by Admin | 22 January 2025 08:46 pm01
Kichwa cha kitabu hichi kinasema “Waraka wa kwanza wa Petro kwa watu wote” Kutuonyesha kuwa Petro Ndiye mwandishi.
Waraka huu mfupi aliuelekeza kwa watakatifu wote waliotawanyika, na kuishi kama wageni maeneo ya Asia ndogo ambayo kwasasa ni nchi ya Uturuki.
Maudhui makuu ya waraka huu tunaweza kuyagawanya katika sehemu kuu nne(4):
1) Ni kuwafariji watakatifu kwa kuwaeleza juu ya utukufu walioandaliwa mbinguni utakaofunuliwa siku ya mwisho. Na kwamba kwa kulitambua hilo basi wafurahi Katika majaribu mbalimbali ya imani, yaliyo ya kitambo tu.
2) Lakini pia unalenga kuwahimiza kuishi maisha ya utakatifu ya kumpendeza Mungu katika wakati wao wa kuishi hapa duniani.
3) Vilevile wajibu wakuishi maisha ya nidhamu katika Jamii ya wasioamini inayowazunguka.
4) Halikadhalika wajibu wa viongozi kulichunga kundi la Kristo kwa uaminifu wotena wajibu wa kanisa lote kumpinga shetani.
Haya ni maelezo mafupi juu ya kila kipengele:
Petro anawahimiza watakatifu kwamba wafurahi katika majaribu mbalimbali (kuliko kuhuzunika) kwa sababu ya uthamani mkuu wa imani yao itakayolipwa siku ile ya mwisho ambayo Yesu atafunuliwa kwetu.
1 Petro 1:6-7
[6]Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali;
[7]ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo.
> Petro Anahimiza kuiga kielelezo cha Kristo ambaye yeye alikubali kuteswa ijapokuwa hakutenda Dhambi, hata alipotukanwa hakurudisha majibu. Vivyo hivyo na sisi tukubali teso lolote kwa ajili yake katika upole wote, uvumilivu na ustahimilivu.
1 Petro 2:19-21
[19]Maana huu ndio wema hasa, mtu akivumilia huzuni kwa kumkumbuka Mungu, pale ateswapo isivyo haki.
[20]Kwa maana ni sifa gani kustahimili, mtendapo dhambi na kupigwa makofi? Lakini kustahimili, mtendapo mema na kupata mateso, huu ndio wema hasa mbele za Mungu.
[21]Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake.
1 Petro 4:12-16
[12]Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho.
[13]Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe.
[14]Mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo ni heri yenu; kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia.
[15]Maana mtu wa kwenu asiteswe kama mwuaji, au mwivi, au mtenda mabaya, au kama mtu ajishughulishaye na mambo ya watu wengine.
[16]Lakini ikiwa kwa sababu ni Mkristo asione haya, bali amtukuze Mungu katika jina hilo.
Sehemu hii ya pili Mtume Petro anawahimiza watakatifu, kuwa kwasababu wanatazamia neema itakayofunuliwa siku ya mwisho ya kuja kwake Yesu Kristo (1:13), hivyo hawana budi kuishi maisha ya kiasi na utakatifu hapa duniani.
1 Petro 1:13-16
[13]Kwa hiyo vifungeni viuno vya nia zenu, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo.
[14]Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu;
[15]bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;
[16]kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.
1 Petro 2:1-2
[1]Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote.
[2]Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;
> Petro anaendelea kuwasihi watakatifu waishi kama wapitaji duniani, kwa kuziepuka tamaa za mwili.
1 Petro 2:11
[11]Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho.
1 Petro 4:2-3
[2]Tangu sasa msiendelee kuishi katika tamaa za wanadamu, bali katika mapenzi ya Mungu, wakati wenu uliobaki wa kukaa hapa duniani.
[3]Maana wakati wa maisha yetu uliopita watosha kwa kutenda mapenzi ya Mataifa; kuenenda katika ufisadi, na tamaa, na ulevi, na karamu za ulafi, na vileo, na ibada ya sanamu isiyo halali;
> Anaeleza pia Wajibu wa kupendana kuhurumiana, kunyenyekeana, tuwe watu wasiolipa baya kwa baya, bali wenye kubariki(3:8-12, 4:7)
> Kadhalika pia anaeleza wajibu wa wanandoa. Kwamba wake wawatii Waume zao, na kujipamba kwao kunapaswa kuwe kwa mapambo ya rohoni, Lakini pia waume kuishi na wake zao kwa akili. (3:1-7)
Katika sehemu hii ya tatu anahimiza watakatifu kuwa na mwenendo unaopasa kwa watu wasioamini, ili wakose nafasi ya kutushitaki au kutulaumu kwa lolote.
> Anagusia katika eneo la watumwa Kwamba wawatii bwana zao, si wale tu wapole bali pia wale wakali.(2:18)
> Lakini pia Watakatifu waitii kila kilichoamriwa na mamlaka.
1 Petro 2:13-15
[13]Tiini kila kiamriwacho na watu, kwa ajili ya Bwana; ikiwa ni mfalme, kama mwenye cheo kikubwa;
[14]ikiwa ni wakubwa, kama wanaotumwa naye ili kuwalipiza kisasi watenda mabaya na kuwasifu watenda mema.
[15]Kwa sababu ndiyo mapenzi ya Mungu, kwamba kwa kutenda mema mzibe vinywa vya ujinga vya watu wapumbavu;
> Lakini pia anahimiza watakatifu wawaheshimu watu wote(2:17)
Mwishoni Petro anatoa wito wa waangalizi wa kanisa la Mungu (wazee), kwamba walichunge kundi kwa hiari, sio kwa kulazimishwa au kutazamia malipo ya kifedha, bali kwa moyo.
1 Petro 5:1-3
[1]Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye;
[2]lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo.
[3]Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi.
> Pamoja na hayo anasisitiza watakatifu wote wawe na kiasi na kukesha, kwasababu adui yetu ibilisi ni mfano wa simba angurumaye akitafuta mtu ammeze, hivyo wana wajibu wa kumpinga sikuzote.(5:8-9)
Hitimisho:
Hivyo kwa maelezo machache ni kwamba Petro analihimiza kanisa kutembea katika uvumilivu wote na uthabiti Wa imani, pamoja na utakatifu, na kutimiza wajibu wao katika utakatifu na adabu kwa wanadamu wote, katika wakati ambao kanisa linasubiria neema kuu itakayofunuliwa siku ya mwisho Yesu atakaporudi.
Na ndivyo ambavyo sote tunapaswa tuishi hivyo sasa.
Kama mkristo je unaendelea kufurahi katika majaribu? Unaishi maisha matakatifu? Unaishi vema na jamii yako? unaifanya kazi ya Mungu? Unampinga shetani kwa kudumu katika sala?
Ikiwa hayo, unayazingatia basi, wewe ni mshirika wa neema hiyo kuu ya Mungu itakayofunuliwa siku ya mwisho.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >>
https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Mwandishi na uchambuzi wa kitabu cha Wakorintho wa kwanza (1Wakorintho)
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/01/22/uchambuzi-wa-kitabu-cha-kwanza-cha-petro-1petro/
Copyright ©2025 unless otherwise noted.