MAANA ROHO HUCHUNGUZA YOTE, HATA MAFUMBO YA MUNGU.

by Admin | 28 October 2024 08:46 am10

Wakorintho 2:10  Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.

11  Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu

Sifa mojawapo ya Roho Mtakatifu, ni kuchunguza, na tunajua mpaka kitu kichunguzwe ni lazima tu kitakuwa kimesitirika, kwa lugha nyingine tunaweza kusema kipo katika mafumbo. Hivyo Roho Mtakatifu anafanya kazi ya  kuyachunguza “YOTE”. Akiwa na maana Mafumbo yote, si tu yale yaliyo chini bali pia hata yaliyo kule juu Mungu mwenyewe alipo.

Na leo tutanyambua aina hizo za mafumbo kwa upana, ili tuelewe ni kwa jinsi gani Roho Mtakatifu alivyomsaada mkubwa sana kwetu.

Mafumbo yamegawanyika katika sehemu kuu tatu (3)

  1. Mafumbo ya wanadamu
  2. Mafumbo ya shetani
  3. Mafumbo ya Mungu

Mafumbo ya Wanadamu:

Ukipokea Roho Mtakatifu,  moja kwa moja unaongezewa hekima, ya kuweza kupambanua, na kuhukumu, akili zote za kibinadamu. Wala hakuna litakalokushinda, kwamfano Bwana Yesu alipowekewa mitego mingi na wayahudi ili watafute kosa ndani yake, wapate kumshitaki, hawakuweza kumshinda kwasababu saa ile ile, alielewa vema mawazo yao kwa Roho Mtakatifu aliyekuwa ndani yake.

Kwamfano katika ile habari ya kulipa kodi walipomjaribu, walishindwa kabisa kabisa.

Mathayo 22:15  Ndipo Mafarisayo wakaenda zao, wakafanya shauri, jinsi ya kumtega kwa maneno.

16  Wakatuma kwake wanafunzi wao pamoja na Maherodi, wakasema, Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na njia ya Mungu waifundisha katika kweli, wala hujali cheo cha mtu awaye yote, kwa maana hutazami sura za watu.

17  Basi utuambie, Waonaje? Ni halali kumpa Kaisari kodi, ama sivyo? 18  Lakini Yesu akaufahamu uovu wao, akasema, Mbona mnanijaribu, enyi wanafiki?

19  Nionyesheni fedha ya kodi. Nao wakamletea dinari. 20  Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii, na anwani hii?

21  Wakamwambia, Ni ya Kaisari. Akawaambia, Basi, mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu. 22  Waliposikia, walistaajabu, wakamwacha, wakaenda zao

Wakati mwingine walimletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, ili wamnase wakashindwa pia, kwasababu Yesu alikuwa na Roho wa Mungu ndani yake(Yohana 8:1-11). Ndio maana Yesu naye akatupa hakikisho hilo kwamba katika kuenenda kuhubiri kwetu,  tusihofu watakapotaka kutushitaki, na kutupeleka mabarazani, au mahakamani, kutuhukumu, kwani yeye mwenywe atatupa kinywa cha hekima ambacho watesi wetu hawatatuweza.

Yohana 21:12  Lakini, kabla hayo yote hayajatokea, watawakamata na kuwaudhi; watawapeleka mbele ya masinagogi, na kuwaua magerezani, mkipelekwa mbele ya wafalme na maliwali kwa ajili ya jina langu.

13  Na hayo yatakuwa ushuhuda kwenu.

14  Basi, kusudieni mioyoni mwenu, kutofikiri-fikiri kwanza mtakavyojibu;

15  kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga.

Lakini pia Roho achunguzaye mafumbo hutupa hekima sio tu ya kutambua lakini pia ya kufanya hukumu sahihi.

Utakumbuka kisa kile cha Sulemani na wale wanawake wawili makahaba, ambao kila mmoja alikuwa ana mng’ang’ania mtoto Yule mmoja wakisema ni wake. Lakini Sulemani alipewa hekima ya kutoa hukumu vema, kwa kuwaambia nileteeni upanga, nimgawanye, ili kila mtu achukue nusu yake. Yule ambaye mtoto si wake akasema na iwe hivyo, lakini Yule mwingine akamwonea huruma. Ndipo Sulemani akatambua kuwa mtoto ni wa Yule mama aliyemwonea huruma (1Wafalme 3:16-28)

Sasa hiyo yote ni kazi ya Roho Mtakatifu ya kuchunguza mafumbo ya wanadamu, na kutupasha habari.

Lakini pia hutumia  njia ya maono au  ndoto kutufahamisha. Mafumbo yaliyositirika mioyoni mwa watu. Mfano wa Yusufu kwa Farao, na Danieli kwa ile ndoto ya Nebukadreza, Mambo ambayo hata walioziota ndoto zenyewe hawakuzikumbuka wala kujua maana zao, lakini Roho Mtakatifu aliwafunulia.

Hivyo ndivyo Roho Mtakatifu anavyotusaidia kuchunguza mafumbo ya wanadamu.

Mafumbo ya shetani:

Si kawaida ya shetani kujidhihirisha kwa wazi kama wengi wanavyodhani, bali huja kama malaika wa nuru, hivyo kama hujajazwa Roho Mtakatifu vema kamwe huwezi yajua mafumbo yake. Ndicho walichokikosa baadhi ya watakatifu wa kanisa la Thiatira.

Ufunuo 2:24  Lakini nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, wo wote wasio na mafundisho hayo, wasiozijua fumbo za Shetani, kama vile wasemavyo, Sitaweka juu yenu mzigo mwingine.

25  Ila mlicho nacho kishikeni sana, hata nitakapokuja.

Swali ni je haya Mafumbo ya shetani yanakujaje?

Yapo Manabii wa Uongo:

Manabii hawa wa uongo wamegawanyika katika makundi mawili.

Kundi la watumishi wa Mungu: Hawa ni ambao hawajasimama vema, hivyo wakati mwingine shetani hutumia vivywa vyao au mafundisho yao kupotosha wengine, bila hata ya wao kukusudia wakati mwingine. Mfano wa hawa alikuwa ni Petro, wakati ule aliposimama mbele ya Yesu na kuanza  kumkemea kwamba hatakwenda msalabani. Lakini Yesu palepale alitambua si Petro anayezungumza bali ni shetani, akamkea na kumwambia nenda nyuma yangu shetani (Mathayo 16:23).

Mfano wa hawa pia ni wale manabii 400 wa Ahabu. Ambao walimtabiria mfalme kuwa akienda vitani atashinda, kumbe ni pepo la uongo liliwaingia vinywani mwao likawaonyesha maono feki. Matokeo yake yakawa ni mfalme kufa (1Wafalme 22).

Mfano wa watumishi wa namna hii wanaompa shetani nafasi kuwatumia ni wengi sana. Hivyo si kila neno ambalo utaambiwa na kila anayeitwa mtumishi ulipokee tu au uliamini, ukijawa Roho vema utaweza yapambanua vizuri mafumbo haya ya shetani katikati ya vinywa vyao. Atakupa upambanuzi, kwa mafuta aliyoyaweka ndani yako.

Kundi la watumishi wa shetani: Hawa wanajijua kabisa kuwa ni watumishi wa ibilisi, ni wachawi wanaovaa suti na majoho, na kusimama madhabahuni, hawana hata ushirika na Kristo. Kuwatambua hawa Roho alitufundisha, ni kutazama matunda yao. (Mathayo 7:15-20), asilimia kubwa ya hawa wanajigamba kwa vitu, ukubwa. Na mafundisho yao ni ya mwilini. lakini pia kwasababu wana mapepo ya utambuzi hupendelea sana kujitii manabii. Ni wengi leo wanawafuata kwasababu ya kazi hiyo, wakidhani wanatabiriwa na Roho Mtakatifu kumbe ni mizimu. Ukijawa Roho vema utaweza kuzitambua hizo Roho. Kwasababu hazina ushirika hata kidogo na jina la Yesu, au mambo ya rohoni.

Mafumbo ya Mungu.

Mungu pia ana mafumbo yake, ambayo kama huna Roho Mtakatifu huwezi yatambua. Kwamfano Kristo anatembea leo duniani, akiwa na kiu, na njaa na uchi, na anagonga kwenye milango ya watu..Sasa kwasababu wewe hujui unadhani akija kwako atakutokea amevaa mavazi meupe na uso unaong’aa kama jua,  hujui kuwa amekuja kama watumishi wa Mungu wa kweli wanaojitaabisha kwa ajili ya roho yako, kukulea na kukulisha neno la Mungu. Lakini wewe unasema hawa ni matapeli, omba omba.

Mathayo 25:31  Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake;

32  na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi;

33  atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto.

34  Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu;

35  kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha;

36  nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia.

37  Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha?

38  Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika?

39  Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia?

40  Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.

Umeona hao wanaozungumziwa hapo, sio wale maskini unaowaona barabarani, au omba-omba, bali ni watendakazi wa Mungu. Hivyo watu wanaoonyosha mikono yao, kuwatengemeza watumishi na madhabahu za kweli za Mungu, wamejaliwa kuyajua mafumbo haya ya Mungu.

Mafumbo ya Mungu yapo mengi sana, ndio siri za ufalme wa mbinguni ambazo zipo ndani ya Yesu Kristo. Ambazo Yesu mwenyewe alizizungumza pia katika Mathayo 13.

Vilevile ukitaka umwone Mungu fumbo lake ni upendo, Ukitaka upewe na Mungu, fumbo lake ni utoe, ukitaka ukwezwe na Mungu fumbo lake ni unyenyekevu.

Kwanini leo utaona mtu anasema sijawahi kumsikia Mungu, na angali Mungu anasema nasi kila siku? Sijawahi kukutana na Mungu, na angali Mungu anakutana nasi kila siku? Sijawahi kuziona nguvu za Mungu, na wakati zipo nasi kila kitu? Ni kwasababu hajajawa vema Roho Mtakatifu, ambaye atamjalia kuujua moyo wa Mungu upo wapi.

Hivyo kwa hitimisho ni kuwa, tunahitaji  kujazwa Roho na hiyo inakuja tutengapo muda wetu mwingi kila siku kutafakari sana Neno, pamoja na kuomba kila siku kwa muda usiopungua saa moja , hiyo itakupelekea kujazwa vema Roho, na hatimaye tutaweza kuyachunguza yote, na kuyatambua yote. Na wala hatutashindwa aidha na mwanadamu au shetani.

Ubarikiwe.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

JINSI ROHO MTAKATIFU ANAVYOKUJA JUU YA MTU.

Roho Mtakatifu ni nani?.

ZIFAHAMU KAZI KUU (10) ZA SHETANI DUNIANI.

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/10/28/maana-roho-huchunguza-yote-hata-mafumbo-ya-mungu/