Pazia la ushahidi ilikuwaje? Na lina ujumbe gani kiroho  (Walawi 24:3)

by Admin | 5 February 2025 08:46 am02

Jibu: Turejee…

Walawi 24:3 “Hapo nje ya pazia la ushahidi, ndani ya hema ya kukutania, Haruni ataitengeza tangu jioni hata asubuhi mbele za BWANA daima; ni amri ya milele katika vizazi vyenu”.

“Pazia la ushahidi” au kwa lugha nyingine “Pazia la Sitara” lilikuwa ni pazia lililotenga “patakatifu” na “Patakatifu pa patakatifu”.

Pazia hili lilisitiri eneo la ndani kabisa ya hema mahali palipokuwepo sanduku la Agano au sanduku la ushahidi.

Kipindi wana wa Israeli wapo jangwani wakitaka kuondoka eneo moja kwenda lingine walikuwa hawana budi kulivunja hema, na ili kulisitiri sanduku la agano mbali na macho ya watu wakati wanatembea, Bwana aliwaambia watumie pazia hilo la ushahidi linalotenga patakatifu na patakatifu pa patakatifu kulifunika hilo sanduku.

Na walipopiga makambi tena walilitengeneza hema na kilitumia hilo pazia kusitiri sehemu hizo mbili, hiyo ndiyo ilikuwa desturi yao.

Hesabu 4:5 “hapo watakapong’oa safari, Haruni ataingia ndani, na wanawe, nao watalishusha pazia la sitara, na kulifunika sanduku la ushahidi kwa hilo pazia” 

Sasa Pazia la sitara kiroho liliwakilisha kiambazi kulichotutenga sisi na rehema za Mungu, kwamba hapo kwanza hakuna mtu yeyote ambaye angeweza kupaingia patakatifu (ndani ya pazia) na kudai rehema isipokuwa kuhani mkuu tu, tena mara moja kwa mwaka, na dhambi zilifunikwa tu na hazikuondolewa.

Lakini Kristo alipokufa pale msalabani maandiko yanaonyesha kuwa hili Pazia la sitara lilipasuka kati kwa kati, vipande viwili.

Mathayo 27:50 “Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. 

51 Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka”.

Hiyo nikufunua kuwa sasa watu wote tunaweza kukikaribia kiti cha neema kupata rehema..

Waebrania 4:14 “Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu”

Ni neema kubwa sana tuliyonayo sasa ambayo haikuwepo zamani, watu wa kale walitamani kuipata neema hii tuliyonayo lakini hawakuipata.

Lakini swali kuu linabaki kwetu…Je tunaithamini hii Neema, au tunaichukulia tu kama kitu cha kawaida?.

Waebrania 10:29 “Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema?”.

Bwana atusaidie tusimame imara.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/02/05/pazia-ushahidi-ilikuwaje-na-lina-ujumbe-gani-kiroho-walawi-243/