Je Malaika wana maamuzi binafsi?

by Admin | 3 February 2025 08:46 pm02

Swali: Je Malaika wa mbinguni wana maamuzi binafsi kama tuliyonayo sisi wanadamu, mfano wakiamua kufanya jambo fulani wanafanya pasipo kuongozwa wala kuamuliwa?


Jibu: Maandiko yanatuonyesha kuwa viumbe pekee walioumbwa na Mwenyezi MUNGU walio na utashi ni Wanadamu pamoja na Malaika.

Na kama vile wanadamu tulivyo na utashi pamoja na maamuzi binafsi, (kwamba kuna mambo tunaweza kuamua wenyewe na mengine kuamuliwa) vile vile na malaika nao waliumbwa kwa mfumo huo huo,  wanayo maamuzi yao binafsi, na mengine kuamuliwa na MUNGU…

Na tena maamuzi mengine ya Malaika ni magumu kuliko hata yetu wanadamu..

Kwamfano tukirejea kabla ya Uasi wa shetani kule juu mbinguni, wakati ambao alikuwa ni malaika mkuu (Kerubi), biblia inatuambia kuwa ilifika wakati moyo wake ulinyanyuka na kuanza uasi, wa kutaka kuwa kama MUNGU, (yaani kuabudiwa).. sasa kitendo cha kuchukua hatua ya kutaka kuabudiwa hayo sio maamuzi madogo, na wala si hisia za kawaida… Kwahiyo malaika wa mbinguni na wale walioasi (yaani mapepo) wanayo maamuzi na hisia..

Sasa na malaika wengine wote wa mbinguni ni hivyo hivyo, wanayo maamuzi na hisia, na wana akili timamu…Ndio maana Bwana katika kutufundisha kuomba alisema tuombea “mapenzi ya yake yafanyike duniani kama kule juu mbinguni (Mathayo 6:10)”.

Ikiwa na maana kuwa mbinguni kuna shughuli zinaendelea, na malaika waliosalia mbinguni wanayafanya mapenzi ya MUNGU kila siku, na si kwamba wapo tu wamekaa wakisubiri amri Fulani!.. La wanaendelea na shughuli zao ambazo nyingi ya hizo sisi wanadamu hatuzijui, (lakini zote zipo ndani ya mapenzi ya MUNGU).

Zaidi tunaweza kusoma maandiko machache yanayozidi kutuonyesha kuwa Malaika wanayo maamuzi binafsi na ya kipekee..

Kutoka 23:20 “Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengezea. 

21 Jitunzeni mbele yake, mwisikize sauti yake; wala msimtie kasirani; maana, hatawasamehe makosa yenu; kwa kuwa jina langu limo ndani yake”.

Hapo anasema “huyo malaika” hatawasamehe, kuonyesha kuwa yeye si robot.. bali anatafakari na kapewa mamlaka na Mungu juu ya watu hao..soma tena Waamuzi 2:2-3.

Waamuzi 2:1 “Kisha malaika wa Bwana alikwea juu kutoka Gilgali kwenda Bokimu. Akasema, Mimi nimewaleta ninyi mkwee juu kutoka nchi ya Misri, nami nimewaleta hata nchi niliyowaapia baba zenu; nami nilisema, Mimi milele sitalivunja hilo agano langu nililoagana nanyi; 

2 nanyi msifanye agano lo lote na hawa wenyeji wa nchi hii; zipomosheni nchi madhabahu zao; lakini hamkuisikia sauti yangu; je! Mmefanya haya kwa sababu gani?

3 Basi kwa ajili ya hayo mimi nilisema zaidi, Mimi sitawafukuza watoke mbele zenu; lakini watakuwa kama miiba mbavuni mwenu, na miungu yao itakuwa ni tanzi kwenu.

 4 Ikawa, hapo huyo malaika wa Bwana alipoyanena maneno haya, kuwaambia wana wa Israeli wote, ndipo hao watu wakainua sauti zao na kulia”.

Tusome tena habari za Balaamu na Punda…

Hesabu 22:31 “Ndipo Bwana akafunua macho ya Balaamu akamwona malaika wa Bwana amesimama njiani, ana upanga mkononi mwake, umekwisha kufutwa naye akainama kichwa, akaanguka kifudifudi. 

32 Malaika wa Bwana akamwambia, Mbona umempiga punda wako mara tatu hizi? Tazama mimi nimekuja ili kukupinga, KWA SABABU NJIA YAKO IMEPOTOKA MBELE ZANGU,

 33 punda akaniona, akageuka upande mbele zangu mara tatu hizi; kama asingejiepusha nami, bila shaka ningalikuua wewe, nikamwacha yeye hai”.

Hapo Malaika anamwambia Balaamu kuwa njia za Balaamu zimepotoka mbele zake (huyo Malaika)

Lakini pamoja na na kwamba Malaika waliopo mbinguni wanayo maamuzi, lakini bado maamuzi yao hayavuki Neno la MUNGU,.. kwahiyo hawawezi kufanya lolote lililo kinyume na Neno la MUNGU, na wanafanya kazi pamoja na watu wa Mungu katika kuwahudumia (Soma Waebrania 1:14), na wanafurahi wanadamu wanapookoka.

Luka 15:10 “Nawaambia, Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye”.

Malaika walioasi, yaani shetani na mapepo yake hao wanafanya maamuzi yao, yaliyo kinyume na mapenzi ya MUNGU na ndio chanzo cha matatizo yote ya wanadamu leo.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/02/03/je-malaika-wana-maamuzi-binafsi/