JINSI YA KUJIWEKA KARIBU NA MUNGU.

by Admin | 27 November 2019 08:46 pm11

JINSI YA KUJIWEKA KARIBU NA MUNGU.

Hakuna kitu kinachomtamaisha Mungu kama kujiweka karibu na sisi, tunalithitisha hilo katika maandiko haya “Yakobo 4:5 Au mwadhani ya kwamba maandiko yasema bure? Huyo Roho akaaye ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu?” Unaona? lakini kwa bahati mbaya sisi ndio hatujui kanuni ya jinsi ya kujiweka karibu na Mungu..Na ndio maana tukiendelea mbele kidogo maandiko yanasema:..

Yakobo 4:8 Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi…

Unaona biblia inatupa ufahamu mwepesi wa  namna ya sisi kuwa karibu na Mungu, nao ni kwa kumkaribia tu.. Watu wengi wanadhani wanaweza kuwa karibu na Mungu, au Mungu kuwa rafiki yao wa karibu wakiwa katika hali zao zile zile za kale, na mienendo ile ile wanayoiendea kila siku, na huku hawataki kuonyesha jitihada za kumkaribia Mungu, ndio hapo mwisho wa siku wanaona kama vile Mungu hana faida yoyote maishani mwao, au wanaona kama vile amekufa hayupo, au hawasikii, au hawajali…yote hiyo ni kwasababu hawajajua namna ya kumkaribia Mungu..

SASA TUNAWEZAJE KUMKARIBIA MUNGU?

Tukiendelea kusoma ule ule mstari unasema…

Yakobo 4:8 “Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili.

9 Huzunikeni na kuomboleza na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu.

10 Jidhilini mbele za Bwana, naye atawakuza”.

Unaona anatoa kanuni kadha wa kadha  hapo ya kwanza na ya msingi ni:

ITAKASENI MIKONO YENU, ENYI WENYE DHAMBI:

Ukiwa mwenye dhambi, yaani kwa ufupi ukiwa hujaokoka, kamwe hutakaa umkaribie Mungu kwa namna yoyote ile, haijalishi, unatoa zaka kiasi gani, haijalishi unasaidia yatima kiasi gani, haijalishi, unahudhuria ibadani kiasi, maadamu upo nje ya Kristo, tayari wewe upo mbali sana na Mungu. Hivyo hatua ya kwanza na ya msingi ya Mungu kukuribia ni kutubu kwa kudhamiria kabisa kuacha dhambi zako zote, kumwambia Bwana Yesu akusamehe dhambi zote ulizomkosea, kisha kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi Kwa jina la Yesu Kristo sawasawa na Matendo 2:38, kisha kupokea  Roho Mtakatifu. Kwa kufanya hivyo utakuwa umeshakamilisha hatua ya kwanza ya kumkaribia Mungu..

JAMBO LA PILI ANASEMA NI : KUISAFISHA MIOYO YENU, ENYI WENYE NIA MBILI:

Wapo watu baada ya kumpa Kristo maisha yao, bado wanayatamani mambo yale yale waliyoyaacha kule nyuma, sasa watu kama hao Mungu hawezi kuwakaribia kwasababu mioyo yao inakuwa imegawanyika, nusu kwa Mungu, nusu kwenye dunia..Ikiwa umedhamiria kweli kumfuata Kristo mfuate kwa kumaanisha kweli kweli, acha kila kitu mfuate, na hiyo inakuja kwa kujikana nafsi yako na kujitwika msalaba wako na kumfuata, unakuwa tayari kukubali kuchekwa, au kudharauliwa, au kutukanwa au kufanyiwa jambo lolote baya kwa ajili ya imani yako bila kutetereka..Na Mungu akishaona moyo wako upo thabiti kwake, hapo ndipo na yeye anaongeza hatua yake nyingine ya kukukaribia.

YA TATU NI: HUZUNIKENI NA KUOMBOLEZA NA KULIA:

Tena anaendelea kusema.. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu…Hii haimaanishi kuwa ujifanye kuwa mtu wa huzuni kila saa, kama vile mfiwa hapana, bali unaugua kwa kuchukia dhambi, unaomboleza kwa mabaya yanayofanyika, sio unafurahia kuona ubaya, au dhambi zikifanyika, Na kwa kawaida kuugua pamoja na maombolezo kunazaa pia na kuombea wengine, na kuliombea kanisa lote kwa ujumla..na kuwashuhudia wengine habari njema..Sio pale tunapokuwa wakristo ndio basi tena, maadamu sisi tumeshaokolewa hayo mengine hayatuhusu…Tukiwa watu wa namna hiyo basi vilevile tufahamu kuwa Mungu naye atakuwa mbali na sisi lakini kama tukiwa tunahuzunika na kuomboleza kwa ajili yetu sisi na kwa wengine ili waokolewe, na kuchukua hatua stahiki basi tufahamu kuwa Mungu hapo atakuwa tena karibu zaidi na sisi, kwasababu tunaichukua ile huzuni yake tunaifanya ya kwetu..Mungu hafurahii maovu, wala hapendi mtu hata mmoja apotee.

NA MWISHO NI: JIDHILINI MBELE ZA BWANA.

 Kwa namna ya kawaida hakuna mtu asiyempenda mtu mnyenyekevu, Vivyo hivyo na kwa Mungu tukiwa watu wanyenyekevu watu wa kujishusha mbele zake, watu tunaoungama makosa yetu, basi tutamvuta kwa haraka sana aje karibu sana na sisi kama ilivyokuwa kwa Daudi..Lakini tukijiona sisi kila kitu tunajua, hatutaki kuambiwa chochote, hata kama ni kweli, tunajiona tunajua biblia sana, dini zetu na madhehebu yetu yanatutosheleza kama vile mafarisayo na waandishi walivyokuwa, kwa kiburi chao walimkosa Mungu, walidhani wapo karibu na YEHOVA kumbe walikuwa hatua mia mbali na yeye.

FAIDA ZA KUWA KARIBU NA MUNGU NI ZIPI?

Faida kubwa ni kuambukizwa ule utukufu wake, kama tu vile pale unapokaa  karibu na mtu aliyejipulizia marashi makali kwa muda mrefu akiondoka ile harufu bado itabakia katika mwili wako..Vivyo hivyo na kwa Mungu ikiwa umezifuata hizo hatua zote basi ule utukufu wa Mungu unaingia ndani yako, kama vile Musa alivyokaa uweponi mwa Mungu kwa siku zile 40 kule mlimani, aliposhuka uso wake uling’aa kama vile wa malaika..Ni kwasababu alikuwa karibu sana na Mungu…Lakini sisi hatung’ai uso wa mwilini bali uso wa rohoni..

Matokeo yake ni kuwa jambo lolote tutakalomwomba Mungu tutatendewa…

Yohana 15:7 Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa.

Vilevile wewe utakuwa ni wa kwanza kuzipokea zile siri za ndani kabisa za Mungu, kwasababu wewe ni bibi-arusi wa Kristo, na sikuzote bibia-arusi ndiye anayejua siri ya Bwana arusi, halikadhalika hakuna jambo lolote au adui yoyote atakayekushida kwasababu muda wote unaonekana kama miale ya moto duniani..Vilevile Mungu anakufanya kuwa chombo chake kiteule cha kuwachunga kondoo wake wengine.

Hizo ndio faida zake kuu. Kwanini tusitamani kuwa karibu naye? Tufanye bidii sote tufike hapo. Amen.

Ubarikiwe sana.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

KWANINI DAUDI ALIKUWA NI MTU ALIYEUPENDEZA MOYO WA MUNGU?

NITAFUNGUAJE MILANGO ILIYOFUNGWA MBELE YANGU?

ALIYE MKUU KATIKA UFALME WA MBINGUNI.

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/11/27/jinsi-ya-kujiweka-karibu-na-mungu/