Kumaka ni nini katika biblia? (Mathayo 8:27)

by Admin | 13 November 2023 08:46 pm11

Jibu: Neno “kumaka” limeonekana mara mbili katika biblia na maana yake ni “kushangaa/ mshangao”. Mtu anapokutana na jambo au anapoona kitu au tukio la ajabu ambalo hajawahi kuliona au kukutana nalo hapo kabla huwa anapatwa na mshangao! Sasa huo mshangao ndio unaoitwa “kumaka”.

Mathayo 8:27  “Wale watu WAKAMAKA wakisema, Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zamtii?”

Hapa wanafunzi walipomwona Bwana Yesu anazikemea pepo za bahari na kumtii, waliingiwa na mshangao wa ajabu kujiuliza yule ni mtu wa namna gani?

Utalisoma tena tukio hilo katika Luka 8:27, Lakini pia utaona Bwana Yesu alifanya mambo mengi makubwa ambayo yaliwashangaza watu wengi, (soma Marko 5:42, na Luka 4:36).

Hiyo ni kuonesha uweza wa Bwana Yesu Kristo wa kutenda miujiza ulivyokuwa Mkuu. Lakini uweza Mkuu na Muujiza Mkuu Bwana Yesu alioufanya na anaondelea kufanya leo, ambao hakuna mwingine yeyote awezaye kuufanya ni Muujiza wa KUFUTA DHAMBI!.

Miujiza mingine yote Bwana Yesu alisema nasi pia tunaweza kuifanya, lakini ule wa kusamehe dhambi ni yeye tu ndiye anayeweza kuufanya.

Marko 2:9 “Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende?

10  Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (hapo amwambia yule mwenye kupooza)”

Kwahiyo na sisi tunapaswa kuutafuta na kuupokea huu muujiza mkuu anaotoa Bwana Yesu wa kusamehewa dhambi, kwasababu kama hatutasamehewa dhambi na tukaponywa magonjwa peke yake bado haitatufaidia chochote, lakini tukipata msamaha wa dhambi hata kama tusipopokea uponyaji wowote katika mwili bado ni faida kubwa kwetu, kwasababu tutaurithi uzima wa milele.

Je! Umepokea msamaha wa dhambi zako?.. na je unaijua kanuni ya kupokea msamaha mkamilifu kutoka kwa Bwana?

Kanuni ya kupokea msamaha wa dhambi ni rahisi, nayo ni Kutubu kwa kumaanisha kuacha dhambi, kubatizwa na kupokea Roho Mtakatifu. Hatua hizo tatu ukizifuata, utapokea muujiza ambao hujawahi kuupokea katika maisha yako yote.

Matendo 2:36  “Basi nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulibisha kuwa Bwana na Kristo.

37  Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

38  Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

39  Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

NI NINI BWANA ANATAKA KUTOKA KATIKA MUUJIZA ALIOKUFANYIA?

BABA UWASAMEHE

NINI MAANA YA KUTUBU

UMEONDOLEWA DHAMBI?

TAFUTA MSAMAHA HALISI, NA SI MSAMAHA TU!

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/11/13/kumaka-ni-nini-katika-biblia-mathayo-827/