by Admin | 1 September 2019 08:46 pm09
JIBU: Kuongoka maana yake ni kugeuka au kutubu..Katika habari hiyo tunasoma..
Luka 22: 31 “Akasema [YESU], Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano;
32 lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe UTAKAPOONGOKA waimarishe ndugu zako.
33 Akamwambia, Bwana, niwapo pamoja nawe, mimi ni tayari kwenda gerezani au hata kifoni.
34 Akasema, Nakuambia, Petro, jogoo hatawika leo, kabla wewe hujanikana mara tatu ya kuwa hunijui.”
Tunaona hapo Bwana alishafahamu kuwa wakati wa mamlaka ya giza umefika, kwa Bwana pamoja na wanafuzi wake katika muda mchache mbeleni watatiwa chini ya yule mwovu, na ndio maana kwa kulijua hilo kuwa wanafunzi wake watashindwa kustahimili majaribu pasipo msaada wake, alimwambia Petro maneno yale, “Nimekuombea wewe ili imani yako isitindike”, kwasababu shetani atakwenda kuwapepeta kama ngano, hivyo inaweza ikawapelekea kuikana Imani mara moja, na kurudi nyuma kuacha kabisa kuambatana na Bwana…
Tena Bwana akamwambia nimekuombea ili Imani yako isitindike pale utakapojaribiwa, na utaona jaribu lile lilikuwa ni kumkana Yesu mara tatu muda mchache baadaye, hivyo kama Bwana asingemuombea angeweza kujinyonga kabisa kama Yuda au kuacha kabisa kuambatana na njia ya Kristo badala ya Kuongoka(kutubu). Utakuja kuona Wale wanafunzi wengine walikuwa tayari katika mashaka ya kuiacha imani..Hivyo Bwana alimchagua Petro ili baada ya yeye kutubu (kuongoka) kwa machozi pale alipata nguvu ya kwenda kuwaimarisha na wale wanafunzi wengine waliokuwa wametawanyika.
Na ndio maana baada ya Bwana kufa Petro ndiye alikuwa anashughulika kuwakusanya wanafunzi wote, hata wakati wa kwenda kuvua samaki wanafunzi wengine walitaka kwenda nae, utaona pia yeye ndiye aliyetoa pendekezo la kuteuliwa mwanafunzi mwingine mahali pa Yuda kadhalika hata katika siku ile ya Pentekoste Petro ndiye alikuwa wa kwanza kufungua kinywa na kuwaeleza watu upya habari ya maneno ya wokovu kwa nguvu nyingi…Kwahiyo Petro alishughulika sana kuwaimarisha ndugu zake (mitume) waliokuwa naye.
Kadhalika hili neno KUONGOKA, limeonekana katika
1Timotheo 3: 2 “Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha;
3 si mtu wa kuzoelea ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole; si mtu wa kujadiliana, wala asiwe mwenye kupenda fedha;
4 mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu;
5 (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?)
6 WALA ASIWE MTU ALIYEONGOKA KARIBUNI, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi.
7 Tena imempasa kushuhudiwa mema na watu walio nje; ili asianguke katika lawama na mtego wa Ibilisi.”
Sasa hapo neno hilo limetumika kwa mtu aliyetubu hivi karibuni (yaani kumpa Bwana maisha yake hivi karibuni)..Mtume Paulo alitoa maagizo kwamba kazi ya uaskofu inahitaji mtu aliyedumu kwa muda fulani mrefu katika Imani, ili isiwe rahisi kwa mtu huyo kunaswa na mitego ya ibilisi kiwepesi.
Tunajifunza nini?..Kama tu vile shetani alivyowataka mitume kuwapepeta kama ngano, na sisi vivyo hivyo anatutaka leo kutupepeta, na nia yake ni tuikane imani, hivyo wewe kama mkristo ni jukumu lako kudumu katika fundisho la mitume(biblia), na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali, kama maandiko yanavyotuagiza katika (Matendo 2:42 ). Ili uwe na nguvu ya kushinda mawimbi ya shetani.
Ubarikiwe sana.
Mada zinazoendana:
NINI TOFAUTI YA HAYA MANENO. 1) KUOKOKA, 2) WOKOVU, 3) KUONGOKA?
UKIAMINI NA UKIMKIRI YESU KWA KINYWA CHAKO, UTAOKOKA.
ALIYE MKUU KATIKA UFALME WA MBINGUNI.
NI WAKATI GANI SHETANI ANAPENDA KUMSHAMBULIA MWAMINI?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/09/01/petro-aliambiwa-na-bwana-yesu-ukiongoka-waimarishe-na-ndugu-zako-je-kuongoka-maana-yake-nini/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.