by Admin | 4 October 2019 08:46 pm10
Napendelea kabla mtu hajakimbilia kutafuta tafsiri ya ndoto yake, ni vizuri kwanza apate elimu juu ya aina za ndoto, hiyo itamsaidia kujua ndoto yake inaangukia katika kundi la aina gani, hivyo atapata wepesi wa kuweza yeye mwenyewe kuzitafsiri ndoto pasipo hata kutegemea msaada wa mtu mwingine.
Ikiwa utapenda kujua aina hizi za ndoto bofya hapa >> NITAJUAJE KAMA NDOTO NI YA MUNGU AU YA SHETANI? ukishamaliza kusoma kisha tuendelee…
Sasa kama ndoto yako sio ile inayotokana na shughuli za kila siku au mazingira yanayokuzunguka na unaiota mara kwa mara, basi fahamu kuwa kuna jambo Mungu anazungumza na wewe hapo zingatia sana..Biblia inasema..
Ayubu 33:14 “Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali.
15 Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani;
16 Ndipo huyafunua masikio ya watu, Na kuyatia muhuri mafundisho yao,”
Mungu anakukumbusha kuwa upo safarini hapa duniani, kwamba kila jambo unalolifanya ukumbuke kuwa upo safarini hakuna na chochote utashikamana nacho hapa duniani milele,..
Na kama tunavyojua safarini, hata mkishuka kupumzika pengine kula au kujisaidia basi ni dakika chache tu 10 au 15 basi safari inaendelea, hakuna muda wa kuzurura zurura au kuanza kujihangaisha na mambo ya hapo mlipokuwa mnapita, utakuwa ni mjinga kama utawaza kuwekeza eneo hilo, au kwenda kufanya shughuli hapo, gari litaondoka na kukuacha, na mwisho wa siku kule ulipokuwa unatazamia kwenda hutafika..
Hivyo Mungu kukuonyesha hivyo ni kukuonya usiangalie sana mambo ya ulimwengu huu yanayopita bali angalia vya kule mbele vinavyodumu na ukumbuke kuwa upo safarini, inamaanisha kuwa kwa namna moja au nyingine ulishawahi kuyatazama mambo ya kule, ishi kama maisha ya mpitaji, kwasababu watu wote wa Mungu ndivyo wanavyoishi..
Isaya 35:8 “Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio, wajapokuwa wajinga, hawatapotea katika njia hiyo.”
Hivyo angalia ni vitu gani vinavyokusonga katika maisha yako, Je! Ni shughuli za ulimwengu huu mpaka hauna muda na Mungu? Je! Ni tamaa ya mambo ya ulimwenguni huu, Je ni anasa? Biblia inasema:
1Petro 2:11 “Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho.
12 Mwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa.”
Hivyo Fahamu kuwa Mungu anakupenda na ndio maana amekuonyesha ndoto za namna hiyo, basi usipuuzie sauti yake, anza sasa kumtazama YESU ikiwa bado upo mbali naye, Unachopaswa kufanya ni kutubu sasa mkabidhi yeye maisha yako upya, nenda kabatizwe kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako, kisha yeye mwenyewe atakupa kipawa cha Roho Mtakatifu…nawe utakuwa na uhakika wa kuwa salama katika safari yako fupi iliyobakia hapa duniani… Aidha kama utakuwa upo tayari ndani ya Kristo na unajihisi huna kando lolote basi fahamu kuwa Mungu anataka uzidi kuiangalia safari yako zaidi kuliko kitu kingine chochote, kwasababu ipo thawabu kubwa amekuandalia mbele.
Ubarikiwe.
Kwa mgawanyo bora wa masomo download App hapa>> App wingu la mashahidi
Mada Nyinginezo:
NJIA KUU YA KUINGIA KATIKA ULE MJI.
NINI MAANA YA KUISHI KWA KUUKOMBOA WAKATI?.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/10/04/kuota-unasafiri/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.