1Nyakati 28:17 “na nyuma, na mabakuli, na vikombe vya dhahabu safi; na kwa MATASA ya dhahabu, kwa uzani kwa kila TASA; na kwa matasa ya fedha, kwa uzani kwa kila tasa”.
Ukisoma kuanzia juu utaona kuwa hivyo ni vyombo ambavyo vingepaswa viwepo ndani ya MUNGU aliyokusudia kuijenga Mfalme Daudi.
Lakini kwasababu haikuwa mapenzi ya MUNGU mfalme Daudi aijenge ile nyumba bali mwanae (Sulemani)…hivyo ilimbidi Mfalme Daudi ampe maelekezo ya namna ya kuijenga ile nyumba na viwango vyake.
Moja ya maagizo aliyompa kulingana na alivyooneshwa na Bwana ni uwepo wa MATASA ndani ya nyumba hiyo..(kwamba atakapoijenga basi aweke Matasa ya dhahahu ndani yake).
Sasa Matasa yalikuwa ni nini?
Matasa yalikuwa ni “Makarai/mabeseni” ya dhahabu yaliyowekwa ndani ya Hekalu kwa kusudi la kutawadha (kunawa).
Kwasababu ndani ya Hekalu kulikuwa na makuhani wengi waliokuwa wanafanya kazi mbalimbali na kwa zamu, na kulingana na desturi za wayahudi ilikuwa ni lazima kila Kuhani anawe
(atawadhe) kabla ya kuanza kazi ya kikuhani na hata baada ya kumaliza.
Hivyo vyombo hivyo (MATASA) vilitumika kuhifadhia maji kwaajili ya shughuli hiyo.
Na pia vilikuwepo VITASA hivi vilikuwa ni vibaluli vidogo vya kuweza kushikwa kwa mkono, tofauti na Matasa ambayo yalikuwa yanabeba ujazo mkubwa wa maji, na vitasa ndio vile vinavyotajwa katika kitabu cha Ufunuo wa Yohana mlango wa 15 na 16.
Ufunuo 15:5 “Na baada ya hayo nikaona, na hekalu la hema ya ushuhuda mbinguni lilifunguliwa;
6 na wale malaika saba, wenye mapigo saba, wakatoka katika hekalu, wamevikwa mavazi ya kitani safi, ya kung’aa, wamefungwa vifuani mwao mishipi ya dhahabu
7 Na mmoja wa wale wenye uhai wanne akawapa wale malaika saba VITASA SABA vya dhahabu, vimejaa ghadhabu ya Mungu, aliye hai hata milele na milele”.
Ni nini tunajifunza katika hayo?
Tunachoweza kujifunza ni kuwa matasa ya Hekalu la duniani yalijaa maji ya kuoshea makuhani lakini vile VITASA vya Hekalu la mbinguni vimejaa hasira na hukumu ya MUNGU kwa wanadamu wasiomcha yeye.
Bwana atusaidie tumtafute, tusipotee wala kuangukia katika hukumu yake.
Maran atha.