Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.

by Admin | 1 September 2019 08:46 pm09

SWALI: Yesu alikuwa na maana gani alipomwambia yule Mama kwamba chakula cha watoto hawapewi mbwa?

JIBU: Tusome,

Mathayo 15: 21 “Yesu akaondoka huko, akaenda kando pande za Tiro na Sidoni.
22 Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo.
23 Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu.
24 Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.
25 Naye akaja akamsujudia, akisema Bwana, unisaidie.
26 Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.
27 Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao.
28 Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile”.

Kumbuka Bwana Yesu alipokuja duniani, hakutumwa kwanza kwa watu wa mataifa, hapana kwasababu wao hawakuwa wanamtazamia mwokozi yeyote, kadhalika watu wa mataifa walikuwa ni watu wasiokuwa ni dini, wapagani, wasiomjua Mungu, walikuwa wanaabudu miungu,na ndio maana Bwana akawafananisha na mbwa katika mfano huo…

Lakini wayahudi ni watu wa Mungu tangu zamani uzao wa Ibrahimu, pamoja na hayo kwa miaka mingi walikuwa wanalitazamia taraja la wokovu wao ambalo lingeletwa tu na MASIHI mwenyewe atakayeshuka kutoka mbinguni, Hivyo kwa kuwa wale ni uzao wa Mungu, uzao wa Ibrahimu, sasa ulipofika wakati wa Mungu kuwatimizia haja yao waliyokuwa wanaisubiria kwa muda mrefu, ndio akamleta Bwana Yesu duniani aje kuwakomboa..

Na ndio maana sasa tunamwona Bwana Yesu alipokuwa duniani, hakuhubiri katika nchi yoyote ya mataifa, kadhalika hakuwatuma hata wanafunzi wake katika mji au kijiji chochote cha mataifa, kwasababu hakutumwa kwao, bali kwa wale waliomtazamia (yaani wayahudi).

Lakini hapa tunamwona huyu mwanamke ambaye ni mtu wa Tiro, (mwanamke aliyekuwa wa kimataifa), asiyekuwa na dini wala Imani katika Mungu wa kweli, alipomwona Bwana akipita kando kando ya miji yao, akamfuata ili ahudumiwe naye, lakini Bwana hakuonyesha kumjali kwa namna yoyote ile, lakini kwa vile alivyokuwa akimsumbua sumbua, ndipo Bwana akamwambia sikutumwa [kwa watu wa mataifa] ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli (yaani wayahudi)..lakini alipozidi kumsumbua sumbua, aliongezea na kumwambia “si vema kutwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa”..yaani akiwa na maana kuwa si vizuri kuiondoa ile neema ya wokovu kwa wale waliostahili kuipokea(yaani wayahudi) na kuwapatia watu ambao hawakustahili kuipokea au kuitazamia(watu wa mataifa).

Lakini pamoja na hayo tunakuja kuona baadaye, ile neema ililetwa kwetu sisi mataifa, baada ya wale ambao waliostahili kuipokea kuikataa, hivyo sisi sasa sio mbwa tena bali tumefanywa kuwa wana wa Mungu kwa damu ya Yesu Kristo.

Hiyo ndio siri iliyokuwa imefichwa tangu zamani kwamba sisi watu wa mataifa tumehesabiwa kuwa warithi wa wokovu sawa na wayahudi kwa njia ya Yesu Kristo. Haleluya. Hivyo ndio maana Mtume Paulo akasema katika..

Waefeso 3: 4 “Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake Kristo.
5 Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho;
6 ya kwamba MATAIFA NI WARITHI PAMOJA NASI WA URITHI MMOJA, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili;”

Hivyo somo la kujifunza, hapo ni lipi?. Tumwendeapo Mungu, kwa haja ihusuyo wokovu wetu, hata kama ni kweli tutakuwa hatustahili mbele za Mungu, pengine njia zetu zimekuwa mbaya sana, na tumeomba mara ya kwanza, na ya pili na ya tatu hatujajibiwa…Hatupaswi kukataa tamaa, tuzidi kuomba tuzidi kuomba kama yule mwanamke..Kwasababu Bwana Yesu alishatupa mfano unaofanana na huo, juu ya yule kadhi dhalimu, aliyekuwa hamchi Mungu, lakini yule mwanamke mjane alivyomwendea mara ya kwanza hakupewa haki yake, lakini kwa jinsi alivyokuwa akimwendea endea mara kwa mara, alimpatia haki yake, japo hamchi Mungu, ili asije akamsumbua daima…(Luka 18:1-8)

Vivyo hivyo na sisi tusiache kumwomba Mungu neema ya wokovu, neema ya uponyaji, mahitaji binafsi, hata kama hatutaona dalili zozote za kujibiwa maombi yetu. Kwasababu Mungu anapendezwa na mtu aombaye kwa bidii.

Ubarikiwe.

Ikiwa utahitaji msaada zaidi ya mafundisho ya kila siku/maombezi/ubatizo/ushauri basi wasiliana nasi kwa namba zetu hizi +255693036618/+2557890001312

Au jiunge na makundi yetu ya mafundisho ya kila siku kwa kwa njia ya Whatsapp kwa kubofya hapa >>>> WHATSAPP GROUP


Mada zinazoendana:

JINSI YA KUITUMIA VYEMA NEEMA YA MUNGU ILIYO JUU YANGU.

MPAKA UTIMILIFU WA MATAIFA UTAKAPOWASILI.

MADHARA YA KUUPIZIA MAAGIZO YA MSINGI MUNGU ANAYOKUPA.

NINI MAANA YA KUISHI KWA KUUKOMBOA WAKATI?

CHANZO CHA MAMBO.

MAVAZI YAPASAYO.


 

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/09/01/si-vema-kukitwaa-chakula-cha-watoto-na-kuwatupia-mbwa/