NAO WAKAMSHINDA KWA DAMU YA MWANA-KONDOO.

NAO WAKAMSHINDA KWA DAMU YA MWANA-KONDOO.

Mafundisho maalumu kwa waongofu wapya: Sehemu ya tatu.

Ikiwa wewe ni mwongofu mpya, yaani umeokoka hivi karibuni, basi mafundisho haya yanakufaa sana katika hichi kipindi ulichopo.

Ikiwa ulipitwa na mafundisho ya nyuma, basi waweza kututumia ujumbe kwa namba zetu hizi +255693036618 tukakutumia mafundisho hayo.

Ni muhimu kufahamu kuwa, unapookoka yupo adui atakayesimama kinyume chako kukupinga wakati wote, ili uiache imani. Na huyo si mwingine zaidi ya shetani. Hivyo katika hatua hizi za awali, huna budi kufahamu silaha madhubuti za kuweza kumwangusha, Kwasababu ukizikosa ujue kuwa utakufa tu kiroho. Na silaha yenyewe tunazisoma katika vifungu hivi;

Ufunuo 12:9 “Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.
10 Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.
11 NAO WAKAMSHINDA KWA DAMU YA MWANA- KONDOO, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa”.

Jiulize hapo kwanini haijasema wakamshinda kwa mafuta ya upako, au kwa kanisa zuri, au kwa maombi ya vita.. Bali kwa damu ya Mwana kondoo na kwa neno la ushuhuda wao.
Kuna nini katika damu ya Yesu? Na ushuhuda ulionao?
Ni lazima ufahamu umuhimu wa damu yake, katika maisha yako ya wokovu.
Damu ya Yesu ilifanya mambo makuu matatu

  1. Kuondoa dhambi
  2. Kunena juu yetu
  3. kukanyaga nguvu za ibilisi

1) Kuondoa dhambi.


Biblia inasema..

Waebrania 9:22 “Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo”.

Katika agano la kale Utakaso wa kila namna, ulitegemea damu za wanyama, kwasababu ndio kanuni ya Mungu ya kiroho ya kuondoa dhambi, hivyo tangu zamani zile haikupatikana damu yoyote kamilifu isiyo na hila wala mawaa itakayoweza kuondoa dhambi za mtu moja kwa moja, bila kuacha kimelea chochote. Na ndio maana kumbukumbu la dhambi lilikuwepo wakati baada ya wakati , hivyo ilimpasa kuhani mkuu kila mwaka aingie kule hemani akiwa na damu ya wanyama ili kuwapatanisha wana wa Israeli,
Lakini sasa Yesu alipokuja, damu yake ilikuwa ni kamilifu zaidi ya wanyama, yeye tu ndiye aliyeweza, kusafisha na kuondoa kabisa dhambi ya mwanadamu isikumbukwe na Mungu milele, bila kuhitaji tena kuhani kila mwaka kwenda kuomba rehema kwa dhambi zilizotangulia.


Hii ikiwa na maana gani?
Ukiukosa ufunuo huu, kuhusiana na nguvu iliyopo katika damu ya Yesu iliyomwagika msalabani, basi ni ngumu sana, kuamini kama dhambi zako za kale Mungu alishazifuta na kuzisahau kabisa kabisa.
Ni kawaida kwa waongofu wapya kuletewa mawazo haya na ibilisi kwamba, bado Mungu anawaona ni wachafu, bado Mungu anakumbuka zile dhambi walizozitenda nyuma, zile mimba walizotoa, ule uzinzi walioufanya nje ya ndoa, rushwa walizokuwa wanakula, mauaji waliyoyafanya, waganga waliokuwa wanawafuata.


Hii ndio silaha kubwa ya ibilisi kwa waongofu wapya. Wanajiona kama vile bado hawajasamehewa vizuri, bado laana zinawafuatilia, Ndugu, ujue hayo ni mawazo ya shetani, kwasababu umekosa kujua gharama Yesu aliyoingia kwa ajili ya dhambi zako. Ile damu yake kumwagika, ilikuwa ni kukomesha dhambi zako zote na laana zako kabisa kabisa..


Ndio maana hapo biblia inasema, wakamshinda kwa damu ya mwana-kondoo, na ushuhuda wao, yaani ushuhuda wa kukombolewa na Yesu. Ndio silaha kubwa sana ya kumshinda ibilisi.
Hivyo mawazo kama hayo yakikujia yakatae, sema mimi nimeshasamehewa, ya kale yamepita, tazama yamekuwa mapya. Mimi sina deni la dhambi, Ukifanya hivyo, shetani atajua umeshafahamu nafasi yako, hivyo atakukimbia, na utaishi maisha ya amani na kutojihukumu.


2) Kunena juu yetu.


Damu pia inafanya kazi ya kunena.

Waebrania 12:24 “na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili”.

Kaini alipomuua ndugu yake Habili, Biblia inasema Mungu alimwambia Kaini sauti ya damu ya ndugu yake inamlilia kutoka ardhini (Mwanzo 4:10). Maana yake ni kuwa Mungu alikuwa anaisikia ili sauti ikinena, ikiomba, ikitaka haki itendeke, haikutulia tu.
Hata leo ukiona mtu anapitia majanga majanga fulani hivi, utasikia watu wakisema, ni kwasababu alimuua mama yake hivyo ile damu inamfuatilia..


Kuonyesha kwamba kuna uhalisia fulani katika damu ya mtu kupatiliza mema au mabaya.
Na ndivyo ilivyo kwa damu ya Yesu, inanena Mema, kuliko ile ya Habili, maana yake, hata sasa inazungumza, juu ya wale wote waliompokea yeye mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Inasema huyu anastahili kulindwa, huyu anastahili baraka, huyu anastahili furaha, huyu anastahili heshima, huyu anastahili kibali, afya n.k.


Hivyo wewe uliyeokoka ni wajibu wako kujua jambo hili, ili usiishi kama yatima hapa duniani. Ulipokuwa dhambini damu ya Yesu ilikuwa haineni juu yako, kwasababu haukuwa ndani ya agano lake. Lakini sasa upo, fahamu kuwa, Yesu anakuombea kila siku kwa Baba, hivyo kuwa na ujasiri ukijua kabisa nyuma yako ipo baraka, neema na habati wakati wote. Kwa jinsi siku zinavyozidi kwenda utayathibitisha hayo yote.

Warumi 8:33 “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki.
34 Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea”.

Hivyo mishale yote ya hofu, wasiwasi, mashaka, ambayo shetani atajaribu kukutumia ili urudi nyuma, ikatae, mishale ya kesho nitaishije, nikipoteza kile kwasababu ya Yesu itakuwaje? ondoa hayo mawazo ya kuangamia, kwasababu ipo damu inayonena kwa ajili yako usiku na mchana, ili utembee katika njia salama ya uzima.

Zaburi 27:1 “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani?
2 Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka.
3 Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini.
4 Neno Moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa Bwana Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari hekaluni mwake”.
Lishike sana hili, ukilikosa, shetani atatumia upenyo huu kukurudisha nyuma, kama alivyofanikiwa kuwarudisha wengi.


3) Kukanyaga nguvu za ibilisi.

Utajiuliza ni kwanini Bwana Yesu, hakulisema hili neno “IMEKISHWA”, Mahali popote katika huduma yake, mpaka siku ile alipopelekwa pale msalabani? Ni kwamba alijua hakuna kuzimaliza nguvu na utawala wa ibilisi bila agano la damu timilifu.


Hivyo aliposema IMEKWISHWA, Ni kweli ilikwisha, na ndio maana aliwaambia mitume wake maneno haya;

Luka 10:18 “Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme.
19 Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.

Ni lazima ujue kwa damu ya Yesu, shetani, hana nguvu yoyote juu yako. Kwamfano mwanajeshi dhaifu akitambua kuwa bomu alilonalo la nyuklia linaweza kuteketeza mji mzima, hataweza kuwa na hofu, na wanajeshi 1000 wenye nguvu, wanaomjia na bunduki zao. Kwasababu anafahamu akilituma tu kombora lake moja, kikosi chote kinakuwa jivu.


Ndivyo ilivyo kwako wewe uliyeokoka, fahamu kuwa hatua uliyopo, shetani hana nguvu zozote za kukushinda, kwasababu tayari nguvu zako ni nyingi kuliko zake, haijalishi hali yako ya uchanga kiroho. Hivyo, usiogope wachawi, usiogope mapepo, usiogope hata maadui zako. Lolote linalokuja mbele zako, uwe ni udhaifu, magonjwa, mashambulizi ya shetani, kemea kwa jina la Yesu, vitaondoka, usiwe mnyonge kwa shetani, kwasababu yule ni kama kinyago tu kinasimama hapo kukutisha, lakini hakina nguvu yoyote.
Hivyo zingatia sana kuyatafakari hayo.


Na Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

MAFUNDISHO MAALUMU KWA WAONGOFU WAPYA.

KAA MAJANGWANI.

USIMPE NGUVU SHETANI.

NIFANYE NINI ILI MUNGU AYAJIBU MAOMBI YANGU?

KUNA AINA NGAPI  ZA MAOMBI?

Nini maana ya “Nitaomba kwa roho, tena nitaomba kwa akili pia?

FUNGUO ZA UZIMA, MAUTI NA KUZIMU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
4 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
7 months ago

Amen

daudi
daudi
1 year ago

Mungu awabariki sana kwa mafundisho haya mazuri..kazi yenu ni njema sana

Blaise
Blaise
1 year ago

Jambo,
Naitaji kupata mafundisho kila mara nama ushuhuda.