MHESHIMU MCHUNGAJI WAKO.

by Admin | 14 December 2024 08:46 pm12

Kila mahali pana mamlaka yake, na mamlaka hizo huwa ni  wajibu kwa walio chini yake kuzitii. Kwamfano katika familia Mungu ameweka mamlaka, Baba awe kichwa, na mama msaidizi wake, hivyo ni wajibu wa watoto kuwatii wazazi wao . Familia haiwezi kusimama,.kama mtoto atataka nafasi ya baba, kwamba yeye ndio atoe maamuzi ya mwisho, au ajiamulie la kufanya, awapangie wazazi wake majukumu ya ndani. hilo haliwezekani.

Vilevile katika ngazi ya utawala wa kidunia, Mungu kaziweka mamlaka na anataka watu wote wazitii, kwasababu hazijaamuriwa na mwanadamu bali yeye Mungu mwenyewe..

Warumi 13:1-2

[1]Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu.

[2]Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu.

Tito 3:1-2

[1]Uwakumbushe watu kunyenyekea kwa wenye uwezo na mamlaka, na kutii, na kuwa tayari kwa kila kazi njema; [2]wasimtukane mtu ye yote, wasiwe wagomvi, wawe wema, wakionyesha upole wote kwa watu wote.

Sasa hizi ni mamlaka za kidunia. Zipi kuhusu Mungu, unadhani hana mamlaka?

Mungu pia ameweka mamlaka yake duniani, ambayo ni kuu kupita hizo zote, na kupitia hiyo huwahudumia watu wake. Na anataka tuitii na kuitetemekea kwasababu ni yeye mwenyewe atendaye kazi kupitia hiyo.

Je mamlaka hiyo kaiweka kupitia nani?

Bila shaka kupitia wachungaji wetu/waangalizi wetu, ndani ya kanisa

Ni vema kufahamu kuwa kiongozi yoyote wa kiroho (anayeisimamia kweli). Hakujiteua mwenyewe kwenye nafasi hiyo.  Mitume wa Yesu hawakujichagua wao. Bali walichaguliwa na Mungu mwenyewe.

Mtu yeyote aliyepewa maono ya kuanza kanisa, na ukajikuta upo chini yake, au kateuliwa na Roho Mtakatifu mwenyewe ndani ya kanisa (Matendo 14:23), Huyo ni wa kumtii sana. Kama vile unavyowatii watawala au mazazi wako kwenye familia, haijalishi atakuwa na mapungufu kiasi gani, au umri wake ni mdogo au mkubwa kiasi gani, awe mwenye uwezo au asiye na uwezo kiasi gani.

Kwanini uwaheshimu.

1) Wanajitaabisha kwa ajili yako kukuchunga, kukuonya na kukuombea.

Hivyo wajibu ni wako kurudisha moyo wa upendo, na kuwasikiliza.

1 Wathesalonike 5:12-13

[12]Lakini, ndugu, tunataka mwatambue wale wanaojitaabisha kwa ajili yenu, na kuwasimamia ninyi katika Bwana, na kuwaonyeni; [13]mkawastahi sana katika upendo, kwa ajili ya kazi zao. Iweni na amani ninyi kwa ninyi.

2) Watasimama mbele ya kiti cha hukumu siku ya mwisho kutoa hesabu juu yako.

Hivyo ni wajibu kuonyesha moyo wa kunyenyekea kwao.

Waebrania 13:17

[17]Watiini wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi.

Madhara ya kutowasikiliza/ kutowatii.

i) Watafanya kazi ya Mungu kwa kuugua.

Hapo kwenye Waebrania 13:17b anasema..

..ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi

Na matokeo yake utendaji kazi ndani ya kanisani utakuwa hafifu. Ukishaanza kuonyesha tabia ya kutosikiliza unachoelekezwa, unapewa jukumu hutekelezi, hurudishi mrejesho, unafanya tofauti na wengine, yeye anataka uende kulia wewe unaenda kushoto, , yeye anafundisha hiki wewe unafundisha kile. Fahamu kuwa jambo hilo litamhuzunisha kiongozi wako. Na hivyo kupelekea hamasa ya kuhudumu kupungua. Na madhara yake ni kuwa Mungu kukata utendaji kazi wake mahali hapo,

ii) Dhara lingine ni kuwa utajisababishia adhabu kwa Mungu.

Wakati ule Haruni na Miriamu dada yake. walimnenea Musa maneno mabaya kwasababu na mke wake ambaye hakuwa myahudi. Mungu aliwaadhibu kwa kumpiga ukoma Miriamu kwasababu tu hiyo ya kutoonyesha adabu kwa mtumishi wake.

Hesabu 12:7-8

[7]Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote;

[8]Kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la BWANA yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa Kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa?

Ni kosa kumnenea vibaya mchungaji wako. Epuka masengenyo na uasi na matabaka ndani ya kanisa. Uonapo kosa mwombee, au mfuate mweleze  uwapo naye peke yake. Hilo litamjenga zaidi ya kutoa malaumu na manung’uniko. Adui hutumia sana njia hii kuleta mafarakano na magomvi, na mapigo kanisani.

Mheshimu mchungaji wako, zaidi ya raisi wa nchi kwasababu yeye ni balozi wa mbinguni na Mungu atakuinua (1Petro 5:1-6)

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

TEMBEA NDANI YA SUKOTHI YAKO.-Maafundisho maalumu kwa watumishi

Ipi tofauti kati ya KUHANI na MCHUNGAJI.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/12/14/mheshimu-mchungaji-wako/