NIFANYE NINI ILI MUNGU AYAJIBU MAOMBI YANGU?

NIFANYE NINI ILI MUNGU AYAJIBU MAOMBI YANGU?

Ukienda kuomba kazi yoyote halali, kikawaida huwezi kupewa majibu ya papo kwa papo na kuambiwa anza kazi leo, bila ya kutaka kwanza taarifa Fulani kutoka kwako, hata kama ni ile ndogo ya kufagia, vipo vigezo  vitaambatanishwa tu na kazi hiyo, aidha utaulizwa umri wako, au hali yako ya kiafya, au fani uliyonayo, au jinsia yako, au elimu yako n.k. Lakini ikiwa hujasoma vigezo vyao, halafu ukapeleka maombi yako kienyeji, Ni wazi kuwa barua yako itatupwa kapuni.

Vivyo hivyo na kwa Mungu, tunapopeleka maombi yetu, ni sharti tujue vigezo vya kujibiwa, vinginevyo, tutabakia kumlaumu Mungu, mbona tulifunga, na kukesha lakini hujasikia maombi yetu.

Hivi ndio vigezo kivuu vya maombi yetu kujibiwa na Mungu

  1. Kaa mbali na dhambi:

Hili ndio jambo la kwanza na la msingi; Dhambi ndiyo inayomdhoofisha Mungu, na kumdumaza kwenye eneo la kujibiwa maombi yetu.

Isaya 59:1 “”Tazama, mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia;

2 lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia”.

Hakikisha unakaa mbali na mambo yote yanayomchukiza Mungu, yaliyo ndani yako, mfano uzinzi, ulevi, uongo, rushwa, wivu, matusi n.k.

  1. Omba vizuri:

Kuomba vizuri, sio kupangalia maneno katika uombaji, hapana, bali kuomba jambo linalotimiza mapenzi ya Mungu.

Yakobo 4:2 “Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi!

3 Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu”.

Jiulize unachokiomba je kina  lengo gani, ni ili umkomoe yule adui yako?, au ili ukaongezee mtaji wa ile biashara yako ya bar?, au ili uonekane mwanamke wa kisasa mfano wa Yezebeli? Kama sivyo  ni Ili nini?..Fahamu kuwa Mungu anachunguza mioyo. Hakikisha unachokiomba ni kwa utukufu wa Mungu. Vinginevyo hutapokea chochote.

    3. Usiombe ili utazamwe na watu unajua kuomba:

Bwana Yesu alisema..

Mathayo 6:5 “Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao.

6 Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi”.

Mawazo yako yanapaswa yamwelekee Mungu, na sio Mungu Pamoja na wanadamu. Ukilijua hilo, basi hutaona sababu ya kujionyesha kwa watu ili wakupe utukufu.

     4. Omba kwa bidii:

Ukweli ni kwamba yapo maombi utahitaji kuonyesha bidii kwa Mungu ili uyapate, na sio kuomba dakika 5 halafu basi, hapo unaweza usipokee chochote, bali yakupasa kung’ang’ana mbele za Mungu ndipo yaje kutokea.

Yakobo 5:16 “… Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii.

17 Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita.

18 Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake.

Hivyo ongeza misuli yako ya maombi. Hata ya masafa mrefu na mikesha.

    5.  Usikate tamaa:

Yakupasa ujifunze uvumilivu. Uvumilivu ni muhimu sana ikiwa hujajibiwa leo, haimaanishi kuwa Mungu hajakusikia, bali omba tena kesho, na kesho kutwa, kwasababu ipo sababu kwanini hujakipata kwa muda huo.

Luka 18 : 1-8

18:1 “Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.

2 Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu.

3 Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu.

4 Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu,

5 lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima.

6 Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu.

7 Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?

8 Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani”?

    6. Jifunze kumtolea Mungu:

Ni jambo dogo, lakini linamatokeo makubwa sana rohoni. Sio kwamba Mungu anahaja na fedha zetu hapana, lakini umtoleapo unaonyesha upendo wako kwake. Ukipelekea maombi yako kwake, jijengee utaratibu pia wa kuambatanisha na sadaka, kwa kile ulichojaliwa, ikiwa ni senti mbili, au milioni 10, mpelekee Bwana. Wengi waliotenda hivi walifanikiwa.

Malaki 3:10 “”Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la”.

Hivyo kwa kuzingatia, mambo hayo sita, basi ni hakika Mungu atakujibu maombi yako. Na utamfurahia yeye.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

KUNA AINA NGAPI  ZA MAOMBI?

Nifanyeje niwe mwombaji mzuri, wa masafa marefu?

Namna ya kuomba

MLANGO MWINGINE WA ADUI KUTULETEA MAJARIBU.

JINSI YA KUPOKEA UPONYAJI, TUNAPOMWOMBA BWANA ATUGUSE MARA YA PILI.

Tofuati kati ya kifo na mauti ni ipi?

UNYAKUO WA KANISA UMEPITA LEO!!

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments