MIEZI 13 YA KIYAHUDI.

MIEZI 13 YA KIYAHUDI.

Tofauti na Kalenda ya Kirumi ambayo ndiyo tunayoitumia sasa yenye miezi 12, Kalenda ya kiyahudi yenyewe inakuwa na miezi 13 kwa mara saba kila baada ya miaka 19. (Yaani katika kipindi cha miaka 19, miaka 7 inakuwa na miezi 13, na miaka 12 iliyosalia inakuwa na miezi 12 kama kawaida), Na miaka yenye miezi 13 ni inakuwa ni mwaka wa 3, 6,8,11,14, 17 na 19 na mzunguko wa miaka 19, unapoisha na unapoanza mzunguko mwingine, basi mgawanyo wa miezi unakuwa ni huo huo, wa baadhi ya miaka kuwa na miezi 13 na mingine 12.

Sasa mwezi wa 13, unaoongezeka juu ya miezi 12 ya kiyahudi ni mwezi ujulikanao kama Adari II, Sasa kabla ya kwenda kuutazama huu mwezi wa 13 wa Adari, hebu tuitazame miezi 12, na rejea zao katika biblia.

Mwezi wa 1: Abibu au Nisani.

Mwezi wa Abibu au Nisani ni mwezi wa kwanza katika kalenda ya kiyahudi, mwezi huu unaanza katika mwezi Machi katikati na kuisha mwezi Aprili katikati katika kalenda yetu ya kirumi tunayoitumia..

Mwezi wa Abibu ndio mwezi ambao wana wa Israeli walitoka Misri..

kutoka 13:3 Musa akawaambia hao watu, Kumbukeni siku hii, mliyotoka nchi ya Misri, kutoka nyumba ya utumwa; kwa kuwa Bwana aliwatoa mahali hapa kwa nguvu za mkono wake; na usiliwe mkate uliochachwa.

 4 Ninyi mwatoka leo katika MWEZI WA ABIBU.

Na wakati ambapo Hamani ananyanyuka kutaka kuwaangamiza Israeli yote katika ufalme wote wa Ahasuero, tunasoma wazo hili lilimjia katika Mwezi wa Nisani/ Abibu..

Esta 3:7 “Basi mwezi wa kwanza, ndio MWEZI WA NISANI, mwaka wa kumi na mbili wa mfalme Ahasuero, wakapiga Puri, yaani kura, mbele yake Hamani; siku kwa siku, na mwezi kwa mwezi, hata mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari”.

Na pia tunausoma huu mwezi ukitajwa wakati Nehemia alipoingiwa na wazo la kwenda kuujenga Yerusalemu..

Nehemia 2:1 “Ikawa katika MWEZI WA NISANI, mwaka wa ishirini wa mfalme Artashasta, na divai imewekwa mbele yake, nikaishika ile divai, nikampa mfalme. Nami mpaka sasa sikuwa na huzuni mbele ya mfalme wakati wo wote.”.

 Mwezi wa 2: Zivu au Ayari

Mwezi huu unaangukia kati ya mwezi Aprili na mwezi May kwa kalenda yetu tunayoitumia, na ni mwezi wa pili katika kalenda ya kiyahudi.

Mwezi huu ndio mwezi ambao Mfalme Sulemani alianza kulijenga Hekalu la Mungu katika Yerusalemu..

1Wafalme 6:1 “Ikawa katika mwaka wa mia nne na themanini baada ya kutoka wana wa Israeli katika nchi ya Misri, katika mwaka wa nne wa kutawala kwake Sulemani juu ya Israeli, katika MWEZI WA ZIVU, ndio mwezi wa pili, akaanza kuijenga nyumba ya Bwana.

 2 Nayo nyumba hiyo mfalme Sulemani aliyomjengea Bwana, urefu wake ulikuwa mikono sitini, na upana wake ishirini, na kwenda juu kwake mikono thelathini”.

Mwezi wa 3: Siwani

Huu ni mwezi wa tatu kwa kalenda ya kiyahudi, lakini kwa kalenda yetu ni mwezi unaoangukia kati ya mwezi Mei na mwezi Juni.

Katika mwezi huu ndio mwezi ambao Mfalme Ahasuero, enzi za malkia Esta alitoa ruksa kwa wayahudi kujilipizia kisasi juu ya adui zao.

Esta 8:9 “Basi, waandishi wa mfalme wakaitwa pale pale, siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa tatu, ndio MWEZI WA SIWANI; na kama vile Mordekai alivyoamuru, Wayahudi wakaandikiwa, pamoja na maakida na maliwali, na wakuu wa majimbo toka Bara Hindi mpaka Kushi, majimbo mia na ishirini na saba, kila jimbo kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake; na Wayahudi kwa mwandiko wao na kwa lugha yao”.

Mwezi wa 4: Tamuzi

Huu ni mwezi wa Nne katika kalenda ya kiyahudi, lakini kwetu sisi unaanguka katika ya mwezi Juni na mwezi Juni na mwezi Julai.

Mwezi huu katika bibli unaonekana kutajwa mara moja tu katika kitabu cha Ezekieli.

Ezekieli 8:14 “Ndipo akanileta mpaka mlango wa kuingilia katika nyumba ya Bwana, ulioelekea upande wa kaskazini, na tazama, wanawake wameketi wakimlilia TAMUZI”.

Mwezi huu wa nne umetajwa sehemu nyingine kama kwa namba na si kwa jina (Soma Yeremia 39:1-2, na Yeremia 52:6-7).

Mwezi wa 5: Avu

Huu ni mwezi wa tano kwa wayahudi na kwetu sisi unaangukia kati ya mwezi wa Julai na Mwezi Agosti.. Mwezi huu katika biblia haijatajwa kwa jina bali kwa namba..

Kwamfano tunasoma Ezra aliwasili Yerusalemu katika mwezi wa 5

Ezra 7:8 “Naye Ezra akafika Yerusalemu mwezi wa tano katika mwaka wa saba wa huyo mfalme”

Na pia katika (2 Wafalme 25:8-10, Yeremia 1:3 na Yeremia 52:12-30)

Mwezi wa 6: Eluli

Huu ni mwezi wa 6 kwa kalenda ya kiyahudi na unaangukia kati ya mwezi wa Agosti na Septemba katika kalenda yetu.

Katika biblia mwezi huu ndio mwezi ambao Nehemia alimaliza kati ya kuukarabati ukuta Yerusalemu..

Nehemia 6:15 “Basi huo ukuta ukamalizika siku ya ishirini na tano ya mwezi wa ELULI, katika muda wa siku hamsini na mbili”

Mwezi huu pia umetajwa kwa namba katika kitabu cha Hegai 1:14-15.

Mwezi wa 7: Ethanimu

Huu ni mwezi wa 7 kwa kalenda ya kiyahudi na kwa kalenda yetu unaangukia katika ya mwezi wa Septemba na Oktoba.

Hekalu la Sulemani liliwekwa wakfu katika mwezi huu wa Ethanimu

1Wafalme 8:1 “Ndipo Sulemani alipowakusanya wazee wa Israeli, na wakuu wote wa kabila, wakuu wa mbari za mababa wa wana wa Israeli, wamwendee mfalme Sulemani huko Yerusalemu, ili walipandishe sanduku la agano la Bwana kutoka mji wa Daudi, yaani, Sayuni. 

2 Wakakutana mbele ya mfalme Sulemani watu wote wa Israeli wakati wa sikukuu, katika MWEZI WA ETHANIMU, ndio mwezi wa saba.  3 Wazee wote wa Israeli wakaja, nao makuhani wakajitwika sanduku”

Unaweza kuusoma pia mwezi huu katika..(1Wafalme 8:2, Walawi 23:24, Nehemia 8:13-15).

Mwezi wa 8: Buli.

Mwezi huu ni mwezi wa 8 kwa kalenda ya kiyahudi na unaangukia kati ya mwezi Octoba na mwezi mwezi Novemba katika kalenda yetu ya kirumi.

Katika mwezi huu ndio mwezi ambao Sulemani alimaliza kuijenga nyumba ya Mungu (Hekalu).

1Wafalme 6:38 “Hata katika mwaka wa kumi na mmoja, katika MWEZI WA BULI, ndio mwezi wa nane, nyumba ikaisha, mambo yake yote, na sharti zake zote. Basi muda wa miaka saba alikuwa katika kuijenga.

Unaweza kusoma pia habari za mwezi huu katika  (1Wafalme 12:32-33, 1Nyakati 27:11).

Mwezi wa 9: Kisleu

Huu ni mwezi wa 9 kwa kalenda ya kiyahudi na unaangukia kati ya mwezi wa Novemba na Disemba katika kalenda yetu ya sasa ya kirumi.

Katika mwezi huu Nabii Zekaria alioneshwa maono juu ya Yuda na Israeli.

Zekaria 7:1 “Ikawa katika mwaka wa nne wa mfalme Dario, neno la Bwana lilimjia Zekaria, siku ya nne ya mwezi wa kenda, yaani, KISLEU”

Mwezi wa 10: Tebethi

Huu ni mwezi wa 10 kwa Wayahudi na kwa kalenda ya kirumi unaangukia kati ya mwezi Disemba na January.

Katika biblia mwezi huu ndio mwezi ambao Esta aliingizwa katika nyumba ya kifalme..

Esta 2:16 “Basi Esta alipelekwa kwa mfalme Ahasuero, katika nyumba ya kifalme, mwezi wa kumi, ndio mwezi wa Tebethi, mwaka wa saba wa kumiliki kwake. 

17 Mfalme akampenda Esta kuliko wanawake wote, naye akapata neema na kibali machoni pake kuliko mabikira wote; basi akamtia taji ya kifalme kichwani pake, akamfanya awe malkia badala ya Vashti”.

Na ndio mwezi ambao Nebukadreza aliuhusuru Yerusalemu (2Wafalme 25:1, Yeremia 52:4).

Mwezi wa 11: Shebati

Mwezi huu unaangukia kati ya mwezi Januari na mwezi Februari kwa kalenda ya kirumi na katika kalenda ya kiyahudi ni mwezi wa 11.

Katika mwezi huu ndio mwezi ambao Zekaria aliona maono tena juu ya Yerusalemu..

Zekaria 1:7 “Siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, yaani, mwezi uitwao Shebati, katika mwaka wa pili wa Dario, neno la Bwana lilimjia Zekaria, mwana wa Berekia, mwana wa Ido, nabii, kusema,

 8 Naliona wakati wa usiku, na tazama, mtu amepanda farasi mwekundu, akasimama kati ya mihadasi iliyokuwa mahali penye uvuli; na nyuma yake walikuwapo farasi wengine wekundu, na wa rangi ya kijivujivu, na weupe”.

Mwezi wa 12: Adari I.

Huu ni mwezi wa 12 na wa mwisho kwa kalenda za kiyahudi, ambapo kwa kalenda ya kirumi unaangukia kati ya Mwezi Februari na mwezi Machi.

Esta 3:7 “Basi mwezi wa kwanza, ndio mwezi wa Nisani, mwaka wa kumi na mbili wa mfalme Ahasuero, wakapiga Puri, yaani kura, mbele yake Hamani; siku kwa siku, na mwezi kwa mwezi, hata mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari”.

Kutokana na kuwepo na miaka mirefu na mifupi, Marabi wa kiyahudi katika karne ya 4, wakiongozwa na Rabbi Hillel II, waliongeza mwezi mmoja wa 13, katika kalenda ya kiyahudi ambao waliuita mwezi ADARI II (Adari wa pili).

Lengo la kuongeza mwezi huu ni ili kuziweka sikukuu za kiyahudi katika majira halisia, vinginevyo sikukuu za kiyahudi zingeangukia misimu ambayo sio, kwamfano sikukuu ya pasaka ambayo kwa wayahudi inaseherekewa katika mwezi wa March au April kwa kalenda yetu, kama kusingekuwepo huu mwezi wa 13, basi huenda miaka mingine sikukuu hii ingeangukia mwezi wa 8 kwa kalenda yetu, jambo ambalo lingekuwa halina uhalisia hata kidogo.

Lakini swali ni je!, sisi wakristo tunapaswa kuifuata kalenda ipi?, ya kiyahudi au hii inayotumika sasa ya kirumi?

Jibu ni kuwa Kalenda hazitusogezi karibu na Mungu wala hazipeleki mbali na Mungu,  tukitumia kalenda ya kiyahudi, au ya kirumi au ya kichina au hata ya kichaga haituongezei chochote, kilicho cha muhimu ni kuishi kwa kuukomboa wakati kama biblia inavyosema katika..

Waefeso 5:15 “Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima;

16 mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu”

Na tunaukomboa wakati kwa kufanya yale yanayotupasa kufanya, ikiwemo Kujitakasa, kufanya ibada, kuomba, kusoma Neno, kuifanya kazi ya Mungu kupitia karama iliyo ndani yako kabla ya ule mwisho kufika na mambo mengine yote yanayohusiana na hayo.

Bwana akubariki.

Maran atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Mwandamo wa mwezi/Mwezi mpya Ni nini kibiblia?

UWEZA WA MUNGU UNAONEKANA WAPI?

Je! kuna sikukuu za pasaka mbili? (Hesabu 9:11)

Je! ni sahihi kwa Mkristo kusherekea siku yake ya kuzaliwa.[Birth day]?

Nini maana ya wokovu watoka kwa Wayahudi? (Yohana 4:22)

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Edward mdimi
Edward mdimi
2 months ago

Nimebarikiwa mbarikiwe saa