HAWEZI KUWA MWANAFUNZI WANGU.

by Admin | 13 July 2024 08:46 am07

Luka 14:27 “Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, HAWEZI KUWA MWANAFUNZI WANGU”.

Je unaelewa maana ya kuwa Mwanafunzi?

Zifuatazo ni sifa za mwanafunzi.

   1. KUFUNDISHWA

   2. KUJIFUNZA.

   3. KUFANYA MITIHANI.

   4. KUHITIMU.

Mtu akikosa hizo sifa basi sio mwanafunzi.

Na kwa upande wa BWANA wetu YESU KRISTO ni hivyo hivyo (Tutazame moja baada ya nyingine).

       1. KUFUNDISHWA

Hakuna mwanafunzi yoyote anayejifundisha mwenyewe, ni lazima awe na mwalimu

Na vile vile Ili ukidhi vigezo vya kufundishwa na BWANA YESU mwenyewe ni “lazima ujikane nafsi”.. Na matokeo ya kukosa kufundishwa na Bwana ni kushindwa mitihani ya maisha ikiwemo VIPINDI VYA KUPUNGUKIWA na VIPINDI VYA KUWA NA VINGI.

Katika biblia tunaona mtu aliyefundishwa Vizuri na Bwana YESU na kuelewa ni Paulo… Yeye alifundishwa jinsi ya kuishi vipindi vyote vya (njaa na kutokuwa na njaa, vya kupungukiwa na kuongezekewa).

Wafilipi 4:12 “Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa.

13  Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”

2. KUJIFUNZA.

Hii ni sifa ya pili ya Mwanafunzi yoyote, ni lazima awe anajifunza. Na kwa upande wa Imani ni lazima kujifunza kama mwanafunzi wa Kristo…

Na tukitaka tuweze kujifunza biblia na kuielewa  vizuri ni lazima tujikane Nafsi na kubeba misalaba yetu na kumfuata Bwana YESU. (hakuna njia nyingine tofauti na hiyo).

Si ajabu leo hii inakuwa ngumu sana kuweza kuielewa biblia, pindi tuisomapo…sababu pekee ni kutojikana nafsi na kubeba msalaba na kumfuata Bwana YESU, tunapenda ule ukristo laini laini, ambao hauna matokeo yoyote kiroho.

   3. KUFANYA MITIHANI.

Hii ni sifa ya tatu ya mwanafunzi yoyote anayesoma, ni lazima awe na vipindi vya kujaribiwa kwa mitihani.

Vivyo hivyo ili tuwe wanafunzi wa YESU wa Bwana ni lazima tupitishwe katika vipindi vya kujaribiwa na Bwana YESU mwenyewe….. Na lengo la mitihani hiyo (au majaribu hayo) ni kumwimarisha mtu huyo kiimani.

Yakobo 1:2 “Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali;

3  mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi”.

Na madhara ya kukosa kujaribiwa kwa mitihani ya BWANA YESU ni kushindwa kuhitimu na hatimaye kukosa cheti.

    4. KUHITIMU.

Mwanafunzi anayehitimu ni yule aliyemaliza mitihani yote na kufaulu, (huwa anapewa cheti) kile cheti ni kibali maalumu, na fursa  pamoja na heshima ya daima kwa mwanafunzi yule.

Vile vile na mtu aliye mwanafunzi wa BWANA YESU, akiisha kumaliza majaribu yote na kuyashinda, atahitimu kwa kupewa cheti ambacho ni TAJI YA UZIMA..

Yakobo 1:12 “ Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, Bwana aliyowaahidia wampendao”.

Jiulize je wewe ni Mwanafunzi wa BWANA YESU au ni mfuasi tu?…. Waliokuwa wanamfuatilia Bwana YESU ni wengi lakini waliomfuata na kuwa wanafunzi wake walikuwa wachache sana.. Wengine wote walikuwa ni washabiki tu aidha wa miujiza au wa siasa, lakini waliojiunga na chuo cha Bwana YESU walikuwa ni wachache sana.

Na kanuni ya kujiunga na chuo hicho cha Bwana YESU na kuwa mwanafunzi wake si nyingine Zaidi ya hiyo ya “KUJIKANA NAFSI NA KUBEBA MSALABA”.

Luka 14:27 “Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, HAWEZI KUWA MWANAFUNZI WANGU”.

Na kumbuka hakuna tafsiri nyingine ya UKRISTO au kuwa MKRISTO Zaidi ya UANAFUNZI..

Matendo 11:26  “….Na WANAFUNZI waliitwa WAKRISTO kwanza hapo Antiokia”.

Hivyo ukitaka kujijua kama wewe ni Mkristo au la!.. sipime tu kama umeshakuwa Mwanafunzi wake, kama huna sifa hizo hapo juu za uanafunzi bado hujawa MKRISTO.

Bwana YESU atusaidie.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

NINI MAANA YA KUWA MKRISTO?

Bwana alimaanisha nini kusema “Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake”?

Mtu akija kwangu naye HAMCHUKII baba yake hawezi kuwa mwanafunzi wangu?

NITAJUAJE KUWA NIMEITWA ILI KUMTUMIKIA MUNGU?

TOA HUDUMA ILIYO BORA.

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/07/13/hawezi-kuwa-mwanafunzi-wangu/