NAFASI YA MWANAMKE KATIKA KANISA

by Admin | 19 July 2018 08:46 pm07

Nafasi ya mwanamke katika kanisa ni ipi? Je anaruhusiwa kuwa mchungaji, au askofu?

Mtume Paulo alisema,..

 1Wakoritho 14;34 “Wanawake na wanyamaze katika kanisa, maana hawana ruhusa kunena bali watii, kama vile inenavyo torati nayo. Nao wakitaka kujifunza neno lo lote, na wawaulize waume zao wenyewe nyumbani mwao; maana ni aibu wanawake kunena katika kanisa. Au je! Neno la Mungu lilitoka kwenu? Au kuwafikia ninyi peke yenu? Mtu akijiona kuwa ni nabii au mtu wa rohoni, na ayatambue hayo ninayowaandikia, ya kwamba ni maagizo ya Bwana”

Hapa maandiko yanaweka wazi kabisa mwanamke hana nafasi ya uongozi wowote katika kanisa, au kutatua tatizo lolote katika kanisa, Mungu aliuweka huu utaratibu, kulifundisha kanisa, maana mwanamke anawakilisha kanisa la Kristo, na kama vile kanisa limtiivyo Kristo katika kila Neno vivyo hivyo na wanawake wanapaswa kujitiisha chini ya waume zao ikiwemo kuongozwa kwa kila jambo kama maandiko yanavyosema kwenye..

 Waefeso 5:22-23Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. 

23 Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili.

24 Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo.   Kwahiyo mwanamke hajapewa mamlaka yeyote ya kumtawala mwanamume iwe kanisani au nyumbani, Kichwa cha mwanamke ni mwanamume na kichwa cha mwanamume ni Kristo.

Sasa zile huduma tano zilizozungumzwa katika waefeso 4:11( “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe”) hizi zilitolewa kwa wanaume tu ,ofisi hizi tano ni za uongozi katika kanisa hakuna hata moja inayomhusisha mwanamke. ikiwemo maaskofu na mashemasi wote wanapaswa wawe wanaume.

Na Bwana Yesu alitoa sababu katika

 1timotheo 2:11-14 ” Mwanamke na ajifunze katika utulivu, akitii kwa kila namna.Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu. Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye.Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa.”

kwahiyo hapa tunaona kuwa Hawa ndiye aliyedanganywa na sio Adamu. Na Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, kama tu vile sisi tunavyowatii wazazi wetu pasipo shuruti na kuwaheshimu na kuwapa mamlaka yote katika familia ni kwasababu wao ndio waliotutangulia kwanza duniani na ndio waliotuzaa, lakini tunawapa heshima yao je! si zaidi kwa mwanamke kumtii Adamu aliyetoka katika ubavu wake na ndiye aliyeumbwa wa kwanza??..

Kuna baadhi ya wanaojiita watumishi wa Mungu wanaoingiza harambee za kijamii katika kazi ya Mungu na kufundisha kuwa kila kitu mwanaume anachofanya, mwanamke pia anaweza kufanya, hawajui kwamba wanaenda nje ya mpango wa Mungu kwa maana kila jambo Mungu aliweka kwa utaratibu na kwa kulifundisha kanisa.

Tunaona mitume 12 wote wa Bwana Yesu walikuwa ni wanaume, katika agano la kale hakuwahi kuwa na kuhani mwanamke, ilikuwa inafahamika hivyo tangu awali shughuli zote zinazohusu madhabahu ya Bwana zilikuwa zinafanywa na wanaume, lakini mambo haya yalianza kujitokeza ilipofika kuanzina karne ya 20 mpaka leo wanawake walipoanza kutafuta haki sawa ndipo hapo walipoanza kujiingiza katika siasa, na  leo hii shetani amefanikiwa kuingiza hiyo roho katika kanisa na kufanya madhabahu ya Mungu itawaliwe na wanawake. Haya ni machukizo mbele za Mungu, na ni dhambi yenye uzito ule ule sawa na wasiokuwa wa kabila la walawi kuhudumu katika nyumba ya Mungu kwenye agano la kale.

Swali ni je! wanawake wanaofanya hivyo Mungu hayupo nao??

Ni siri kubwa imekaa hapo ambayo watu wengi hawaijui, wanapoona mtu anatenda miujiza, vipofu wanaona, unabii unatolewa n.k. wakidhani ndio uthibitisho kuwa mtu huyo yupo katika njia sahihi biblia inasema

Mathayo 7:22-23 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.

22 Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?

23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.”

Kwahiyo tunaona haijalishi unatenda miujiza kiasi gani, uthibitisho pekee wa Mungu kuwa na wewe ni kuyatenda mapenzi ya Mungu ambayo ni kuishi katika Neno lake, na NENO lake ndilo hilo

Mwanamke na ajifunze katika utulivu, akitii kwa kila namna.Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu ” 

Kwahiyo yoyote aendaye kinyume na hayo anaenda nje ya maagizo ya Bwana haijalishi ni miujiza kiasi gani inatendeka kwenye huduma yake, anafanya kazi isiyokuwa na faida.

Je! kazi ya mwanamke ni ipi katika kanisa?
Kuna zile karama Mungu alizitoa kwa wote, kwa mwanaume na mwanamke. (ijulikane kuwa karama ni tofauti na huduma) ukisoma..

1wakoritho 12:4-10 ” Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule.

Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule.

Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.

Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; ” 

 Hivyo basi Mungu anaweza kumtumia mwanamke kutoa unabii/ujumbe katika kanisa lakini sio kufundisha. Mungu anaweza kumtumia mwanamke kuponya wagonjwa, kunena kwa lugha, kutoa unabii, hizi zote ni karama za Mungu na anaweza kumtumia yeyote, lakini zile huduma ambazo ni ofisi kuu tano yaani, mitume, manabii, wainjilisti,waalimu na wachungaji, ikiwemo na mashemasi, hizi ni huduma za uongozi wa kanisa, na hazimuhusu mwanamke hata kidogo.

Wanawake wanapaswa kujifunza, kwa kuuliza maswali kwa mtu yeyote ikiwemo mchungaji wake yahusuyo masuala yake ya kiroho na pia kuruhusu karama za Mungu kutenda kazi ndani yake, ikiwemo, kunena kwa lugha, kutoa unabii, uponyaji, ishara na miujiza, ndoto,kumsifu na kumwimbia Mungu wao, na kushuhudia wengine katika nafasi uliyopo kwa jinsi Mungu atakavyokujalia.

Isipokuwa kufundisha au kuhubiri kanisani au kumtawala mwanaume kwa namna yoyote na kufungua huduma na kujiita mchungaji, au mwinjilisti au askofu au mwalimu au mtume ni makosa, kama ulishawahi kufanya hivyo pasipo kujua jirekebishe na ukae katika nafasi uliyoitiwa.

Mungu akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

TUZO UTAPEWA KULINGANA NA NAFASI YAKO.

NJIA KUU YA KUINGIA KATIKA ULE MJI.

KWANINI MUNGU ANAMPA NABII HOSEA MAAGIZO YA KUMUOA MWANAMKE KAHABA? (HOSEA 3)

KUTOKA 10:1 “BWANA ANASEMA ATAMPA FARAO MOYO MGUMU, ASIMTII, JE! HAPO BWANA ATAMHUKUMU FARAO KAMA MKOSAJI SIKU ILE?”


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2018/07/19/nafasi-ya-mwanamke-katika-kanisa/