by Admin | 13 December 2024 08:46 am12
Swali: Katika Mwanzo 22:17, MUNGU anasema kuwa uzao wa Ibrahimu utamiliki malango ya adui, sasa unamiliki vipi huo mlango wa adui?.
Jibu: Turejee…
Mwanzo 22:17 “katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao”.
Awali ya yote ni muhimu kujua kuwa Mzao wa Ibrahimu aliyebeba ahadi kamili za Ibrahimu ni BWANA YESU KRISTO.
Wagalatia 3:16 “Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani, Kristo”.
Wengine wote, akina Isaka na Yakobo,(yaani Israeli katika mwili). walibeba sehemu za baraka hizo lakini si zote.. Iliweza kumiliki baadhi ya milango ya adui katika mwili lakini si yote.
Sasa kwa namna gani Israeli ya mwilini ilimiliki malango ya adui?
Kwa njia ya vita: kumbuka zamani miji ilikuwa inazungukwa na kuta, na mageti makubwa, hivyo nguvu na udhaifu wa mji ulikuwa katika mageti ya mji, hivyo lango la mji likitekwa na kumilikiwa basi tayari ule mji umeshatekwa,
Na Mungu aliwapa ahadi wana wa Israeli kwa jinsi ya mwili, kumiliki mlango/malango ya adui, ndio maana waliweza kuangusha miji ya kanaani iliyo mikubwa na yenye nguvu, na hatimaye kuiteka nyara miji hiyo.
Lakini mbali na hayo, lipo Lango ambalo Israeli ya mwilini asingeweza kumiliki, na mlango huo si mwingine zaidi ya ule wa MAUTI na KUZIMU.
Na kawaida mtu mwenye miliki ya mlango, ni yule mwenye FUNGUO ZA HUO MLANGO.
Mtu akikosa funguo hawezi kuwa na milki ya mlango wowote ule.
Hivyo Israeli ya mwilini alikuwa na Funguo za kufungua Mageti ya Wakaanani na Yeriko na mageti ya Wafilisti na kuwapiga na kuwatoa katika ardhi yao, lakini hakuwa na FUNGUO za MAUTI na KUZIMU,
Hakuweza kuzuia watu wasiingie kuzimu wala kuwatoa huko na kuwarudisha tena juu sawasawa na Ayubu 7:9.
Ayubu 7:9 “Kama vile wingu likomavyo na kutoweka, Ni vivyo huyo ashukaye kuzimuni hatazuka tena kabisa”
Hivyo Israeli ya mwilini haikuweza kumiliki malango yote…. alikwama hapo kwenye Mauti na Kuzimu, sawasawa na maneno ya Bwana Mungu katika Ayubu 38:17.
Ayubu 38:17 “Je! Umefunuliwa malango ya mauti, Au umeyaona malango ya kuzimu?”
Sasa swali la msingi, kama Israeli ya mwilini imeshindwa kumiliki milango hiyo, ni nani basi mwenye uwezo huo sawasawa na Mwanzo 22:17?.
Jibu la swali hili tunalipata katika kitabu kile cha Ufunuo 1:17-18.
Ufunuo 1:17 “Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho,
18 na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. NAMI NINAZO FUNGUO ZA MAUTI, NA ZA KUZIMU”
Huyo mwenye hizo funguo za Mauti na kuzimu, ndiye mwenye milki ya Mlango wa Adui.
Maana adui wa kwanza na wa mwisho wa mwanadamu ni MAUTI ambaye analetwa na dhambi, huyu ndiye aliyeanza na Adamu pale Edeni na atamalizwa na Mwana wa Adamu siku ya mwisho.
1 Wakorintho 15:26 “Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti”.
Na matokeo ya Mauti katika dhambi ni KUZIMU.
Kwahiyo YESU KRISTO ndiye mwenye funguo za Mauti na Kuzimu.
Wafu wote wanamilikiwa na Bwana YESU, na KUZIMU ipo chini ya mamlaka ya Bwana YESU, utauliza kivipi?..Mtu anayekufa sasa katika dhambi si shetani anayemtupa katika lile shimo la kuzimu, bali mamlaka ya YESU kupitia malaika wake ndio wanaowatupa watu katika lile shimo la kuzimu.
Kwasasa shetani hana mamlaka yoyote na wafu, hizo milki alishapokonywa na Bwana siku ile aloposhuka kuzimu, na hayo malango sasa yanamilikiwa na YESU KRISTO (Mkuu wa Uzima).
Warumi 14:9 “Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia”.
Nguvu za Bwana YESU kwasasa ni KUU SANA!!!, ukitaka kufahamu kwa sehemu kiwango cha nguvu alizonazo juu ya Mauti, ikumbuke ile kauli aliyosema..
Yohana 10:17 “Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena.
18 Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu”.
Tafakari mtu anakuambia anao uwezo wa kuitoa roho yake na kuirudisha tena,…yaani kama vile mtu anavyozima taa na kuiwasha….na tena anasema “hakuna mtu aniondoleaye”..Maana yake Bwana YESU hakuuawa, bali yeye mwenyewe ndiye aliyeitoa roho ndani ya mwili wake.
Ndio maana akasema yale maneno…
Luka 23:46 “Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu”
Sasa mtu aliyeuawa hawezi kusema maneno hayo…lakini Bwana YESU hakuuawa bali yeye mwenyewe aliiondoa roho yake katika ule mwili, na ndio maana hata wale askari walishangaa imekuwaje amekufa mapema vile kabla ya kuvunjwa miguu.
Sasa ni kweli yapo maandiko yanayosema kuwa Bwana YESU aliuawa, lakini fahamu kuwa popote yanapotaja hivyo ni kuitia nguvu mada iliyoanza, lakini ukweli ni kwamba Bwana hakuuawa na mtu bali aliitoa roho yake mwenyewe.
Hiyo yote ni kuonyesha kuwa Mlango wa Adui wa Mauti, Bwana anao funguo zake.
Hivyo basi tukitaka mauti na kuzimu zisiwe na nguvu juu yetu, hatuna budi kumwendea yeye mwenye funguo hizo, na hatimaye atupe wokovu.
Lakini tukimkataa yeye mwenye funguo hizo, tujue kuwa hatutaokoka hata kidogo.
Malango ya adui, ni malango ya kuzimu, na ni malango ya mauti na yote chanzo chake ni dhambi.
Je umempokea Bwana YESU na kuoshwa dhambi zako?.
Kama bado unasubiri nini?.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Je mtu anaweza kupoteza wokovu?
ANDALIZI LA MWISHO LA UJIO WA MPINGA KRISTO.
MUNGU HAJARIBIWI NA MAOVU BALI MEMA.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/12/13/https-wingulamashahidi-org-2024-11-29-uzao-wa-ibrahimu-unamilikije-mlango-wa-adui-mwanzo-2217/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.