NJIA SAHIHI YA KUFUNGA.

by Admin | 28 September 2019 08:46 pm09

Jina la Bwana YESU litukuzwe daima. Karibu tujifunze Neno la Mungu, leo kwa neema za Bwana tutajifunza juu ya njia sahihi ya kufunga.

Zipo aina nyingi za kufunga lakini kwa vyovyote vile, hatufungi ili Mungu atusikie au atujibu maombi yetu, Mungu hasubiri kwanza tuteseke ndio atusikie hapana kwani alishaweka wazi katika Neno lake, kuwa yeye anajua tunachohitaji kabla hata hatujamwomba (Mathayo 6:8)…Lakini pamoja na hayo Kufunga kunasaidia kuongeza uwezekano wa wewe kupata majibu ya maombi yako au kupata unachokitafuta kwa haraka tofuati na yule asiyefunga. Ni sawa tu na mwanafunzi anayesomea maktaba na Yule anayesomea nyumbani, anayesomea maktaba anaongeza uwezekano mkubwa wa kufaulu mitihani kuliko Yule anayesomea nyumbani, kwasababu kule maktaba kunakuwa na utulivu mkubwa na mazingira mazuri ya kujisomea kuliko nyumbani..Lakini hiyo haimfanyi afaulu mtihani moja kwa moja Yule wa nyumbani anaweza kufanya vizuri kushinda hata yeye..Lakini itampasa awe mtu wa kujitambua sana.

Vivyo hivyo na katika kufunga, Mtu mwenye desturi ya kuomba kwa kufunga anajijengea daraja zuri la yeye kuwasiliana na Mungu kuliko Yule apelekaye dua zake kwa Mungu bila kufunga, Kwasababu Kufunga kunampa utulivu Fulani wa Roho tofauti na mtu asiyefunga.

Na hiyo yote ni Kutokana na kutokuwa na Mungu katika mwili, au kutokumwona Mungu katika mwili ndio maana inatupelekea tumtafute Mungu kwa umakini zaidi kuliko kama tungekuwa tunamwona kwa macho…Mitume walipokuwa na Bwana duniani hakukuwa na sababu ya kufunga, ufunge ya nini wakati unayemtafuta upo naye hapo? Mpaka watu wengine wakashangaa inakuwaje hawa ni mitume wa Bwana lakini hawafungi, Ndipo Bwana alikawaambia wanachokifanya hawajakosea kwasababu mimi nipo, Siku zitakuja nitakapoondoka ndipo watakapofunga kama wengine…

Marko 2:18 “Nao wanafunzi wake Yohana na Mafarisayo walikuwa wakifunga; basi walikuja, wakamwambia, Kwani wanafunzi wa Yohana na wanafunzi wa Mafarisayo hufunga, bali wanafunzi wako hawafungi?

19 Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kufunga maadamu bwana-arusi yupo pamoja nao? Muda wote walipo na bwana-arusi pamoja nao hawawezi kufunga.

20 Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana-arusi, ndipo watakapofunga siku ile.”

Hivyo kitendo cha kufunga hakikwepeki sasa kwa mkristo yeyote. Na zipo aina nyingi za kufunga, lakini aina iliyozoeleka ni ile ya kuacha kula chakula. Lakini mfungo huu unafanywa kimakosa na wengi kwasababu ya kutokufahamu ni kwanini mtu anaacha kula..Na ndio hapo mtu mmoja atafunga vizuri kweli hata wiki tatu au mwezi au siku arobaini, lakini anafanya kama desturi za dini nyingine wanavyofanya, ukiangalia huku nyuma utamwona anaendelea na maisha yake ya kidunia anadhani kusikia kule njaa ndo Mungu anampa thawabu,. Hajui kuwa Mungu hamjibu mtu kwa mateso,(Maombolezo 3:31-35) sasa hapo mtu wa namna hiyo kaamua tu kujitesa bure..Hakuna chochote atakachokipata kutoka kwa Mungu.

Au unakuta mwingine anafunga kwa lengo la kumuomba Mungu mambo ambayo sio sawa na mapenzi yake, mwingine atamwomba Mungu ampe mali, lakini ndani ya moyo wake anawaza aitumie kwa anasa, mwingine atamwomba Mungu ampe hiki au kile, lakini nia yake moyoni ni kutumia kwa mambo maovu.. mtu wa namna hiyo pia asitazamie kupata kitu.

Isaya 58:3 “Husema, Mbona tumefunga, lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu, lakini huangalii? Fahamuni, siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu.

4 Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana, na kupiga kwa ngumi ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata kuisikizisha sauti yenu juu.

5 Je! Kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! Ni siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na Bwana?

6 Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira?

7 Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe?

8 Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde.

9 Ndipo utaita, na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu;

10 na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri.”

Unaona? Dhumuni la msingi kabisa la kujizuia kutokula mtu anapaswa afahamu ni kuyaleta mapenzi ya mwili chini na kuruhusu mapenzi ya Mungu yaje juu, ile njaa inakukumbusha kwenda mbele za Mungu kwa unyenyekevu mwingi , sikuzote mtu mwenye njaa anakuwa katika uhitaji sana kuliko mtu aliye shiba, hivyo mtu wa namna hiyo anapokwenda mbele za Mungu kumaanisha kwake kunakuwa kwa kiwango cha juu zaidi kuliko mtu aliyeridhika, hata maombi yake yanakuwa marefu sana, jaribu hata kwako utaligundua hilo..Na hiyo ndio faida kubwa ya kutokula wakati wa maombi. Hivyo inapelekea maombi yako kuwa na nguvu zaidi mbele za kuliko wengine.

Vile vile kuna kufunga ambako sio kwa kula, bali kwa kujizuia na mambo mengine yanayoweza kukusonga usiisikie sauti ya Mungu. Kufunga kwa namna hii kumekuwa kwa kawaida kwa watumishi wengi wa Mungu, Nabii Elisha ilimpasa atumie muda mwingi kujitenga na mazingira ya watu ili kudumisha joto la uhusiano wake na Mungu. Sio kwamba kuna shida kujihusisha na mambo ya kawaida ya kila siku, hapana lakini ni utaratibu wa Mungu kuzungumza katika sauti ya utulivu, na kama ni sauti ya utulivu hivyo naye huwa anahitaji mazingira tulivu ya kumwelewa.

Ufunuo wowote Mungu anaompa mwanadamu, hampi akiwa katika mazingira ya usumbufu wa akili, Usijidanganye kuwa Mungu atakupa ufunuo wowote katika hali ya masumbufu, kama utaisoma biblia na huku unasikiliza miziki ya kidunia, au huku una chat, au huku unafanya mambo mengine, Ni heri uifunge uje usome baadaye usiku peke yako…. inahitaji utulivu wa fikra na mawazo..Na hapo ndipo inakupasa ufunge baadhi ya vitu unavyovifanya, au ulivyozoea kuvifanya..Na kwa jinsi unavyovifunga kwa muda mrefu zaidi ndivyo unavyoongezeka uwezekano wa Mungu kusema na wewe kwa haraka na kwa mara nyingi zaidi.

Kufunga ni kuna faida kwasababu yeye mwenyewe anasema wote wafanyao hivyo huwapa thawabu kama hawatafanya kinafki na kwa nia mbaya..(Mathayo 6:16)

Ni ahadi yake kukulipa, Funga tu kwa kumaanisha kumsogelea Mungu zaidi, utapata zaidi ya kile ulichomwomba. Kuna mtu aliuliza swali je! Maandiko yanasema tunapaswa tufunge kuanzia saa ngapi hadi saa ngapi na ni kwa siku ngapi?..Jibu ni kuwa Biblia haijatoa masharti yoyote juu ya muda wa kufunga au siku za kufunga..Imezoeleka siku 3, siku 21 na siku 40 kwasababu ndio siku ambazo zimeonekana zikifungwa na wengi..Lakini hiyo haimaanishi kuwa nawe ufunge muda huo, ni vile Roho atakavyokuongoza na kulingana na aina ya dua uipelekayo kwa Mungu, unaweza ukafunga, siku moja, au wiki, au mwezi, au mwaka, na Mungu akaridhia, vile vile unaweza ukafunga saa 6 kwa siku, saa 12, au siku tatu bila kula, au siku 40 bila kula , ni vile tu Mungu atakavyokupa neema..Lakini vyovyote vile kufunga ni muhimu kwa kila mkristo. Na kuna manufaa na thawabu nyingi.

Ubarikiwe sana. Tafadhali “Share” Ujumbe huu kwa wengine. Na Bwana atakubariki.


Mada Nyinginezo:

FAIDA ZA MAOMBI YA USIKU

KAZI YA UZURURAJI WA SHETANI.

RUDIA, TENA NA TENA KUMWOMBA MUNGU USIKATE TAMAA.

NINI MAANA YA MSIMWITE MTU BABA DUNIANI?

KAINI ALIPATIA WAPI MKE?


Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/09/28/njia-sahihi-ya-kufunga-2/