by Nuru ya Upendo | 29 July 2025 08:46 am07
Je Mungu anaangalia mwili na kuihitaji?.. jibu ni Ndio!.. maandiko yanathibitisha hilo wazi kabisa..
1Wakorintho 6:13 “Vyakula ni kwa tumbo, na tumbo ni kwa vyakula; lakini Mungu atavitowesha vyote viwili, tumbo na vyakula. LAKINI MWILI SI kwa zinaa, BALI NI KWA BWANA, NAYE BWANA NI KWA MWILI”.
Nataka uone hayo maneno ya mwisho yanayosema “…mwili si kwa zinaa, BALI NI KWA BWANA, NAYE BWANA NI KWA MWILI”… Kumbe “miili yetu” ipo mahususi kwaajili ya “Bwana” na Bwana yupo mahususi kwaajili ya “miili yetu”.. Si ajabu tunapomwomba mahitaji ya mwilini anatujibu haraka sana kama tu vile ya rohoni.
Si ajabu tunapoteseka katika mwili hapendi, kwasababu miili yetu ni ya thamani sana kwake, kwaufupi ili tuwe wanadamu ni lazima tuwe na miili..
Sasa je! huu usemi ya kwamba Mungu haangalii mwili unatoka wapi?.. bila shaka ni kwa ibilisi!.
Maandiko yanazidi kusema kuwa “sisi si mali yetu wenyewe”
1Wakorintho 6:19 “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe”.
Tuzidi kusogea mbele katika andiko hilo… tujifunze ni kwa namna gani MWILI ni Kwa BWANA na BWANA ni kwa MWILI.
Muunganiko wa Miili yetu na Kristo ni mpana sana kiasi kwamba Biblia inatafsiri “viungo vyetu vya mwili ni viungo vya Kristo pia”.. maana yake huo mkono unaouona kama ni wako, kibiblia ni mkono wa Kristo, hayo macho si yako bali ni ya Kristo, kwahiyo kama umemwamini Yesu halafu ukaenda kufanya zinaa, maana yake umechukua kiungo cha Kristo na kukifanyisha zinaa..ndivyo Biblia inavyosema..
1Wakorintho 6:15 “Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha!”
Huo mguu unaoona ni wako kiuhalisia kama umeokoka si wako tena bali ni wa Kristo… ndio maana Bwana Yesu alisema mahali watakapowakaribisha basi wamemkaribisha yeye Kristo..na wakiwakataa wamemkataa yeye Kristo… kwanini?.. ni kwasababu miili yetu si mali yetu wenyewe baada ya kuokoka!, bali viungo vyetu vyote vinakuwa ni vya Kristo na vina mhubiri Kristo.
Luka 10:16 “Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma”.
Umeona??.. maana yake mtu aliyeokoka ni “Kristo anayetembea”.. ukiendelea kujifunza zaidi katika habari ile ya hukumu ya kondoo na mbuzi katika Mathayo 25:31-46… utaona wale watu waliuliza “ni lini Bwana tulipokuona una njaa, upo uchi tukakulisha na kukuvisha” ndipo Yesu atawaambia “kwa kadri mlivyowatendea wadogo wale basi walimtendea yeye”… wadogo wanaozungumziwa pale ni “watu wa Mungu wanaohubiri habari njema”.
Kwahiyo kumbe matumbo yenye njaa ya watu wa kweli wa Mungu ni matumbo ya Kristo, kumbe miguu yenye vumbi ya watu wa Mungu wa kweli ni miguu ya Kristo.. kwaujumla kumbe miili ya watu wa Mungu ni miili ya YESU mwenyewe!… si ajabu pale alisema “…nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha!”
Sasa kama ni hivyo kwanini unauvika mwili wako mavazi ya jinsia nyingine…je ni Kristo yupi unayemhubiri kwa uvaaji wako?..kwanini unafanya zinaa?, kwanini unachora mwili wako?, kwanini unauvutisha sigara na kuunywesha pombe?
Yachukulie haya kwa uzito mtu wa Mungu, wala si usipuuzie!, na kusema Mungu haangalii mwili?.. jihadharia na mafundisho ya uongo! Yanayokuambia kuutunza mwisho ni mafundisho ya sheria na vifungo!.. Tunapookoka hatujapewa uhuru wa kufanya dhambi!, La! Hatujafunguliwa kufanya dhambi!.
Siku ya mwisho hatutafufuliwa roho bali miili ndio itakayofufuliwa, na Kristo hakutoa roho yake kwa ukombozi wetu, bali mwili wake wenye damu, mifupa, mishipa, nyama, moyo, miguu, mikono, ngozi !.. vyote Kristo alivitoa kwaajili ya ukombozi wetu..
Waebrania 10:5 “Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari”.
Biblia inazidi kutufundisha kuitoa miili yetu kwa Bwana..
Warumi 12:1 “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana”..
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
MAAJABU YA AGANO LA UPENDO WA KRISTO.
Tofauti kati ya makuhani na walawi ni ipi?
Je Bwana YESU alimjibu Pilato au hakumjibu? Je biblia inajichanganya?
KILA MMOJA WENU AJUE KUUWEZA MWILI WAKE.
MTUMAINIE YESU ASIYEISHA MATUKIO.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/07/29/mwili-ni-kwa-bwana-na-bwana-ni-kwa-mwili/
Copyright ©2025 Wingu la Mashahidi unless otherwise noted.