Kwanini kuna mrudio wa uumbaji kwenye Mwanzo sura ya pili?

by Admin | 9 July 2024 08:46 am07

Swali: Tukisoma Mwanzo sura ya kwanza tunaona Mungu akimaliza kazi yote ya uumbaji kwa zile siku saba, lakini tukirudi kwenye Sura ya pili tuona ni kama tena Mungu anarudia uumbaji anamuumba mwanadamu,  na pia mimea, je kulikuwa na uumbaji wa aina mbili ulitokea pale. Na ni nini tunajifunza pale?


JIBU: Jibu ni hapana, uumbaji wa Mungu ulikuwa ni ule ule mmoja, tofauti na baadhi ya watu wanavyodhani. isipokuwa Sura ya kwanza Mungu anaeleza ‘kwa taswira ya ujumla’, lakini katika sura ya pili anaeleza jinsi ‘utaratibu wa uumbaji wake ulivyokuja kutokea’, mpaka kuileta hiyo picha ya ujumla.

Kwamfano katika Sura ya kwanza anasema Mungu alimuumba mwanamke na mwanaume..

Mwanzo 1:27 Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.

28 Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.

Lakini katika sura ya pili anaonyesha jinsi alivyoanza kumuumba  kwa kumtoa ardhini mpaka alivyompulizia pumzi ya uhai, hadi utaratibu wake wa kutawala.

Mwanzo 2:4 Hivyo ndivyo vizazi vya mbingu na nchi zilipoumbwa. Siku ile Bwana Mungu alipoziumba mbingu na nchi

5 hapakuwa na mche wa kondeni bado, wala mboga ya kondeni haijachipuka bado, kwa maana Bwana Mungu hajainyeshea nchi mvua, wala hapana mtu wa kuilima ardhi;

6 ukungu ukapanda katika nchi, ukatia maji juu ya uso wote wa ardhi.  7 Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.

8 Bwana Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya.

Umeona,? Vilevile ukisoma Mwanzo 1:11&12, utaona Mungu anaumba mimea yote . Lakini hapo kwenye sura ya pili anaonyesha  jinsi mime hiyo inavyokuja kutokea, anaeleza kwanza inaanza  katika mbegu, kisha inyeshewe mvua, ikue baadaye ndio iwe mche kamili wenye matunda.

Hivyo, Kulikuwa na umuhimu wa kuwekwa sura zote mbili, ili tuelewe  kanuni za Mungu za utekelezaji wa mipango yake. Maana kama tungeishia tu sura ya kwanza tusingeelewa ni kwa namna gani mambo yanaendelea kama yalivyo leo.

Ni fundisho gani lipo hapo?

Hata sasa Mungu anasema jambo. Lakini pia huna budi kuelewa mpango wake wa utekelezaji wa hilo jambo! Ili usiudhike, au usikate tamaa, au usijikwae, au usiwe na mashaka. Unatafakari ni kweli Mungu alimuumba mwanamke tangu awali, lakini kutokea kwake kulikuja baadaye sana, tena sio ardhini bali ubavuni mwa Adamu. Kama hilo tusingelifahamu, tusingeelewa kwanini tunaambiwa sisi wote ni mwili mmoja.

Kama tusingejua kuwa  ili mti ufikie matunda, kama Mungu alivyoukusudia, ni lazima uanze kwanza kama mbegu, ioze ardhini, kisha ipate mvua, imee, itoke katika jani, hadi shina, hadi mti. Tungesema hii si sawa, kuna shida, mbegu kuoza ardhini, hakuna mmea hapo?.

Halikadhalika hata sasa Mungu amekuahidi pengine, atakupa jambo Fulani. Sasa usitarajie lije ghafla tu, pengine litapitia hatua Fulani, huwenda likaonekana kama limetoweka kabisa,kama vile mbegu inayooza ardhini, lakini mwishowe itakuja kutokea tu, kama tu Yusufu alivyoonyeshwa kuwa ndugu zake watamwinamia, Au Ibrahimu kuonyeshwa atakuwa  baba wa mataifa mengi, lakini mapito yao unayajua, Yusufu kuuzwa utumwani, kutupwa gerezani, Ibrahimu kuwa tasa. Lakini mwisho utaona yale waliyoahidiwa yalikuja kutokea vilevile.

Tunapaswa tumwelewe sana Mungu ili tuwe na amani, Neno la Mungu linaposema, kwa kupigwa kwake sisi tumepona, amini kuwa umepona kwa kifo cha Yesu, hata kama utahisi maumivu mengi kiasi gani leo, daktari atakuambia huwezi kupona ugonjwa wako hautibiki. Wewe amini, tu hilo jambo litatokea, haijalishi litachukua wakati gani, utapitia mateso mengi kiasi gani leo, mwisho wa siku utakuwa tu mzima.

Usiishi tu na mwanzo sura ya kwanza, ishi pia na sura ya pili. Utamwelewa Mungu.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

NGUVU YA MUNGU YA UUMBAJI

Kwanini Bwana achukizwe na mtumwa yule aliyeficha talanta yake ardhini? (Mathayo 25:26-30)

Ni maneno gani Bwana Yesu aliyokuwa anayaandika ardhini? (Yohana 8:7).

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/07/09/kwanini-kuna-mrudio-wa-uumbaji-kwenye-mwanzo-sura-ya-pili/