Novena ni nini? Na je ipo kibiblia?

by Admin | 23 October 2023 08:46 am10

Jibu: Neno “Novena” limetokana na neno la kilatini “Novem”… lenye maana ya “Tisa”(9). Madhehebu baadhi ikiwemo Katoliki na Orthodox yamelitoa neno hili na kulitumia katika aina Fulani ya mfululizo wa sala kwa kipindi cha siku 9.

Sala hizo zinahusisha kuomba kwaajili ya  jambo fulani au kushukuru, na zinahusisha ibada za kuomba Rozari kwa wakatoliki (jambo ambalo si sahihi kibiblia). Na kwanini kusali Rozari sio agizo la biblia?, fungua hapa kwa maelezo Zaidi >>>JE SALA YA ROZARI TAKATIFU NI YA KIMAANDIKO?

Sasa msukumo wa kuomba Novena, (yaani siku 9) mfululizo umetokana na matukio maalumu yanayotokea baada ya siku 9, au miezi 9 kumalizika. Kwamfano utaona kabla ya Pentekoste kutimia, walikusanyika Mitume na watu wengine baadhi mahali pamoja kuomba, na wakaomba kwa muda wa siku 9, baada ya Bwana Yesu kupaa na siku ya 10 ikawa ni Pentekoste.

Hivyo ushawishi huu wa kupokea Roho Mtakatifu baada ya maombi ya siku 9, ukaaminika na madhehebu hayo kubwa ni lazima uendelee ili kupokea kitu kingine mfano wa hicho kutoka kwa Mungu, vile vile mwanamke anajifungua mtoto baada ya miezi 9, hili nalo likawafanya viongozi wa madhehebu haya kuamini kuna kitu katika 9, (novena).

Sasa swali ni je! Biblia imetuagiza kutumia mfumo wa Novena, katika maombi ili kupokea jambo maalumu kutoka kwa Mungu? Kwamba tuwe na maombi maalumu ya kurudia rudia kwa muda wa siku 9 ili tupokee jambo kutoka kwa Mungu?.

Jibu ni la!.

Biblia haijaagiza mahali popote tusali “Novena” kwamba tuwe na kipindi Fulani maalumu cha siku 9 mara kwa mara ili Mungu aachilie kitu juu yetu. Utaratibu huu umetengenezwa na wanadamu, kufuatia ushawishi wa siku ya Pentekoste. Hivyo kama umetengenezwa na wanadamu, hauwezi kuwa Sharti, au Agizo la lazima kwa wakristo, kwamba usipofanya hivyo ni kosa kibiblia!.

Agizo hili linaweza kuwa la binafsi, kama tu vile mfungo usivyokuwa sharti, ni jinsi mtu atakavyosukumwa na kuongozwa kufunga!.

Lakini mbali na hilo hata kama Novena ingekuwa ni agizo la biblia, bado inavyofanyika na madhehebu baadhi ikiwemo Katoliki, bado haifanyiki sawasawa na maandiko.. Kwasababu katika biblia tunaona kabla ya Pentekoste walikuwa wamekusanyika mahali pamoja wakisali, wakimwomba Mungu na Mariamu mama yake Yesu alikuwemo miongoni mwao, naye pia akimwomba Mungu, na hawakuwa na sanamu ya mtakatifu Fulani aliyetangulia kufa!, bali walikuwa wakimwomba Mungu aliye juu, (Matendo 1:12-14)

Lakini leo hii katika sala hizo za Novena ni kinyume chake!, wanaoombwa ni watakatifu waliokufa ikiwemo Maria mwenyewe, jambo ambalo ni kinyume kabisa na maandiko!, hivyo badala ziwe sala za Baraka, zinageuka na kuwa ibada za sanamu! (Bwana Yesu atusaidie sana!!).

Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba Novena haipo kibiblia,..kama mtu atajiwekea utaratibu wake binafsi wa kusali Novena, na sala hiyo ikawa ni kulingana na Neno la Mungu, isiyohusisha sanamu wala desturi za kipagani basi hafanyi dhambi!, huenda ikawa bora kwake.

Lakini inapogeuka na kuwa sharti, na tena ikahusisha ibada za sanamu basi inakuwa ni machukizo makubwa mbele za Bwana kulingana na maandiko.

Bwana atusaidie!.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mada Nyinginezo:

SALA YA BWANA. (Namna ya kuiomba)

Ni lazima mtu aongozwe sala ya toba ili awe ameokoka?

SALA YA UPONYAJI/MAOMBI YA UPONYAJI.

Kuna tofauti gani kati ya SALA na DUA?

Ni lazima mtu aongozwe sala ya toba ili awe ameokoka?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/10/23/novena-ni-nini-na-je-ipo-kibiblia/