NA TAA YA MUNGU ILIKUWA BADO HAIJAZIMIKA

NA TAA YA MUNGU ILIKUWA BADO HAIJAZIMIKA

Jina la Bwana na Mwokozi, Mkuu wa Uzima, Yesu Kristo lihimidiwe!..karibu tujifunze Biblia, Neno la Mungu.

Upo wakati ambao TAA ya Mungu itazima!.. Tuitikie wito wa Mungu, kabla ya huo wakati kufika..

1Samweli 3:2 “Ikawa wakati huo, Eli alipokuwa amelala mahali pake (tena macho yake yalikuwa yameanza kupofuka, hata asiweze kuona), 

3 NA TAA YA MUNGU ILIKUWA HAIJAZIMIKA BADO, na Samweli alikuwa amelala katika hekalu la Bwana, palipokuwa na sanduku la Mungu;

 4 basi, wakati huo Bwana akamwita Samweli; naye akasema, Mimi hapa.”

Sasa ili kuelewa vizuri Taa ya Mungu ni kitu gani, na ilikuwa inazimika wakati gani..hebu turejee ile Hema ambayo Musa aliagizwa aitengeneze, tunasoma Ilikuwa imegawanyika katika Sehemu kuu tatu, Ua wa Ndani, Patakatifu na Patakatifu pa patakatifu.

Na ndani katika Patakatifu, palikuwa na madhabahu ya uvumba, Meza ya mikate ya wonyesho pamoja na KINARA CHA TAA, ambacho kilikuwa na Mirija saba. (Tazama picha juu).

Hiki kinara cha Taa kazi yake ilikuwa ni kutia Nuru ile hema wakati wa USIKU. Kwamba Nyakati zote za usiku ni sharti ndani ya Hema kuwe na Nuru, na amri hiyo ilikuwa ni ya Daima, maana yake ya kila siku!.. haikupaswa hata Usiku mmoja upite bila Kinara hicho kuwashwa ndani ya Hema.

Kutoka 27: 20 “Nawe waamuru wana wa Israeli wakuletee mafuta ya zeituni safi ya kupondwa kwa ajili ya nuru, ili kufanya ile taa kuwaka daima. 

21 Ndani ya ile hema ya kukutania, nje ya hilo pazia, lililo mbele ya huo ushuhuda, Haruni na wanawe wataitengeza TANGU JIONI HATA ASUBUHI MBELE YA BWANA; itakuwa ni amri ya milele katika vizazi vyao vyote kwa ajili ya wana wa Israel”

Tusome tena..

Walawi 24:1 “Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 

2 Waagize wana wa Israeli kwamba wakuletee mafuta ya zeituni safi ya kupondwa kwa ajili ya ile nuru, ili hiyo taa iwake daima. 

3 Hapo nje ya pazia la ushahidi, ndani ya hema ya kukutania, Haruni ataitengeza TANGU JIONI HATA ASUBUHI MBELE ZA BWANA DAIMA; ni amri ya milele katika vizazi vyenu”

Hapo mstari wa 3, unasema ataitengeneza “tangu jioni hata asubuhi” maana yake wataiwasha tangu jioni mpaka asubuhi, na kukiisha pambazuka basi taa ile inazimwa, kwasababu kulikuwa na Nuru ya mwanga wa Nje wa jua iliyokuwa inaingia ndani ya Hema.

Sasa tukirudi katika habari hiyo ya Samweli,  maandiko yanasema Samweli alikuwa analala katika Hema karibu na sanduku la BWANA, na wakati ambapo Taa ya Mungu bado haijazimika..Maana yake bado hakujapambazuka, (kwasababu kukisha pambazuka tu, tayari ile taa ilikuwa inazimwa).

Wakati huo ndipo Samweli aliisikia Sauti ya Mungu ikimwita mara 4, na Samweli akaitikia wito wa Mungu.

Lakini ni nini tunajifunza katika hiyo habari?

Upo wakati ambao sauti ya Mungu inaita juu ya Mtu..na wakati huo ni wakati wa giza Nene juu ya maisha ya mtu.. Huo ndio wakati ambapo Mungu anamwita mtu, na anamwita kwa sauti ambayo inakuwa inayofanana na ya watu wa Mungu.. kiasi kwamba mtu anaweza kudhani ni mtu anayemwita/kumshawishi kumbe ni Mungu, ndio maana Samweli alipoitwa alikimbilia kwa Eli akidhani ni Eli anayemwita kumbe ni MUNGU.

Vile vile Mungu anawaita leo watu kutoka katika dhambi, na uvuguvugu lakini watu wanadhani ni wachungaji wao ndio wanaowaita, wengine wanadhani ni wahubiri ndio wanaowatafuta wawe washirika wao, pasipo kujua kuwa ni sauti ya Mungu ndio inayowaita na si watu.

Sasa endapo Samweli asingeitikia ule wito wakati ule ambapo TAA BADO HAIJAZIMIKA, huenda ile sauti ya Mungu asingeisikia tena kwa wakati ule mpaka labda kipindi kingine ambapo Taa hiyo itakuwa inawaka.

Ndugu TAA ya Mungu leo ni NEEMA,  Hii Neema kuna wakati itasimama!, na hakutakuwa tena na nafasi ya kumkaribia Mungu, wakati ambao unyakuo wa kanisa utapita, ndio wakati ambao TAA itakuwa imezima, vile vile wakati ambao utaondoka katika haya maisha huo ndio wakati ambao Taa ya Mungu itakuwa imezimika juu yako.

Je umemkabidhi Yesu maisha yako?.. Umebatizwa katika ubatizo sahihi? Umeokoka?.. Kama bado ni vyema ukafanya hivyo sasa kabla Taa haijazimika.

Mhubiri 12:1 “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo. 

Maran atha!

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Hema ya kukutania ni nini, na ilikuwaje?

IELEWE SAUTI YA MUNGU.

Kiango na Pishi ni nini (Mathayo 5:15)?

NAO WAKAMSHINDA KWA DAMU YA MWANA-KONDOO.

NYAKATI AMBAZO NI LAZIMA TUKUTANE NAZO TU:

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anna msemwa
Anna msemwa
9 months ago

Amen. Mungu abariki NENO lake. Nimejifunza na nimeelewa somo zuri .