Tafsiri ya Mithali 27:18 Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake;

by Admin | 23 July 2024 08:46 pm07

SWALI: Maana ya Mithali 27:18 Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake; Naye amhudumiaye bwana wake ataheshimiwa.


JIBU: Mstari huo una vipengele viwili cha kwanza ni Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake

Na cha pili ni naye amhudumiaye bwana wake ataheshimiwa.

Tukianzana na hicho cha kwanza. Tufahamu kuwa Mungu ameiandika injili yake sio tu kwenye kitabu chake, bali pia kwenye vitu vya asili, ndio maana Yesu alitumia mifano mingi ya namna hiyo, kuzungumza nao habari zake mwenyewe. Kuanzia wakulima, mimea, wanyama, wafanya biashara, wafalme n.k.

Sasa hapa anasema yeye atunzaye mtini atakula matunda yake. Kumbe kula matunda ni “kutunza”. Usipotunza huwezi pata chochote. Ili uone kazi yako, utaiwekea mbolea, utaipalilia, utaipiga dawa n.k. Na mwisho utakuwa mvumilivu aidha miaka mitatu/ minne ukisubiri  mazao.

Halidhalika rohoni. Sisi kama watoto wa Mungu (tuliookolewa), kila mmoja wetu anao “mtini” moyoni mwake, na huo si mwingine zaidi ya Yesu Kristo. Wengi wasichojua ni kwamba Kristo huanza kama kichanga, kisha huwa kijana mdogo, baadaye huwa mtu mzima, na mwisho huanza kutenda kazi zake. Kama tu alivyokuwa hapa duniani alivyoishi na Mariamu na Yusufu, hakuanza kufanya chochote pindi anazaliwa.

Hivyo usipomlea ipasavyo hutafaidi matunda yake vema. Ndio mfano wa mpanzi ambao Yesu mwenyewe aliutoa, akasema zile mbegu ziliporushwa nyingine zikaishia njiani, nyingine kwenye miamba, nyingine kwenye miiba, na nyingine kwenye udongo mzuri, moja ikazaa thelathini, nyingine sitini, nyingine mia. Akatoa ufafanuzi wake, kwamba zile zilizofanikiwa kuzaa, ni kwamba zilichangiwa na KUVUMILIA (Luka 8:15). Sasa kuvumilia nini? Kuvumilia  hatua zote tatu za mwanzo, yaani dhiki kwa ajili ya Kristo, kujiepusha na anasa, udanganyifu wa mali, na uvivu wa kulitendea kazi Neno.

Ukuaji wa kiroho tafsiri yake ni ‘Kristo kukua ndani yako’. Ukiona upo  ndani ya wokovu kwa miaka mingi, halafu huoni matunda yoyote ya wokovu wako, katika ufalme wa Mungu, tatizo linakuwa hapo, hukuwa na nafasi ya kuutunza mtini wako.

Ukiokoka, ni lazima bidii ya kusoma Neno iwe ndani yako kila siku, usiwe mvivu wa maombi, vilevile epuka maisha ya kidunia, na ubize uliopitiliza, ambao unakufanya hata nafasi ya Mungu wako unakosa. Ukizingatia hayo, baada ya kipindi Fulani utaona Kristo anavyojengeka nafsini mwako , na kukutumia.

Lakini pia sehemu ya pili inasema naye amhudumiaye bwana wake ataheshimiwa,. Ni hekima ya kawaida, ukiwa mfanyakazi mwema kwa bwana wako, hawezi kukuchikia kinyume chake atakupa heshima yako, lakini pia na watu wengine wote wa nyumbani kwake watafanya hivyo.

Si zaidi Mungu?

Heshima hasaa kwa Mungu wako, sio kumwambia “Shikamoo” au kuomba kwa sauti ya unyenyekevu, au kuinamisha kichwa uwapo ibadani. Heshima yake hasaa ni pale unapomtumikia, unapotii agizo lake la kuwaeleza wengine habari za injili, na pale naposimama katika nafasi yako kwenye mwili wa Kristo.

Tutafute kuheshimiwa na Bwana kwa kuwashuhudia wengine injili.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

MTINI, WENYE MAJANI.

Biblia imemaanisha nini kusema Nyoka atakula mavumbi?(Opens in a new browser tab)

(Opens in a new browser tab)Je ile habari ya mtini kunyauka inajichanganya?(Opens in a new browser tab)

MAUTI NA UZIMA HUWA KATIKA UWEZO WA ULIMI.(Opens in a new browser tab)

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/07/23/mithali-2718-yeye-autunzaye-mtini-atakula-matunda-yake/