu waliokufa katika Kristo walivyo huru, rohoni.

Hiyo ni kufunua kuwa, mtakatifu yeyote anayekufa leo, haendi tena kaburini kama watu wanavyodhani..ataliona tu kaburi kwa pale pembeni, lakini yeye hatakwenda huko kabisa bali ataondoka na kwenda kuendelea kuishi sehemu nyingine fulani iliyo nzuri sana, ijulikanayo kama Paradiso (peponi) Luka 23:43. Huko atakuwepo na Bwana Yesu mwenyewe, na watakatifu wengine, watakuwa ni kama tu vile hawajawahi kufa, wanaishi kama tunavyoishi hapa, isipokuwa tu huko ni kuzuri sana.

Na ndio maana Bwana Yesu alisema maneno haya,

Yohana 11:25b….Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi;

Yapo maisha baada ya kufa kwa mtakatifu.. , hawi kifungoni, anakuwa huru kule PEPONI (Paradiso), akimfurahia Kristo, huku akingojea siku ya Unyakuo ifike, aje kuuchukua mwili wake, aende mbinguni.

Lakini mtu anayekufa katika dhambi, ni moja kwa moja kaburini, kifungoni, kwenye giza nene, ndio kuzimu kwenyewe, maisha yake yanagotea pale anapokufa, hayawezi kuendelea kuishi, sio kwamba roho yake itakufa, hapana, bali ni kwamba hawezi kuwa na maisha, kama sisi tuliyonayo, au wale wale wengine waliyonayo.

Biblia inasema hivi, juu ya Bwana Yesu alipokwenda kuzimu;

1Petro 3:19 “ambayo kwa hiyo aliwaendea roho waliokaa kifungoni, akawahubiri;

20 watu wasiotii hapo zamani, uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja, siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane, waliokoka kwa maji”.

Unaona watu wote wenye dhambi sasa wapo huko vifungoni, kwa maelezo marefu juu ya habari hiyo, tutumie ujumbe inbox tukutumie somo lake..

Lakini utajisikiaje wewe uliye dhambini, ukifa leo katika hali hiyo? Siku hiyo utatamani upate hata nuru kidogo hutaona, utatamani, utembee tembee huku na huko  kama wale wengine hutaweza, utatamani ule au unywe hutaweza, utakuwa katika jehanamu ya mateso daima, ukiteseka, kama Yule tajiri wa Lazaro, ambaye aliomba hata achovyewe maji kidogo kwenye ncha ya kidole cha Lazaro,akashindwa,(Luka 16:19-31) utakaa huku  huku ukingojea na wewe siku ile ya hukumu ifike, ufufuliwe, uhukumiwe kisha utupwe kwenye lile ziwa la moto milele na milele.

Ndugu, kumbuka kifo hakina hodi, vilevile Unyakuo pia hauna hodi, ni siku yoyote au wakati wowote, unaondoka hapa duniani, au Yesu anarudi, inasikitisha kusoma katika biblia kwamba “kuzimu hakishibi watu”. Ikiwa na maana Maelfu kwa maelfu wa watu wanaenda huko kila siku.

Tutawezaje kupona tusipoujali wokovu mkuu namna hii. Aliyeshinda kaburi na mauti kwa ajili yetu, yupo hata sasa kutuokoa, Embu tufungue mioyo yetu, atupe wokovu huu bure. Atusamehe makosa yetu yote. Hata siku tukifa tuwe na uhakika kuwa kaburi sio sehemu yetu.

Tubu dhambi zako kwa kumaanisha kabisa kuziacha, kisha uwe tayari kubatizwa kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako kuukamilisha wokovu wako, Na Bwana atakupokea.

Ikiwa utahitaji msaada wa kumpokea Yesu, basi unaweza kuwasiliana nasi pia kwa namba hizi. +255693036618 / +255789001312

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

UVUMILIVU WA MUNGU ULIPOKUWA UKINGOJA.

YANAYOENDELEA SASA KATIKA MADHABAHU YA MUNGU ROHONI.

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 3

UNYAKUO.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
3 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
2 years ago

AMEEN

Antelm Barack
Antelm Barack
2 years ago

Ameni..Ubarikiwe sana Mtumishi kwa ufunuo huu wa ajabu wa Neno la Mungu.
Mungu azidi kukupaka mafuta kwa ajili ya kulifunua Neno lake, hasa zaidi katika nyakati hizi za mwisho mwisho za kuimalizia safari yetu hii ya imani.
Ubarikiwe mno mno mno!!