by Admin | 24 October 2023 08:46 pm10
(Masomo maalumu kwa watumishi wa Mungu).
Kama Mtumishi wa Mungu je unamhubiri Kristo katika Kweli yote?.
Ni rahisi kutamani na kutafuta Ishara kama njia KUU ya Kumhubiri Kristo, lakini nataka nikuambie kama utatafuta ishara halafu umeacha kumhubiri Yesu Kristo katika kweli yote, hiyo kwako ni hasara kubwa sana?
Hebu tumtazame mtu mmoja ambaye hakufanya ishara hata moja lakini alimzungumzia Kristo katika kweli yote na hiyo ikafanya kazi yake kuwa kubwa sana mbele za Mungu,…na mtu huyo si mwingine Zaidi ya Yohana Mbatizaji.
Yohana 10:40 “Akaenda zake tena ng’ambo ya Yordani, mpaka mahali pale alipokuwapo Yohana akibatiza hapo kwanza, akakaa huko.
41 Na watu wengi wakamwendea, wakasema, YOHANA KWELI HAKUFANYA ISHARA YO YOTE, LAKINI YOTE ALIYOYASEMA YOHANA KATIKA HABARI ZAKE HUYU YALIKUWA KWELI.
42 Nao wengi wakamwamini huko”
Umeona? Yohana hakufanya ishara hata moja, hakutoa pepo, hakuponya mtu kwa jina la Bwana, hakushusha moto kama Eliya ingawa roho ya Eliya ilikuwa juu yake, wala hakutembea juu ya maji ili watu waone waamini…. lakini Yote aliyoyasema kumhusu Yesu na ujio wake yalikuwa kweli, wala hakudanganya!.. Hivyo hiyo ikamfanya awe Nabii mkuu Zaidi hata ya Musa na Eliya na manabii wengine wote waliotangulia.
Luka 7:26 “Lakini, mlitoka kwenda kuona nini? Nabii? NAAM, NAWAAMBIA, NA ALIYE ZAIDI YA NABII.
27 Huyo ndiye aliyeandikiwa haya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako mbele yako.
28 Nami nawaambia, KATIKA WALE WALIOZALIWA NA WANAWAKE HAKUNA ALIYE MKUU KULIKO YOHANA; lakini aliye mdogo katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko yeye”.
Huyo ni mtu ambaye hakufanya ishara yoyote! Lakini alimzungumzia Kristo katika KWELI YOTE!.. Kwahiyo kumbe kinachojalisha ni KWELI YOTE na si Miujiza wala ishara, wala umaridadi wala utashi!, bali KWELI YOTE!.
Je wewe kama Mtumishi wa Mungu, unahubiri madhara ya dhambi na hukumu ijayo?, au unahubiri tu mafanikio na kutoa pepo?.. Je unahubiri pia Ubatizo wa maji na wa Roho Mtakatifu au unahubiri tu upendo na faraja?.. Je unahubiri juu ya unyakuo na ziwa la moto, au unahubiri tu Amani?.. Ni Vyema kuhubiri yote pasipo kuacha hata moja, na hapo tutakuwa tumemhubiri Yesu katika kweli yote.
Epuka injili za kubembeleza na kuwastarehesha watu katika dhambi, Yohana Mbatizaji alihubiri na kusema…
Luka 3:7 “Basi, aliwaambia makutano ya wale waliomwendea ili awabatize, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja?
8 BASI, TOENI MATUNDA YAPATANAYO NA TOBA; WALA MSIANZE KUSEMA MIOYONI MWENU, TUNAYE BABA, NDIYE IBRAHIMU; KWA MAANA NAWAAMBIA YA KWAMBA KATIKA MAWE HAYA MUNGU AWEZA KUMWINULIA IBRAHIMU WATOTO.
9 NA SASA HIVI SHOKA LIMEKWISHA KUWEKWA PENYE MASHINA YA MITI; BASI KILA MTI USIOZAA MATUNDA MAZURI HUKATWA NA KUTUPWA MOTONI”.
Bwana Yesu atusaidie.
Maran atha.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group
Mada Nyinginezo:
TOFAUTI YA UBATIZO WA YOHANA NA UBATIZO WA BWANA YESU
NI NINI BWANA ANATAKA KUTOKA KATIKA MUUJIZA ALIOKUFANYIA?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/10/24/je-unamhubiri-kristo-katika-kweli-yote/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.