ZIFAHAMU KARAMA 9 ZA ROHO MTAKATIFU NA UTENDAJI KAZI WAKE.

by Admin | 21 February 2024 08:46 pm02

Karama tisa (9) za Roho mtakatifu tunazisoma katika kitabu cha 1Wakorintho 12.

Tusome,

1Wakorintho 12:4  “Basi pana tofauti za KARAMA; bali Roho ni yeye yule.

5  Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule.

6  Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.

7  Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.

8  Maana mtu mmoja kwa Roho apewa NENO LA HEKIMA; na mwingine NENO LA MAARIFA, apendavyo Roho yeye yule;

9  mwingine IMANI katika Roho yeye yule; na mwingine KARAMA ZA KUPONYA katika Roho yule mmoja;

10  na mwingine MATENDO YA MIUJIZA; na mwingine UNABII; na mwingine KUPAMBANUA ROHO; mwingine AINA ZA LUGHA; na mwingine TAFSIRI ZA LUGHA;

11  lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye”.

Tuangalie utendaji kazi wa moja baada ya nyingine.

      1. NENO LA HEKIMA.

Hii ni karama ya upambanuzi wa jambo lililo gumu kutatulika.. Kwamfano kunaweza kutokea jambo katika kanisa ambalo ni gumu sana kutatulika au kufahamika, (fumbo kubwa)..sasa mtu mwenye karama hii ya Neno la Hekima anaweza kulijua jambo hilo na kulitatua, au kutoa mapendekezo ya kulitatua kwa njia ya mafundisho au matendo..

Mfano wa mtu aliyekuwa na karama hii ni Sulemani..

Watu wenye karama hii wakiwemo ndani ya kanisa, basi ndoa nyingi zitasimama, na wizi na mambo ya kando kando hayataweza kupata nafasi kwasababu yatawekwa wazi.

     2. NENO LA MAARIFA.

Hii ni karama ya MAARIFA kama jina lake lilivyo.. Mtu mwenye karama hii anakuwa na uwezo mkubwa wa kujua mambo mengi..ya kidunia na kibiblia.. (Maarifa aliyonayo kuhusu biblia yanamtofautisha na mtu mwingine).. Vile vile maarifa anayokuwa nayo juu ya mambo mengine ya ulimwengu yanamtofuatisha na mkristo mwingine.

Watu wenye karama hii wakiwemo ndano ya kanisa, mafundisho ya manabii wa uongo ni ngumu kupata nafasi, (kwasababu manabii wa uongo wanawadanganya watu wasio na maarifa ya kutosha) sasa wakiwepo watu wenye karama hii ya maarifa, basi wanaweza kulifundisha kundi au kulielekeza mambo mengi kiusahihi kabisa.

Lakini wakikosekana ndio linatimia lile Neno “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa (Hosea 4:6)”

     3. IMANI

Hii ni karama ya kutenda matendo ya Imani.. Watu wenye karama hii katika kanisa ni wale wenye kutenda au kuhamasisha watu katika kanisa kufanya matendo ya Imani. Na maisha yao yote yakijaa matendo ya Imani.

Huwa hawaogopi magonjwa, changamoto, wala dhoruba yoyote.. Kukitokea hofu wamesimama imara!, kanisa likiishiwa nguvu, watu wenye hii karama wanalitia nguvu na kulihamasisha..

Watu kama hawa wakiwepo katika kanisa basi kanisa hilo haliwezi kupungua nguvu ya kuendelea mbele, wala watu wake hawawezi kukata tamaa daima.

     4. KARAMA ZA KUPONYA.

Zinaitwa “Karama za kuponya” na si “Karama ya kuponya”… Maana yake ni Karama hii inafanya kazi ya kuponya vitu vingi, ikiwemo magonjwa, maisha, roho, nafsi na vitu vingine vilivyoharibika.

Mtu mwenye karama hii anakuwa na uwezo wa kumwombea mtu na akapona kirahisi, au kumfundisha mtu na akapokea uponyaji kirahisi.. Vile vile ana uwezo wa kumwekea mtu mikono akapokea uponyaji kirahisi ikiwa ana ugonjwa au maisha yake yameharibika.

Vile vile anaweza kumfundisha mtu na mtu yule akaponyeka roho yake na majeraha ya adui.

Vile vile kama kazi ya mtu au maisha yake yameharibika mtu mwenye karama hii anaweza kumjenga upya kwa kumfundisha au kumwombea na mtu yule akaponyeka kabisa kabisa dhidi ya mapigo yote ya yule adui.

Watu kama wenye karama hii wakiwemo ndani ya kanisa, basi kanisa hilo litakuwa na watu wanaosimama kila siku na hakuna atakayekuwa anaanguka.

     5. MATENDO YA MIUJIZA.

Hii ni karama ya Ishara ndani ya kanisa. Watu wenye karama hii ni wale ambao maisha yao yamejaa miujiza na ishara.. Wakiwemo ndani ya kanisa basi ni lazima kuna miujiza itaonekana ambayo itawashangaza wengi na kuwafanya waaamini mahali pale kuna Mungu.

Kuna watu wakiingia mahali au wakienda mahali lazima kuna tukio la ajabu litatokea pasipo hata kupanga au kusema (ni ishara ambazo zinafuatana nao).

Kunatokea ajali ghafla anatoka mzima bila dhara lolote.. hajala wiki 2 lakini bado anaonekana ana nguvu zile zile.. Anafika mahali kivuli chake kinaponya watu.. anaimba tu au anaongea!, watu wanajazwa Roho Mtakatifu n.k

Watu wa namna hii kwa ufupi, wanakuwa wanafanya vitu vya ajabu, na kuwa na matukio mengi ya kushangaza shangaza na wengi wenye karama hii wanakuwa na vipindi vya kukutana/kutokewa na malaika. Yote ni kwa lengo la kuthibitisha uwepo wa Mungu katika kanisa.

     6. UNABII

Hii ni karama inayohusika na kutabiri mambo yajayo au yanayoendelea sasa, au kuelezea yaliyopita.

Watu wenye karama hii wanakuwa na uwezo wa kuona mambo yajayo ya Mtu, Watu, kanisa au Taifa. Na nabii zao zinaegemea biblia. Na Mungu anawafunulia kwa njia aidha ya Ndoto, Neno au Maono.

Pia wana uwezo wa kumfundisha na kumwombea mtu au kumshauri kuhusiana na kile walichooneshwa! (kilichopita, kinachooendelea au kijacho).

Watu wenye karama hii wakiwemo ndani ya kanisa basi kanisa litasimama na kuendelea.

    7. KUPAMBANUA ROHO.

Hii ni karama ya kupambanua au kuzijaribu roho. Mtu mwenye karama hii anakuwa mwepesi wa kuzitambua roho (kama ni roho wa Mungu au roho nyingine).

Kama kuna roho ya uchawi inaingia basi anakuwa na uwezo wa kupambanua, kama ni roho ya uzinzi, wizi, uadui, fitina, n.k anakuwa na uwezo wa kuiona kabla ya wengine na hivyo kutoa mashauri au kuomba iondoke.

Vile vile mtu mwenye karama hii anakuwa na uwezo wa kujua utendaji kazi wa Roho Mtakatifu, ni rahisi kujua karama za watu katika migawanyo yake..(kwamba huyu ana karama hii na yule ile).. Na pia anakuwa na uwezo mkubwa wa kufundisha juu ya karama za roho.

Watu wenye karama hii wakiwemo ndani ya kanisa.. ni ngumu sana kanisa hilo kushambuliwa na roho nyingine..

     8. AINA ZA LUGHA.

Hii ni karama ya ishara ndani ya kanisa, ambayo madhumuni yake ni kama yale ya karama ya MIUJIZA.

Mtu mwenye karama ya lugha, anakuwa na uwezo wa kuzungumza lugha nyingi kimiujiza, (lugha za rohoni na za mwilini).. Lugha za rohoni ambazo (maarufu kama kunena kwa lugha).. mtu anakuwa na uwezo wa kuzinena na wakati mwingine kutoa tafsiri zake.

Lakini Zaidi sana anakuwa na uwezo wa kunena lugha nyingine za jamii nyingine.. Pindi anapojaa Roho Mtakatifu anajikuta anauwezo wa kunena lugha ya taifa lingine au kabila lingine ambalo sio lake, tena anazungumza vizuri sana.

Na watu wa wanapoona huyu mtu hajasoma kabisa lakini anaongea kiingereza kizuri namna hiyo, basi wanamshangaa Mungu na kumtukuza na kumwamini, na baadaye yule mtu akimaliza kunena basi anarudi katika hali yake ya kawaida ya kuongea lugha yake ya asili.

Watu wenye karama hii wakiwepo ndani ya kanisa..basi hofu ya Mungu inaongezeka na kuthibitisha kuwa Mungu yupo katikati ya kanisa lake.

     9. TAFSIRI ZA LUGHA.

Hii ni karama ya 9 na ya mwisho iliyotajwa katika orodha hii..  Karama hii inahusiana pakubwa sana na ile ya “Aina za lugha”.. Kwani mwenye karama ya Aina za lugha, mara nyingine atamwitaji huyu mwenye Tafsiri za lugha ili aweze kutafsiri kinachozungumzwa.. ili kanisa lisiingie katika machafuko. (Soma 1Wakorintho 14:27).

Hizi ndizo karama 9 maarufu katika biblia. Zipo karama nyingine kama za kukirimu, au Uimbaji hizo zinaangukia katika kundi la huduma ya UINJILISTI, Mtu anayeimba anafanya uinjilisti, hivyo ni mwinjilisti!.

Na mtu anaweza kuwa na karama Zaidi ya moja, (Maana yake mtu anaweza kuwa na karama ya Imani na pia ya kinabii au ya Aina za Lugha, na Tafsiri za lugha hapo hapo) ingawa jambo hilo linakuwa ni nadra sana!…. Lakini Roho Mtakatifu ndiye anayemgawia mtu na si mtu anajipachikia!.

Na kumbuka!. Karama za Roho Mtakatifu ni kwa lengo la kufaidiana na si kuonyeshana au biashara.. Karama nyingi shetani kaziua kwa njia hiyo (anawapachikia watu kiburi, au kupenda sifa na utukufu na fedha).. mwisho wa siku kile kipawa kinazima!.

Ili kufufua karama iliyozima, njia ni kujishusha, kuwa mnyenyekevu, vile vile uwe na nia ya Kristo ya kulijenga kanisa, na pia ukubali na uheshimu kujengwa na karama nyingine, lakini ukijiona wewe ni wewe huhitaji wengine, fahamu kuwa hata cha kwako hakitaweza kufanya kazi.

Kanisa la siku za mwisho, tuna tatizo kubwa sana wa kuruhusu utendaji kazi wa Roho Mtakatifu kupitia karama zilizowekwa ndani yetu.. Na tatizo kubwa lipo kwa “viongozi” na “wasio viongozi (washirika)”.

Viongozi wengi hawaruhusu vipawa hivi vitende kazi aidha kutokana na wivu, au kutokuwa na maarifa ya kutosha kuhusiana na vipawa hivyo…

Lakini pia na watu wengine ndani ya kanisa (washirika) wanaoujenga mwili wa Kristo. Wanapokataa kujishughulisha vya kutosha na mwili wa Kristo, basi vile vipawa vilivyopo ndani yao vinazima, na hivyo kanisa linabaki na karama moja au mbili zinazofanya kazi.

Fahamu kuwa unapoenda kanisani, unacho kitu cha kiroho kwaajili ya ule mwili.. Ni wajibu wako kupambana mpaka kitokee, na kionekanane na kifanye kazi…usinyooshee tu kidole, wala usilaumu tu, na wakati huo wewe mwenyewe karama imekufa ndani yako (hujijui wewe ni nani/wala nafasi yako ni ipi), kanisani unaenda tu kama mtu anayeangalia Tv asiyehusika na mambo yanayoendelea kule (Hiyo haifai kabisa kwa mkristo aliyeokoka).

Ukiambiwa uombe huombi!! Karama yako itatendaje kazi ndani yako??,..ukiambiwa ufunge hufungi!! kuhudhuria tu kwenye ibada ni lazima ukumbushwe kumbushwe!..na bado unalaumu kanisani hakuna karama?..hiyo karama ipo kwa nani kama si ndani yako, na wewe umeiua kwa ukaidi wako???

Katika nyumba ya Mungu kila mtu lazima awe kiungo, ndipo udhihirisho mkamilifu wa Roho utaonekana.

Bwana akubariki na atusaidie.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

NITAIFAHAMU VIPI KARAMA YANGU?.

JE! KARAMA NI UTHIBITISHO WA KUWA NA MUNGU?

USIJISIFIE KARAMA KWA UONGO.

Karama ya pili inayozungumziwa katika 2Wakorintho 1:15 ndio ipi?

JE! NI LAZIMA WATU WOTE WANENE KWA LUGHA?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/02/21/zifahamu-karama-9-za-roho-mtakatifu-na-utendaji-kazi-wake/