SADAKA INAHARIBU NGUVU ZA MADHABAHU ZA MASHETANI.

SADAKA INAHARIBU NGUVU ZA MADHABAHU ZA MASHETANI.

(Masomo maalumu yahusuyo matoleo  na sadaka).


Karibu tujifunze bible, Neno la Mungu wetu lililo mwanga wa Njia yetu na Taa iongozayo miguu yetu (Zab. 119:105).

Kuna umuhimu mkubwa sana wa kutoa Sadaka katika agano jipya, na shetani anafanya kila awezalo kuwazuia watu wasitoe sadaka kwa Mungu, kwani anaijua Nguvu iliyopo katika sadaka kwa mkristo.

Na moja ya njia anayotumia kuwafanya watu wasimtolee Mungu, ni kuwanyanyua watu/watumishi wake ambao watalichafua eneo hilo kwa aidha kuwalazimisha watu, au kuwatapeli, au kutumia uongo kwa kivuli cha biblia.

Na mtu aliye dhaifu kiimani, akishaona kasoro hizo basi moja kwa moja anakata shauri au anaadhimia kutotoa kabisa sadaka mahali popote kwa kuamini kuwa ni utapeli tu ndio unaoendelea, hivyo adui anakuwa ameshinda juu ya huyo mtu katika eneo la utoaji.

Lakini jambo ni moja tu!.. SADAKA INA NGUVU, na kila MKRISTO (pasipo kujali wadhifa wake, iwe mchungaji au mwanafunzi) NI LAZIMA AJIFUNZE KUTOA SADAKA ili KUFUNGUA MILANGO YA BARAKA na KUONDOA VIKWAZO.

Sasa zipo faida nyingi za SADAKA, lakini leo nataka tuizungumzie hii moja, ambayo ni muhimu sana kuijua…Nayo si nyingine Zaidi ya “KUHARIBU NGUVU ZA MADHABAHU”. Si kila madhabahu inaharibiwa kwa kuomba tu!, la! Nyingine ni lazima zihusishe matoleo/Sadaka.

Hebu tusome habari ya Gideoni kidogo.

Waamuzi 6:25 ”kawa usiku uo huo Bwana akamwambia, MTWAE NG’OMBE WA BABA YAKO, yaani ng’ombe wa pili, wa miaka saba, UKAIANGUSHE MADHABAHU YA BAALI, aliyo nayo baba yako, UKAIKATE ASHERA ile iliyo karibu nayo;

26 UKAMJENGEE BWANA, MUNGU WAKO, MADHABAHU juu ya ngome hii, kwa taratibu zake; UKAMTWAE YULE NG’OMBE WA PILI NA KUMTOA AWE SADAKA YA KUTEKETEZWA, kwa kuni za ile Ashera uliyoikata”

Hapo kuna hatua 4 Gideoni alizoambiwa na Mungu azifanye, ambazo zimebeba funzo kubwa..

   1.MTWAE NG’OMBE WA BABA

Kwanini Amtwae Ng’ombe wa Baba yake?.. Kwasababu madhabahu ile ya baali ilikuwa imemshika sana baba yake (ilikuwa na nguvu juu ya nyumba ya baba yake yote). Ikifunua kuwa na sisi tunapotaka kushughulika na madhabahu za mababa, ni lazima tutafute sadaka kwajili yao, tena zile zinazowagusa kama hiyo ya Gideoni.

   2. UKAIANGUSHE MADHABAHU YA BAALI.

Baada ya Gideoni kumtwaa Ng’ombe wa baba yake, hatua iliyofuata ni kuangusha ile madhababu ya baali na ashera iliyomshika baba yake (kwa kuivunja vunja na kuiponda ponda). Na sisi baada ya kuandaa sadaka hatua inayofuata ni kuzivunja hizo madhabahu kwa damu ya YESU kwa njia ya maombi na kwa KUZIONDOA KABISA KIMWILI KAMA ZINAONEKANA..

Kama kuna miti fulani inatumika kiibada hapo ulipo unaikata, kama ni mazindiko yamewekwa juu ya dari unayaondoa, wala usiogope, na tena wakati mwingine usimwambie mtu..wewe yaondoe kimya kimya kama alivyofanya Gideoni..ukienda kutafuta ruhusa hawatakuruhusu..zaidi utanyanyua vita vikali..

Gideoni angeenda kumpa kwanza taarifa baba yake kwamba ile madhabahu ya baali anaenda kuivunja baba yake asingemwelewa kabisa, kwani zile roho zilikuwa zimemshika baba yake na alikuwa anaiogopa sana ile miungu.. Vile vile madhabahu za mababa/na mababu zimewashika na kuwaogopesha wanaoziabudu.

Hivyo wewe vaa ujasiri kuwasaidia, kwani baada ya hapo watamshukuru Mungu wako kwa mambo yatakayofanyika baada ya hapo.

  3.UKAMJENGEE BWANA MADHABAHU.

Baada ya Gideoni kuvunja ile madhabahu akaijenga madhabahu ya BWANA pale pale. Na sisi baada ya maombi na kusafisha kila uchafu..tunalisimamisha jina la Bwana mahali pale, kwa kuanzisha ibada, au kanisa…Wengi baada ya maombi hakuna tena kinachoendele, jambo ambalo ni la hatari sana!..

Ni lazima jina la Bwana liendelee kutamkwa mahali pale, ili madhabahu ya adui isisimamishwe tena, kama ni nyumbani au kijijini. (Maombi ya asubuhi na jioni lazima yafanyike, vile vile nyakati za kujifunza Neno la Mungu lazima ziendelee, na watu waendelee kumtafuta Mungu).. Sio kuomba tu na kuacha!.

   4. UKAMTOE NG’OMBE KUWA SADAKA.

Baada ya Gideoni kujenga madhabahu akamtoa yule Ng’ombe wa baba yake awe sadaka na hapo ndipo ukawa mwisho wa Nguvu ya ile madhabahu ya baali kutenda kazi…ikamwachia baba yake moja kwa moja, hata alipokuja na kusikia kuwa ile madhabahu ya ashera imevunjwa na mwanae wala hakuogopa kwani tayari vifungo vya uoga vilikuwa vimeshamwachia…. na hata yeye (Gideoni) naye pia alifunguliwa kwa ujumla.. Na hapo ndio ukawa mwanzo wa ushujaa wa Gideoni!.

Vile vile na sisi tunapomaliza maombi na kuhitimisha kuvunja madhabahu…Ile sadaka inapaswa itumike kujenga kanisa la pale, au kuimarisha ibada za pale, ikiwa na maana kwamba kama fedha basi zitumike kununua biblia, au vitabu vya nyimbo, au kama ni kiwanja kimetolewa kama sadaka basi kitumike kujenga kanisa ili watu wa Mungu waendelee kumwabudu Mungu wa kweli pale.

Lakini ikiwa hakuna namna ya wewe kufika mahali pale ambapo madhabahi hizo zimesimamishwa, aidha kutokana na umbali.. basi baada ya maombi toa sadaka katika madhabahu nyingine yoyote ya Mungu aliye hai na italeta matokeo yale yale. Lakini kumbuka USIOMBE TU, BILA KUTOA!..TOA TOA TOA!!!!!

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

MADHABAHU NI NINI?

YANAYOENDELEA SASA KATIKA MADHABAHU YA MUNGU ROHONI.

UDHAIFU WA SADAKA!

Kwanini madhabahu zilitengenezwa kwa mawe yasiyochongwa?

MAVAZI YA NDANI NA YA NJE.

Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments