Je Mungu anaketi katika giza? (1Wafalme 8:12)

Je Mungu anaketi katika giza? (1Wafalme 8:12)

Swali: Maandiko yanasema Mungu anaketi katika Nuru (1Timotheo 6:16 na Yohana 1:5) lakini yanasema tena Mungu anakaa kwenye giza (1Wafalme 8:12) Je yanajichanganya?.

Jibu: Tuisome mistari hiyo kwanza kabla ya kuingia katika ufafanuzi.

1Timetheo 6:16 “ambaye yeye peke yake hapatikani na mauti, AMEKAA KATIKA NURU ISIYOWEZA KUKARIBIWA; wala hakuna mwanadamu aliyemwona, wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye hata milele. Amina”

Tusome tena kitabu cha Wafalme..

1Wafalme 8:12 “Ndipo Sulemani akanena, Bwana alisema ya kwamba ATAKAA KATIKA GIZA NENE. 

13 Hakika nimekujengea nyumba ya kukaa, iwe mahali pa makao yako milele”

Je biblia inajichanganya?..

Jibu ni La! Biblia haijichanganyi mahali popote kwasababu ni Neno la Mungu lililojaa nguvu na Uweza na kweli.

Tukirudi katika mistari hiyo, ukweli ni kwamba Mungu juu mbinguni aliko, hayupo katika giza wala hakai katika giza, bali yupo katika Nuru kuu isiyoweza kukaribiwa sawasawa na andiko hilo la 1Timotheo 6:16 “…ambaye yeye peke yake hapatikani na mauti, AMEKAA KATIKA NURU ISIYOWEZA KUKARIBIWA”.

Ni sawasawa na jinsi tunavyomtolea matoleo yetu… Si kwamba yeye ana uhitaji na kwamba sisi tunaweza kumwongezea kitu, au tunaweza kumwibia, kiuhalisia sisi hatuwezi kumpa kitu Mungu, kwasababu vyote tutakavyompa ni vya kwake yeye, ndiye kaviumba… vile vile hatuwezi kusema tunamwibia Mungu kwasababu vyote yeye ni vya kwake..

Lakini linapokuja suala la mahusiano yake na sisi, Mungu aliye Mkuu na mweza huwa anajishusha na wakati mwingine kujifananisha na sisi, ndio maana utaona anajiweka na yeye kama mwanadamu mwenye kuhitaji kuhudumiwa kuhudumiwa, mwenye kuhitaji kupendwa, mwenye kujengewa nyumba n.k

Sasa katika hali hiyo ya kujishusha ili kujenga mahusiano yetu sisi na yeye, huwa anahitaji kufanyiwa vitu vilivyo bora kama tu sisi tunavyoweza kuwafanyia wale tunaowaheshimu vitu vilivyo bora, ndio hapo anaagiza tumtolee vile vinavyotugharimu sadaka zisizo kilema, vile vile na tumjengee Nyumba zilizo bora kuliko zetu tunazoishi.

Sasa Mfalme Daudi pamoja na Sulemani mwanae, kwa kutambua hilo waliwaza kumjengea Mungu nyumba yenye utukufu kuliko zao walizoishi. Waliona kule Sanduku la Mungu lilipo ni kwenye “giza nene” ndani ya Mapazia (yaani mahema).. Na wakati wenyewe wanakaa kwenye nyumba za Mierezi zilizojaa marumaru na mwangaza pande zote.

Hivyo dhamiri zao zikawagusa na kusema Mungu hatakaa kwenye “mapazia kule” bali atakaa kwenye nyumba kubwa yenye utukufu na mwangaza mwingi kuliko walizokuwa wanaishi wao, Ingawa walijua kabisa kuwa Mungu kwa ukuu wake na uweza wake hawezi kujengewa nyumba na wanadamu.. lakini waliadhimia kumjengea hivyo hivyo kwasababu walimjua Mungu katika viwango vingine tofauti na wengine walivyomjua.

1Wafalme 8:26 “Sasa, Ee Mungu wa Israeli, nakusihi, ulithibitishe neno lako, ulilomwambia mtumishi wako, Daudi, baba yangu. 

27 Lakini Mungu je? Atakaa kweli kweli juu ya nchi? Tazama, mbingu hazikutoshi, wala mbingu za mbingu; sembuse nyumba hii niliyoijenga!

28 Walakini uyaelekee maombi ya mtumwa wako, na dua yake, Ee Bwana, Mungu wangu, uisikilize sauti na maombi ya mtumwa wako, aombayo mbele zako leo”.

2Samweli 7:1 “Ikawa, mfalme alipokuwa akikaa katika nyumba yake, hapo Bwana alipomstarehesha, asiudhiwe na adui zake waliomzunguka pande zote,

2 mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia.

3 Nathani akamwambia mfalme, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; maana Bwana yu pamoja nawe. 

4 Ikawa usiku uo huo, neno la Bwana likamfikia Nathani kusema,

5 Enenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, Bwana asema hivi, Je! Wewe utanijengea nyumba, nikae ndani yake?

 6 Kwa maana mimi sikukaa ndani ya nyumba, tangu siku ile niliyowatoa wana wa Israeli katika Misri, hata leo, lakini nimekaa katika hema na maskani.

7 Mahali mwote nilimokwenda na wana wa Israeli wote, je! Nimesema neno lo lote na mtu ye yote wa waamuzi wa Israeli, niliyemwagiza kuwalisha watu wangu Israeli, nikisema, Mbona hamkunijengea nyumba ya mierezi? 

8 Basi, sasa, mwambie mtumishi wangu, Daudi, maneno haya, Bwana wa majeshi asema hivi, Nalikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya Israeli;

9 nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina kuu, kama jina la wakuu walioko duniani.

 10 Tena nitawaagizia mahali watu wangu Israeli, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena, kama hapo kwanza; 

11 naam, kama vilivyokuwa tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi, wawe juu ya watu wangu Israeli; nami nitakustarehesha mbele ya adui zako wote. Tena Bwana anakuambia ya kwamba Bwana atakujengea nyumba. 

12 Nawe siku zako zitakapotimia, ukalala na baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitaufanya imara ufalme wake”

Ni nini tunachoweza kujifunza katika habari hii?.

Mungu ni mkuu lakini linapokuja suala la mahusiano yetu na yake anajiweka katika nafasi kama ya Mtu, Ikiwa unaishi katika nyumba nzuri yenye marumaru na Nuru kila mahali, lakini nyumba ya Mungu kule unakoabudu ni giza jitafakari mara mbili, (hapo ni sawa na umemweka Mungu kwenye giza) usiseme Mungu ni mkuu hawezi kujengewa nyumba.. ni kweli ni mkuu lakini anawivu kama wa mwanadamu wa kawaida (Kumbukumbu 4:24).

Kama humtolei Mungu vile vinavyopendeza, ukiwaza kwamba yeye ni tajiri kaumba vyote, na hana haja na chochote, tafakari mara mbili, hata Daudi aliwaza hivyo lakini bado aliwaza kumjengea Bwana Nyumba na Mungu akambariki na kumpa jina.

Kama Kitabu chako cha kumbukumbu za kazi ni kizuri lakini biblia yako ni makaratasi yaliyo chanika chanika, tafakari mara mbili.

Kama vitabu vyako na nyaraka zako zipo sehemu safi na katika hali nzuri lakini kitabu chako cha uzima (biblia) kipo makabatini na kwenye mikoba michafu, hapo umemwekea Mungu kwenye giza nene!! Na ni dharau za hali ya juu, tafakari mara mbili. Haya ni mambo madogo tu! Lakini yanatupunguzia utukufu mwingi sana na heshima yetu nyingi sana kwa Mungu

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Je Kauli ya Mungu katika Warumi 11:4 na 1Wafalme 19:18 inajichanganya?.

Je! Siku ilihesabiwaje kabla ya jua na mwezi kuumbwa?

HAMA KUTOKA GIZANI

MKUU WA ANGA.

Maneno ya mchongezi ni kama vitoweo; Nayo hushukia pande za ndani za tumbo

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Micchael Paul
Micchael Paul
1 year ago

Somo zuri sana