by Devis | 9 June 2025 08:46 pm06
Akaabudu akiegemea kichwa cha fimbo yake.
Waebrania 11:21
[21]Kwa imani Yakobo, alipokuwa katika kufa, akambariki kila mmoja wa wana wa Yusufu, akaabudu akiegemea kichwa cha fimbo yake.
Ulishawahi kujiuliza ni kitu gani Yakobo alikuwa anawaonyesha wana wake siku ile alipokuwa anakaribia kufa.. kitendo cha yeye kusujudu kwa kuegemea kichwa cha fimbo?
Kwanini biblia iseme akaegemea fimbo na sio ukuta, au kitanda au au kiti au isikae tu kimya, bila kueleza chochote?
Yakobo alikuwa na maana kubwa kufanya vile, kwasababu hata alipokuwa akiwabariki watoto wa Yusufu (Efraimu na Manase) alipishanisha mikono..wakidhani kuwa amekosea, akawaambia sijakosea naelewa ninachokifanya, leo ndio tunajua kumbe alikuwa anaunda msalaba, ambao kwa kupitia huo neema inawafikia mataifa kwanza.
Vivyo hivyo na alipokuwa anakufa alisujudu kwa kuegemea kichwa cha fimbo, na huwenda watoto wake walistaajabishwa na kusujudu kule, pengine walijaribu kumwondoa pale ili asujudu vema, lakini akawaambia niacheni naelewa…
Fimbo kibiblia inafunua mamlaka ya mfalme, mchungaji na safari.
Yakobo hakuishi bila tegemeo la mchungaji…udhihirisho Ulikuwa ndio ile fimbo..kwasababu sikuzote alijiona kama kondoo wa Mungu, hakutaka kuiacha fimbo ya mchungaji wake, popote alipokuwepo kwasababu ndio faraja yake.
Daudi alisema…Bwana ndiye mchungaji wangu…gongo lake, na fimbo yake vyanifariji..
Zaburi 23:1-4
[1]BWANA ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu.
[2]Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza.
[3]Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
[4]Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.
Kwa ufupi ni kuwa palipo na fimbo ya mchungaji hapo hapo utaona Na kondoo wamejilaza. Yakobo alitembea na Kristo, Mpaka dakika ya mwisho wa maisha yake.
Lakini pia Fimbo inamfunua msafiri…zamani wasafiri walikuwa wanasafiri na fimbo kuwasaidia kutembea..
Wana wa Israeli walipokuwa wanajiandaa na safari ya kutoka Misri, utakumbuka usiku ule walipewa maagizo kila mmoja kushika fimbo yake.
Kutoka 12:11
[11]Tena mtamla hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya BWANA.
Kristo pia alipokuwa anawatuma wanafunzi wake katika ziara za injili aliwaagiza Kubeba fimbo zao..
Marko 6:8
[8]akawakataza wasichukue kitu cha njiani isipokuwa fimbo tu; wala mkate, wala mkoba, wala pesa za bindoni;
Hii ni kutufunulia kuwa Yakobo alikataa kuishi kama mwenyeji duniani.. bali msafiri..
Hivyo alitamani urithi wake ujue jumla ya mwenendo wa maisha yake hapa duniani ulikuwaje..
Hiyo ndio sababu kwanini historia za maisha ya watu kama hawa Mungu kazihifadhi tuzisome hadi leo.
Hata sasa, ujiulize je na Mimi je! fimbo ya mchungaji wangu(YESU KRISTO), ipo pamoja nami? ujiulize je mimi ni msafiri hapa duniani?
Fahamu tu Wazao wote wa Mungu huwakosi na fimbo ya Mungu, hiyo ndio alama yetu.
Shalom
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Yakobo alimaanisha nini kusema ‘ndipo BWANA atakuwa Mungu wangu’ Mwanzo 28:21
Kwanini Yakobo alimshinda Mungu, Je! Mungu huwa anashindwa na wanadamu?
Ni kwanini mifugo ya Yakobo iliongezeka kwa wingi kiasi kile?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/06/09/akaabudu-akiegemea-kichwa-cha-fimbo-yake/
Copyright ©2025 Wingu la Mashahidi unless otherwise noted.