MSINGI WA NYUMBA YA MUNGU, NI JINA LA MUNGU.

by Admin | 29 March 2024 08:46 am03

Kamwe hatuwezi kuitenganisha nyumba ya MUNGU na JINA LAKE.. Vitu hivi viwili vinakwenda pamoja DAIMA!!!..

Lakini nyumba ya Mungu inapogeuzwa na kuwa  nyumba ya Jina la Mchungaji, au jina la Nabii, au inakuwa nyumba ya Maji ya Upako, au mafuta ya Upako, au chumvi ya Upako..nyumba  hiyo inakuwa si nyumba tena ya Mungu bali inakuwa ni pango la wanyang’anyi kulingana na biblia.

Yeremia 7:11 “Je! Nyumba hii, IITWAYO KWA JINA LANGU, imekuwa pango la wanyang’anyi machoni penu? Angalieni, mimi, naam, mimi, nimeliona jambo hili, asema Bwana”.

Tunapoacha kulinyanyua jina la BWANA YESU ndani ya nyumba yake, na badala yake tunalinyanyua jina la Nabii, au Mchungaji, au Mtume, au mtu Fulani ndani ya kanisa, hapo MUNGU tunayemtamani hayupo!.

Tunapoliondoa jina la BWANA YESU ndani ya Kanisa, na kuanza kutumia mafuta ya upako kila wakati kama njia mbadala!…hapo tumemwondoa MUNGU kabisa na tumemweka mungu mwingine ambaye ni shetani..tunapoliondoa jina la YESU na kutumia chumvi au udongo kama mbadala wake, kwa kila changamoto inayouja mbele yetu…hapo MUNGU hayupo, bali tupo wenyewe!!.

Tunapoacha kuomba kwa jina la BWANA YESU na kuanza kuziomba sanamu..hayo ni machukizo makubwa..

Yeremia 7:30 “Maana wana wa Yuda wametenda yaliyo maovu machoni pangu, asema Bwana; wameweka machukizo yao NDANI YA NYUMBA HIYO, IITWAYO KWA JINA LANGU, hata kuitia unajisi”.

Kama Mkristo au Mhubiri kamwe usilitenganishe jina la BWANA YESU na NYUMBA YAKE!.. Nyumba yake imekusudiwa kukaa jina lake humo MILELE.. Hakuna wakati ambapo JINA LA YESU, Litaisha muda wa matumizi yake ndani ya KANISA.. Hicho kipindi hakipo!.

Zama hizi za siku za mwisho shetani amenyanyua uongo mkubwa sana, kuwa ZAMA ZA JINA LA YESU ZIMEPITA! Hivyo sasa jina la YESU halina nguvu tena wala hatulitumii tena.. Ndugu fahamu kuwa huo ni uongo wa adui asilimia zote, jina la YESU limekusudiwa kutajwa na kutumika ndani ya NYUMBA YAKE DAIMA..

2Nyakati 7:16 “Maana sasa nimeichagua nyumba hii na kuitakasa, ILI KWAMBA JINA LANGU LIPATE KUWAKO HUKO MILELE; yatakuwako na macho yangu, na moyo wangu daima”

Na tena Macho ya Mungu na Moyo wake upo katika Nyumba ile ambayo ndani yake LINAKAA JINA LAKE na si jina la Mtu au kitu. Na tena maandiko yanasema hakuna jina lingine tulilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo isipokuwa hilo jina la YESU.

Matendo 4:12 “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo”.

Na zaidi sana yanasema,  lolote lile tufanyalo liwe kwa tendo au kwa Neno tufanye yote kwa jina la BWANA YESU.

Wakolosai 3:17 “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye”.

Hivyo kwa hitimisho ni kuwa JINA LA YESU ndio MSINGI WA KANISA la kweli la MUNGU.. Mahali pasipotajwa wala kutumika jina hilo, mahali hapo hapana MUNGU wa mbingu na nchi bali pana roho nyingine, ambayo ni ya Adui shetani.

Mistari mingine inayozidi kuthibitisha kuwa nyumba ya MUNGU imekusudiwa kuwekwa jina lake milele ni kama ifuatayo.. 2Samweli 7:13, 1Wafalme 5:5, 1Wafalme 8:18-19, 1Wafalme 9:7, Yeremia 7:10-14, Yeremia 32:34 na Yeremia 34:15.

Je! Umempokea YESU kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako?..fahamu kuwa tunaishi siku za mwisho za kurudi kwake mwana wa Adamu, na hukumu ya mwisho ipo karibu.

Maran atha!

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Je huduma za mitume na manabii, zinaendelea kufanya kazi hadi sasa?

Je ni kweli Tumejengwa juu ya Mitume na Manabii? (Waefeso 2:20)

ORODHA YA MITUME.

Je Mungu anaketi katika giza? (1Wafalme 8:12)

Nitamjuaje nabii wa Uongo?

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/03/29/msingi-wa-nyumba-ya-mungu-ni-jina-la-mungu/