Nitajuaje kama ndoto ni ya Mungu au ya Shetani?

by Admin | 3 Septemba 2019 08:46 mu09

JIBU: Maarifa yanayohusiana na ndoto ni mapana kidogo, lakini kwa ufupi, zipo ndoto za aina tatu,  

1) Ndoto zinazotokana na shughuli (Mhubiri 5:3): hizi ndio mara nyingi zinamjia mtu, kwamfano mtu alikuwa anafanya shughuli fulani siku nzima na usiku anapolala bado anaota anaifanya ile shughuli au anaota mambo yanayoendana na jambo ambalo amekuwa akijishughulisha nalo mara kwa mara. Sasa Kutokana na shughuli ile kuchukua sehemu kubwa ya siku yake au maisha yake, inapelekea pia kuchukua nafasi kubwa katika ulimwengu wa ndoto zake. Ndoto hizi ni mwili ndio unaozitengeneza, hazitokani na Mungu wala shetani.  

2) Ndoto zinazotokana na yule mwovu. Hizi zinatengenezwa na yule mwovu na kutumwa ndani ya mtu, Hizi ni ndoto zote zenye maudhui ya kumfanya mtu aikane au aiache IMANI, au zinampelekea mtu aende mbali na mpango wa Mungu, au kutenda dhambi na huwa zinaambatana na ushawishi fulani mkubwa sana mara baada ya kuamka.  

kwamfano mtu anaota kaachana na mume/mke wake na kupata mke/mume mwingine ambaye ni mzuri kuliko yule aliyekuwa naye, na anapoamka asubuhi anajikuta anaanza kuona kero ya kuishi na mke wake au mume wake kama ilivyokuwa hapo mwanzo. Au anashawishika kuamua kumwacha mumewe au mkewe.  

Au mtu anaota mzazi wake mmoja ni mchawi na hamtakii mema, na ile ndoto inamtaka ajitenge na huyo mzazi, au amchukie awe naye mbali. Au mwingine anaota anafanya uzinzi/uasherati na mtu asiyemjua au anayemfahamu, na anajikuta akiamka asubuhi ile roho ya tamaa bado inakuwa ndani yake kwa nguvu zaidi, tofauti na alivyokuwa jana.  

Au mtu anaota kapata utajiri kwa kumwibia mwajiri wake, au kwa kucheza kamari , na baada ya kuamka anajisikia msukumo ndani yake wa kwenda kufanya jambo lile na wakati mwingine mazingira aliyoyaona kwenye ndoto ndio hayo hayo anayaona akiwa nje ya ndoto kana kwamba ni unabii unatimia..  

Au wakati mwingine mtu anaota ndoto ameenda kwa mganga, akafanikiwa na anapoamka anashawishika kufanya mambo yale, au mtu anajikuta anaota kuna sanamu mahali fulani au kuna mti mahali fulani umebeba mafanikio yake (pengine uani kwake) na kwenye ndoto anaona ameukata ule mti na mambo yote yakaharibika, na anapoamka anajikuta anaogopa kuukata ule mti akijua ndio mafanikio yake yapo pale.  

Au wakati mwingine mtu anaota, ametenda dhambi na amejaribu kumwomba Mungu, na Mungu hataki kumsamehe, na anapoamka asubuhi anashawishika kuamini kuwa Mungu hataki kumsamehe na anamchukia.   Au ndoto nyingine mtu anaota amekufa baada ya kujaribu kuwa mkristo au kumpa Kristo maisha yake. N,k…

Sasa ndoto zote kama hizi zinatoka kwa yule mwovu kwasababu zina maudhui ya kumlazimisha mtu asilitii Neno la Mungu au aende kinyume na maagizo ya Mungu, zinampeleka mtu katika kutenda dhambi zaidi kuliko kumfanya kuwa mtakatifu, nyingine zinamfanya mtu awe mwoga zaidi na kumchukia Mungu kuliko kumpenda! N.k  

Namna ya kuzidhibiti hizi ndoto ni kuamua kuishi maisha masafi yampendezayo Mungu na kujifunza kwa kina Neno la Mungu ili shetani anapoleta mawimbi yake kama bahari uwe na uwezo wa kuyadhibiti, Kadhalika na kudumu katika maombi. kwamfano mtu anayeoota kafanya kosa na hasamehewi, hiyo ni mishale ya shetani kutaka kukuvunja moyo usitake kuendelea kumtafuta Mungu, kwahiyo kama Neno halipo ndani yako linalosema

“1Yohana 1: 9 “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. ” hutaweza kumshinda shetani.  

Au ndoto inapokuja umegombana na mke wako na umeachana naye na kupata mwingine bora kuliko huyo, utajua imetoka kwa yule mwovu kwasababu Neno la Mungu limekaa ndani yako linalosema

“Luka 16:18 Kila amwachaye mkewe na kumwoa mke mwingine azini; naye amwoaye yeye aliyeachwa na mumewe azini. ”

Hivyo unajua ni ndoto iliyotoka kwa yule mwovu kukutaka wewe kutoka nje ya kusudi la Mungu na kutenda dhambi.   Au unapoota umebeti na umekuwa tajiri ghafla, utajua kabisa ni ndoto kutoka kwa yule mwovu kwasababu Neno la Mungu limekaa ndani yako linalosema “11 Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka; Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa. (Mithali 13:11)” Kwahiyo utajua ni yule mwovu anataka kukupeleka kwenye kazi iliyolaaniwa.  

Kadhalika na ndoto nyingine zote zinazofanana na hizo utazipima kwa Neno la Mungu tu! na utaweza kuzishinda na kuzifahamu kama Neno la Mungu linakaa ndani yako. Na pia kusali kabla ya kulala ni muhimu sana..Hiyo itasaidia kufunga mipenyo yote ya yule mwovu anayoweza kuitumia kukujaribu katika ndoto.  

3)Aina ya tatu ya ndoto ni ndoto zinazotoka kwa Mungu. Hizi ni zile zinazomjia mtu kutoka kwa Mungu kwa maudhui ya kumwonya mtu au kumuimarisha katika imani, na hizi haziwi kwa wingi kama zile zinazotokana na shughuli nyingi. Mfano wa ndoto hizi ni pale mtu anapoota kakutana na mtu/muhubiri kamshuhudia na kumwonya juu ya maisha yake maovu na anapoamka asubuhi anajikuta anahukumiwa na maisha ya dhambi anayoishi na kushawishika kutubu. Na mfano mwingine wa hizi ndoto ni pale mtu anaota unyakuo umepita na kaachwa, na anapoamka asubuhi anashawishika kujikagua maisha yake, nyingine mtu anaota kafa na kaenda kuzimu na anapoamka asubuhi anagundua ilikuwa ni ndoto tu.  

Nyingine ni zile mtu anaota kafanyiwa jambo baya sana la kumuumiza, na anapaamka asubuhi anajikuta yeye ndiye kamtendea mtu hilo jambo, hivyo anashawishika kujirekebisha na kutubu,   Nyingine unakuta mtu anaota kabeti, au kaenda kwa waganga, au kufanya uasherati, au kaiba, au kamtukana mtu, au kachukua mke au mume wa mtu, au kamsengenya mtu, au kaua na baada ya kufanya hivyo mambo yake yote yakaharibika, akajikuta kafilisika, au kafungwa, au kahukumiwa kufa, na anapoamka asubuhi anashawishika kutokufanya moja wapo ya mambo hayo ili yasimpate hayo mabaya. Hizo ni ndoto kutoka kwa Mungu, zinalenga kumuonya mtu   Na nyingine unakuta mtu anaota yupo shuleni anasoma, na kumbe alishamaliza muda mrefu sana, na anajiona anapambana kusoma na bado anafeli, ndoto ya namna hii unajua kabisa ni kutoka kwa Mungu kwasababu inayokuonyesha aina ya maisha unayoishi kwamba mwendo wako ni wa taratibu katika kumtafuta Mungu na bado upo nyuma ya wakati.  

Kwahiyo kwa ufupi ndoto zote zinazotokana na Mungu utazijua pia kama Neno la Mungu linalo kaa ndani yako, ndoto yoyote inayokupeleka kumtafuta Mungu zaidi, kutubu, au kukuonya tabia uliyonayo ambayo sio nzuri unajua kabisa ndoto hiyo inatoka kwa Mungu , au uichukie imani au ujitenge na kweli basi hiyo utajua moja kwa moja ni ya shetani.  

Ayubu 33:14 Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali.

15 Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani;

16 Ndipo huyafunua masikio ya watu, Na kuyatia muhuri mafundisho yao,

17 Ili amwondoe mtu katika makusudio yake, Na kumfichia mtu kiburi;

18 Yeye huizuia nafsi yake isiende shimoni, Na uhai wake usiangamie kwa upanga.

19 Yeye hutiwa adabu kwa maumivu kitandani mwake, Na kwa mashindano yaendeleayo daima mifupani mwake;

Ubarikiwe sana.

 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp


Mada Nyinginezo:

TOFAUTI KATI YA NDOTO NA MAONO NI IPI?

NJONI, NUNUENI MLE NA MNYWE.

TULICHUNGUZE UMBO LA YESU NA MWENENDO WAKE.

MADHARA YA KUTAFUTA ISHARA.

NGUVU YA HEKIMA NA AKILI.

WANA WA MAJOKA.

UBATILI.


 

Rudi Nyumbani:

WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/09/03/nitajuaje-kama-ndoto-ni-ya-mungu-au-ya-shetani/