MTUMAINIE YESU ASIYEISHA MATUKIO.

MTUMAINIE YESU ASIYEISHA MATUKIO.

Mtumaini Yesu asiyeisha Matukio. Jina la Bwana Wetu Yesu Kristo libarikiwe. Neno la Mungu linasema katika..

Yohana 21:25 “Kuna na mambo mengi aliyoyafanya Yesu; ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa”.

Kama ni Msomaji mzuri wa Biblia utagundua kuwa Injili zote nne za kwenye biblia yaani, Mathayo, Marko, Luka na Yohana, Zimeandika habari zinazofanana kuhusiana na Bwana Yesu Kristo. Lakini pia utagundua kuwa pamoja na kwamba zinalandana kwa sehemu kubwa lakini pia kuna habari ambazo utazikuta katika kitabu cha Mathayo ambazo hazipo katika Injili nyingine. Vivyo hivyo zipo ambazo utazipata tu katika kitabu cha Luka na hautaweza kuzipata katika kitabu kingine chochote cha Injili.

Kadhalika pia kuna habari ambazo utazipata katika kitabu cha Injili ya Yohana ambazo huwezi kuzipata katika Injili ya Mathayo au Luka wala Marko.

Kwamfano tunaweza kuona ile habari ya Mwanamke Msamaria. Ambaye alikutana na Bwana Yesu kisimani. Habari ile ipo tu katika kitabu cha Yohana Mtakatifu, na huwezi kuipata katika kitabu cha Mathayo au Luka au Marko. Hivyo endapo kitabu cha Injili ya Yohana kisingeandikwa pengine tungokosa tukio la Muhimu kama lile ambalo lilikuwa limebeba funzo kubwa sana kwetu.

Kadhalika kuna habari ya kufufuliwa kwa Lazaro. Tukio hilo pia ambalo Bwana Yesu alilifanya limeandikwa kwenye kitabu kimoja tu cha Yohana. Na halikurekodiwa katika vitabu vingine vya Injili.

Pia kuna Muujiza mwingine ambao Bwana Yesu aliufanya alipoingia mji mmoja unaoitwa Naini,

Pale alipomfufua mtoto wa pekee wa mwanamke mmoja mjane, ambaya alikuwa anachukuliwa kupelekwa makubirini kuzikwa.(Luka 7:11-17). Alimfufua akiwa ndani ya jeneza huku likiwa limebebwa na watu. Mji mzima ukaingiwa na hofu kwa tukio hilo.

Vivyo hivyo kuna tukio lingine tena ambalo tunalisoma katika kitabu cha Mathayo peke yake. Ambalo halipatikani katika vitabu vingine vya injili. Na tukio hilo ni lile la kunyanyuka kwa miili ya watakatifu waliokuwa wamelala makaburini, na kuuingia mji mtakatifu na kuwatokea wengi..(Mathayo 27:51). Tukio hilo endapo kitabu cha Mathayo kisingekuwepo tusingelifahamu.

Kadhalika na matukio mengine mengi ni hivyo hivyo. Utayakuta kwenye Injili hii lakini kwenye nyingine usiyakute. Kwahiyo tunaweza kusema endapo kila Mtume wa Bwana Yesu au kila mtu aliyemjua Bwana angepewa fursa ya kuandika mambo aliyoyaona kwa Bwana Yesu katika kipindi chote alichokuwepo nao duniani. Ni wazi kuwa tungesikia mambo ya ajabu sana ambayo yangetushangaza au hata pengine kutushtusha.

Ndio maana Biblia inasema..

Yohana 21:25 “Kuna na mambo mengi aliyoyafanya Yesu; ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa”.

Leo hii kuna mamilioni ya vitabu yaliyoandikwa ulimwenguni kote. Kila sekunde yanachapishwa mapya, Lakini pamoja na mavitabu yote hayo bado hayajaujaza ulimwengu. Ili Neno “kuujaza ulimwengu” litimie inapaswa ukipita barabarani unakanyaga vitabu tu. Barabarani kote kumejaa vitabu tu, na kila kitabu kinaeleza habari tofauti na kingine, sio Nakala. Hebu tafakari ni mambo mangapi aliyafanya Yesu?.

Kwa ufupi kila sekunde kulikuwa na tukio la kimiujiza alikuwa analifanya. Kila sekunde kulikuwa na Neno la kinabii alilokuwa analitoa. Endapo Mariamu mama yake Yesu na yeye angepewa fursa ya kuelezea kwa maandishi mambo aliyoyaona kutoka kwa Bwana, tangu anazaliwa mpaka anaondoka duniani..pengine angeandika vitabu vyake 2000. Ni wazi kuwa kuna mambo mengi yakimiujiza ujiza yalikuwa yanatokea hata wakati anafanya kazi zake za useremala. Hayajaandikwa tu! Endapo Yusufu babayake angepewa fursa ya kuyandika tungesikia mengi.

Mke wa Pilato ambaye alimwona Bwana Yesu katika ndoto siku ile usiku kabla ya kusulibiwa, akamwambia mume wake,amwaache mtu huyu ni wa haki lakini mume wake hakusikia. Naamini angepewa fursa ya kuandika aliyoyaona kwenye ile ndoto kwa urefu kuhusu Yesu, angeandika vitabu viwili.

Wale walinzi ambao walishuhudia kufufuka kwake, walikuwa na mengi ya kuelezea.

Laiti wangepata fursa ya kuelezea kwa maandishi, Leo pengine tungesikia mambo ya ajabu sana Zaidi ya yale tunayoyajua yaliyotokea pale kaburini. N.k n.k

Hata sasa endapo mambo anayoyafanya katikati ya watu, kila mmoja akapewa tu fursa ya kuandika mambo machache aliyofanyiwa na Yesu. Jiulize ni vitabu vingapi vingechapishwa duniani? Mabilioni ya vitabu. Sasa kwanini mtu wa namna hii tusimtumainie aliyejaa matukio kiasi hichi?.

Hakuna mwanadamu yoyote ambaye alishawahi kutokea aliyefanya mambo mengi kama Yesu. Kama hayupo basi Huyu Yesu ndiye wa kumtumainia. Hadi sasa tunavyoongoa mtu ambaye ni maarufu wa kwanza duniani, tangu miaka 2000 iliyopita hadi sasa, mtu ambaye anazungumziwa zaidi sasa sekunde hii tu tunayozungumza kuliko watu wengine wote ni YESU KRISTO.

Hivyo nakutia moyo wewe unayemtumaini Yesu, kamwe usifikirie hata siku moja kwenda kutafuta msaada kwa mwingine, au kwa wanadamu ambao historia ya Maisha yao kama ikiandikwa ni kitabu kimoja au viwili. Haizidi hapo. Na tena hivyo viwili ni imerefushwa sana. Lakini Bwana Yesu kwa kipindi tu kile kifupi alichoishi duniani tayari matukio yake hata ulimwengu usingetosha. Bwana Yesu ndiye Mkuu wa Uzima, Ngome Imara. Na msingi wa kutegemewa milele. Mwamba wetu, kimbilio letu tegemeo letu, boma letu, fungu letu, na msaada wetu wa kwanza na wa mwisho.

Kama hujampokea upo hatarini sana.

Hivyo ni vyema ukafanya mageuzi haraka kabla muda wako wa kuishi duniani haujaisha. Tubu na yeye atakusamehe kabisa bure, Fikiria wokovu umegharamiwa hivyo, na unatolewa kirahisi hivi..Tubu tu na umfuate naye atakuondolea mzigo mzito wa dhambi ulionao na atakupa tumaini la Uzima wa Milele.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali share na wengine


Mada Nyinginezo:

Je! ni sahihi kwa Mkristo kusherekea siku yake ya kuzaliwa.[Birth day]?

Maswali kuhusu Bwana Yesu.

“Ninyi ni chumvi ya dunia” Andiko hilo lina maana gani?

TUMAINI NI NINI?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Baya kahindi
Baya kahindi
2 years ago

Someni bibilia na kufwata sheria zake.