by Admin | 2 March 2024 08:46 am03
Swali: Kwanini tutoe sadaka? Na Je ni lazima kutoa sadaka?..Na mtu asipotoa sadaka ni dhambi?
Jibu: “Utoaji” (uwe wa sadaka au wa kitu kingine chochote) ni wajibu wa kila “Mwamini”.. Mtu ambaye si mtoaji bado hana badiliko la kweli ndani yake!…na wala Mungu hayupo ndani yake.
Sasa kwanini tunatoa sadaka? Na kwanini mtu ambaye si mtoaji hana Mungu ndani yake?
Jibu, Tunatoa sadaka kwasababu Mungu naye ni Mtoaji (vyote tunavyonufaika navyo ni yeye katupa bure bila gharama). Na kwanini Mungu awe mtoaji na sisi tuwe watoaji?.. Ni kwasababu tumeumbwa kwa sura na Mfano wake! (Mwanzo 1:26).
Kama mtu hatoi maana yake ule mfano wa Uungu ndani yake haupo kwasababu Mungu sifa yake kuu ni utoaji!.. Ametoa uzima bure, ametoa maisha bure Zaidi sana ametupa uzima wa milele bure kupitia kumtoa mwanawe wa pekee (Yohana 3:16) na mambo mengine mengi.. Hivyo na sisi ni lazima tuwe kama yeye…ndivyo maandiko yanavyotuambia.
Mathayo 5:48 “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu”.
Na kutoa ni “Wajibu” Zaidi ya “Agizo”.. Mtu anayejua wajibu wake, hakumbushwi kumbushwi, halazimishwi lazimishwi wala hasukumwi sukumwi.. Anatimiza wajibu wake kwasababu anajua pia ni kwa faida yake.
Ukiona utoaji ni sheria ngumu kwako, kwamba unaona uchungu kumtolea Mungu.. au unaona kama unafilisika, au unaonewa au unadhulumiwa wahi kutafuta msaada kutoka kwa BWANA, Mlile mwambie aiondoe hiyo roho ndani yako kwasababu ndio roho ile ile iliyokuwa ndani ya Kaini alipoona kumtolea Mungu sehemu ya kwanza ya vitu vyake ni hasara kubwa!.. na kwasababu anasukumwa sukumwa na sheria ya utoaji, akalazimika kumtolea Mungu sehemu hafifu na sadaka zake na hivyo zikakataliwa.
Mungu anayekupa pumzi na maisha bure unaonaje uchungu kumtolea sehemu ya kumi tu! Na sehemu 9 zilizosalia zibaki kwako?.. Huoni kuna shida kama unaona uchungu kwa hicho kidogo?..
Mungu unayekanyaga ardhi yake bure, unayevuta hewa yake bure tangu umezaliwa, unayefurahia jua lake bure bila kulipia hata mia, na wakati huo huo unawalipa tanesco fedha nyingi kwa kukupatia tu kanuru kadogo wakati wa usiku.. Huyo Mungu akupaye hayo yote, unamwonea uchungu na hata kumwibia, na ukiambiwa kuhusu kumtolea unaona unafilisiwa na kudhulumiwa, utaachaje kuwa kama KAINI WEWE!!. Moyo wako hauwezi kuwa kwa MUNGU Kamwe!, haijalishi utakuwa unaomba sana wewe bado utakuwa mnafiki.
Usikwepe kumtolea Mungu na tena ifanye kuwa ni wajibu, na si Agizo wala Amri!. Na madhara ya kutomtolea Mungu (kukwepa wajibu) yanapatikana katika Mathayo 25:41-46
+255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine:
Kwanini Sadaka ya Kaini ilikataliwa? (Mwanzo 4:5).
SADAKA INAHARIBU NGUVU ZA MADHABAHU ZA MASHETANI.
Sadaka ya kinywaji ilikuwaje? Na inawakilisha nini?.
Chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu ndio kipi? (Matendo 21:25).
Ipi tofauti kati ya matoleo na sadaka?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/03/02/kwanini-tunatoa-sadaka/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.