by Admin | 24 March 2025 08:46 pm03
Katika kanisa, Mungu aliweka huduma mbalimbali, karama mbalimbali, na utendaji kazi tofauti tofauti, ili kulikamilisha kanisa lake na kuupanda ufalme wake duniani kama alivyokusudia.
Sasa katika upande wa huduma, Mungu aliziweka huduma kuu tano, ambazo zenyewe zinasimama kama kuliongoza kanisa, kulikuza, kulichunga, ni kama nguzo za kanisa ambazo husimama wakati wote, Nao ni;
Mitume, manabii, wainjilisti, wachungaji na waalimu. (Waefeso 4:10-12)
Kwa urefu wa maelezo ya huduma hizo jinsi zinavyotenda kazi basi bofya hapa upitie >>> TOFAUTI YA MITUME, MANABII, WAINJILISTI, WACHUNGAJI NA WAALIMU NI IPI?
Lakini sambamba na hizo aliweka wengine katika kanisa, wanaoshirikiana na hawa watano (5).
Ambao ni WAZEE WA KANISA, MAASKOFU na MASHEMASI
Tuangalie kazi ya kila mmoja;
Tamaduni za kiyahudi tangu zamani walikuwa na desturi ya kuteuwa wazee (watu waliokomaa kiumri), wenye hekima na busara na uzoefu wa Kidini kufanya maamuzi na Kutoa hukumu mbalimbali katikati ya jamii ya wayahudi Soma (Kutoka 3:16, Kumbukumbu 1:9-18)
Hata baadaye kanisa lilipokuja kuanza, nyakati za mitume, tunaona bado walirithi utaratibu huo katika nafasi za kiuongozi ndani ya kanisa. Isipokuwa haikuhitaji awe ni lazima mzee Kiumri, lakini ni lazima Awe amekomaa Kiroho.
Nafasi hii hasaa iliwahusu wanaume, Kwasababu katika nyaraka za mitume hatuoni mahali popote kama kuna mfano wa mwanamke aliyeteuliwa kuwa mzee wa kanisa.
Ukisoma Tito 1:6, inaeleza sifa zao, anasema wazee wawe waume wa mke mmoja..
Tito 1:5-6
[5]Kwa sababu hii nalikuacha Krete, ili uyatengeneze yaliyopunguka, na kuweka wazee katika kila mji kama vile nilivyokuamuru;
[6]ikiwa mtu hakushitakiwa neno, naye ni mume wa mke mmoja, ana watoto waaminio, wasioshitakiwa kuwa ni wafisadi wala wasiotii.
(Matendo 14:23)
Zingatia: Hii haiwafanyi wanawake wasiwe na kazi yoyote katika kanisa hapana, wanaweza kusimama kama huduma-kivuli ambazo zaweza Kuonekana kama za wazee wa kanisa, waalimu, mashemasi, kama wasaidizi wenye huduma hizo, lakini sio rasmi kwao. Mfano wa hawa kwenye biblia walikuwa ni akina Fibi, prisila,
KAZI ZA WAZEE WA KANISA:
1). Kulichunga kundi,
Matendo 20:28
Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.
(Soma pia 1Petro 5:1-4)
ii) Kufundisha vema watu.
1 Timotheo 5:17
[17]Wazee watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha.
Tito 1:9
[9]akilishika lile neno la imani vile vile kama alivyofundishwa, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na kuwashinda wenye kupinga.
iii) Kutatua migogoro ya kiimani ndani ya kanisa.
Utakumbuka wakati ule makanisa ya mataifa yalikuwa yakitaabishwa, na wayahudi juu ya kushika torati, hivyo kukatokea mkanganyiko mkubwa, na kuwalazimu wawafuate wazee kule Yerusalemu ili walitatue tatizo hilo, na kama tunavyosoma baada ya hoja nyingi, walifikia hitimisho sahihi la Roho Mtakatifu.
Matendo 15:6 Mitume na wazee wakakusanyika wapate kulifikiri neno hilo.
7 Na baada ya hoja nyingi Petro akasimama, akawaambia, Ndugu zangu, ninyi mnajua ya kuwa tangu siku za kwanza Mungu alichagua miongoni mwenu ya kwamba Mataifa walisikie neno la Injili kwa kinywa changu, na kuliamini
iv) Kuwaombea wagonjwa.
Yakobo 5:14-15
[14]Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana.
[15]Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa.
2) MAASKOFU.
Maana ya Askofu ni mwangalizi.
Kazi yake kubwa ni kuliangalia kanisa,/ kulisimamia, mfano kusimamia malengo ya kikanisa, kulinda fundisho, na kusimamia uchungaji ulio bora.
Japokuwa mahali pengine maaskofu wanatajwa kama wazee wa kanisa. (Tito 1:5-9).
Lakini tofauti yao hasaa ni kwamba wazee wanayasimamia makanisa madogo madogo, lakini maaskofu ni waangalizi wa makanisa (yote/baadhi), Wazee wanaweza kuwa wengi, lakini maaskofu ni cheo, cha uangalizi hivyo aweza kuwa mmoja au wachache, wazee wanaweza kuwa na wajibu wa kufundisha, na kuchunga, lakini maaskofu hasaa katika kuongoza. Vilevile kwenye maandiko hatuoni mahali popote nafasi hii ikihusisha wanawake.
Sifa za maaskofu na wazee, wa kanisa zinafanana.
Sifa za mtu kuwa mzee wa kanisa. (Tito 1:5-9, 1Timotheo 3:1-7)
3) MASHEMASI.
Mashemasi ni mtumishi wa kanisa. Huduma hii ilitokea katika kanisa kwa mara ya kwanza, mitume walipokuwa wanahudumu na kuona kuwa baadhi ya mapungufu kwamba wajane wanasahaulika katika huduma ya kila siku, ndipo ikalazimika wateue watu saba, ndani ya kanisa watakaoweza kusimamia mambo yote ya kimahitaji ya kundi. (Matendo 6:1-7), mmojawapo alikuwa ni Stefano.
Kazi za mashemasi:
i) Kulihudumia kundi katika masuala ya mahitaji ya mwilini ya kundi:
Hususani kwa maskini, wajane, wenye mahitaji, mayatima.
ii) Kuongoza kwa mifano:
Lazima wawe kipaumbele kitabia, uaminifu, na nidhamu Na kuonyesha roho ya kiutumishi
iii) Kusimamia shughuli za kikanisa:
Ujenzi, taratibu za kiibada na mikutano, kusimamia hazina na mali za kanisa.
Sifa za mtu kuwa shemasi:
Zinatajwa kwenye 1Timotheo 3:8
1Timotheo 3:8 Vivyo hivyo mashemasi na wawe wastahivu; si wenye kauli mbili, si watu wa kutumia mvinyo sana,si watu wanaotamani fedha ya aibu.
9 wakiishika siri ya imani katika dhamiri safi. 10 Hawa pia na wajaribiwe kwanza; baadaye waitende kazi ya shemasi, wakiisha kuonekana kuwa hawana hatia.
11 Vivyo hivyo wake zao na wawe wastahivu; si wasingiziaji; watu wa kiasi, waaminifu katika mambo yote.
12 Mashemasi na wawe waume wa mke mmoja, wakiwasimamia watoto wao vizuri, na nyumba zao.
13 Kwa maana watendao vema kazi ya shemasi hujipatia daraja nzuri, na ujasiri mwingi katika imani iliyo katika Kristo Yesu
Hivyo wazee, maaskofu na mashemasi, ni nguzo muhimu za kulifanya kanisa kusimama, katika nidhamu ya kitabia na kimapokeo, pamoja na kihuduma.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Je huduma za mitume na manabii, zinaendelea kufanya kazi hadi sasa?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/03/24/maaskofu-mashemasi-wazee-wa-kanisa/
Copyright ©2025 unless otherwise noted.