Mwandamo wa mwezi/Mwezi mpya Ni nini kibiblia?

Mwandamo wa mwezi/Mwezi mpya Ni nini kibiblia?

Katika biblia ukiona neno “mwandamo wa mwezi”, au “mwezi mpya”, ujue ni neno lile lile moja linalomaanisha “siku ya kwanza ya mwezi”.

Katika agano la kale siku hii iliheshimiwa na kufanywa kama mojawapo ya siku takatifu, kama  tu vile ilivyokuwa  siku ya sabato, ambayo ni siku ya saba. Vivyo hivyo kila siku ya kwanza ya mwezi mpya, tarehe moja (kwa kalenda ya kiyahudi), ilikuwa ni takatifu kwao, na ni lazima watu wakamtolee Mungu sadaka za kuteketezwa, Sadaka za unga na vinywaji,  Pamoja na kupiga tarumbeta juu ya sadaka hizo, (Hesabu 28:11-15), .Vilevile hukuruhusiwa kufanya shughuli yoyote au biashara yoyote(Nehemia 10:31-33)

Hesabu 28:11 “Tena katika mianzo ya miezi yenu mtamsongezea Bwana sadaka ya kuteketezwa; nayo ni ng’ombe waume wadogo wawili, na kondoo mume mmoja, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza, wakamilifu, saba;

12 pamoja na sehemu ya kumi tatu za efa za unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na mafuta, kwa kila ng’ombe; na sehemu ya kumi mbili za unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na mafuta, kwa huyo kondoo mume mmoja;”

Hesabu 10:10 “Tena katika siku ya furaha yenu, na katika sikukuu zenu zilizoamriwa, na katika kuandama miezi kwenu, mtapiga hizo tarumbeta juu ya sadaka zenu za kuteketezwa, na juu ya dhabihu za sadaka zenu za amani; nazo zitakuwa kwenu ni ukumbusho mbele za Mungu wenu; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu”.

Lakini kuna wakati wayahudi, walizifanya sikukuu hizo kama mazoea tu, wakawa hawazitoi katika utakatifu, bali kama agizo tu la kidini  na huku nyuma mioyo yao ipo mbali na Mungu, hivyo hiyo ikamfanya  Mungu akasirishwe nao na hatimaye kuzitaa sikukuu zao hizo za mwandamo wa mwezi.

Isaya 1:13 “Msilete tena matoleo ya ubatili; uvumba ni chukizo kwangu; mwezi mpya na sabato, kuita makutano; siyawezi maovu hayo na makutano ya ibada.

14 Sikukuu zenu za mwezi mpya na karamu zenu zilizoamriwa, nafsi yangu yazichukia; mambo hayo yanilemea; nimechoka kuyachukua”.

Neno hili utalisoma pia katika vifungu hivi;

Zaburi 81:3 “Pigeni panda mwandamo wa mwezi, Wakati wa mbalamwezi, sikukuu yetu”.

1Samweli 20:5 “Naye Daudi akamwambia Yonathani, Tazama, kesho ni mwandamo wa mwezi, nami hainipasi kukosa kuketi chakulani pamoja na mfalme; lakini niache nijifiche bondeni hata siku ya tatu jioni.

Soma pia, 2Nyakati 2:4, 8:13, Ezra 3:5, Hosea 2:11.

Lakini je! Sheria hii bado inaendelea hadi sasa?

Jibu ni la! Kama tu vile hatujapewa takwa la kuitunza sabato kama sheria , vivyo hivyo, na katika mwandamo wa mwezi mpya.

Wakolosai 2:16 “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato;

17 mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo”.

Lakini Bwana anatufundisha nini katika agizo hili alilowapa?

Ni kwamba tuthaminishe nyakati zetu mpya kwake. Wiki yako inapoisha na kuanza nyingine bila kumfanyia Mungu wako ibada, ni hatari kubwa sana, kama kwako  ni jumapili, au jumamosi, ndio unamfanyia Mungu ibada, hakikisha unakutanika na wengine, kumwabudu Mungu wako, usiruhusu wiki yako ipite hivi hivi tu.

Halikadhalika, mwezi wako mpya unapoanza, usianze hivi hivi tu, bali chukua muda kwenda kumshukuru Mungu nyumbani kwake, ni muhimu sana. Ukiona wiki yako inapita hivi hivi tu, mwezi wako unapita hivi hivi tu, mwaka wako unapita hivi hivi tu, huna Habari na Mungu. Angalia  Maisha yako ni lazima yatakuwa na kasoro Fulani tu.

Hivyo tujitahidi sana, tusiwe na mapengo pengo kwa Mungu wetu.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

SIKUKUU 7 ZA KIYAHUDI ZINAFUNUA NINI KWETU?

SABATO ILIFANYIKA KWAAJILI YA MWANADAMU NA SI MWANADAMU KWAAJILI YA SABATO!

Sadaka ya kutikiswa ilikuwaje?

MWEZI WA ABIBU/NISANI NI MWEZI GANI?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments