by Admin | 17 November 2023 08:46 pm11
Nakusalimu katika jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo. Nakukaribisha katika kuyatafakari maneno ya uzima.
Ulishawahi kuutafakari vema huu mstari?
Zaburi 121:5 Bwana ndiye mlinzi wako; Bwana ni uvuli mkono wako wa kuume. 6 Jua halitakupiga mchana, Wala mwezi wakati wa usiku. 7 Bwana atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako. 8 Bwana atakulinda utokapo na uingiapo, Tangu sasa na hata milele.
Ni rahisi kumwelewa mtu anayekuambia, “leo jua limenipiga”, lakini si rahisi kumwelewa mtu anayesema “leo mwezi umenipiga” Ni wazi kuwa utamwona anakuchezea akili. Si ni kweli?..Lakini hapa katika vifungu hivi ambavyo Mungu anaeleza ulinzi wake kwa watu wake jinsi ulivyo, anatumia mifano hiyo miwili ya jua na mwezi. Na anaonyesha kuwa kama vile jua linavyompiga mtu, ndivyo na mwezi nao unavyompiga mtu.
Akiwa na maana gani?
Tunajua kuwa mwezi hauna nguvu yoyote ya kumuunguza mtu au kumchosha, tofauti na jua. Lakini Mungu anaona hata mwangaza tu huo wa mwezi ni pigo kwa mtu. Akiwa na maana si katika mateso magumu, au dhiki kubwa zinazoonekana kwa macho ndio anazoshughulika nazo Mungu, lakini pia hata katika zile ndogo sana, ambazo unaweza kuona zikiendelea kuwepo hazina madhara yoyote kwako, Bwana anakulinda nazo.
Kwamfano wewe huwezi kuona umepata hasara pale nywele yako moja imepungua kichwani mwako, tena si rahisi kugundua, lakini yeye anaithamini na ndio maana amezihesabu zote. Ikidondoka moja tu, anaona mapungufu, umekutana na mateso..
Mathayo 10:30 lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote.,
Vivyo hivyo rohoni, unaweza kumwomba Mungu, niepushe na majaribu, kichwani kwako ukafikiri hili na hili labda magonjwa, umaskini, vita, vifungo,ajali, kuteswa kwasababu ya imani, N.K. ndio Bwana anashughulika navyo hivyo kukulinda, au kukupa nguvu ya kuvishinda. Lakini anahakikisha hata zile honi za magari unazopishana nazo barabarani, haziyaharibu masikio yako, jani ulilokanyaga jana, halijaharibu mguu wako, bacteria walio katika mikono yako, hawaui seli za ngozi, idadi ya minyoo walio tumboni mwako, hawaendi kula maini na figo zako, kiwembe kinachopita kichwani mwako kila siku haking’oi mizizi ya nywele, n.k…Haya mambo unaweza kuona ni ya kawaida tu, lakini Bwana akitoa mkono wake umeisha.
Kwa ufupi ni kuwa zipo Nyanja nyingi sana za hatari, ambazo Bwana anatuepusha nazo, Ndio maana tunapaswa tuwe waombaji sikuzote, unapojiona upo salama, omba, unapojiona upo kwenye matatizo omba, muda wote dumu uweponi mwa Bwana. Hata kama utaona kama majaribu yamekulemea, Bwana ameahidi ushindi mwishoni, Ayubu alilemewa na mateso lakini mwishoni alirejeshewa mara dufu.
Ulinzi wa Mungu ni uhakika kwa watu wake, dumu katika katika maombi ili Bwana apate nafasi ya kutulinda vema, nyakati za jua na nyakati za mwezi. (Mathayo 26:41)
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group
Mada Nyinginezo:
MAJARIBU MATANO (5) YA MKRISTO.
Je! Siku ilihesabiwaje kabla ya jua na mwezi kuumbwa?
UWEZA WA MUNGU UNAONEKANA WAPI?
Mwandamo wa mwezi/Mwezi mpya Ni nini kibiblia?
Kumaka ni nini katika biblia? (Mathayo 8:27)
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/11/17/jua-halitakupiga-mchana-wala-mwezi-wakati-wa-usiku/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.