KIJITO CHA UTAKASO.

by Admin | 5 December 2019 08:46 pm12

Kijito cha Utakaso, Ni kijito cha  Damu ya Yesu, kidhihirishwacho kwa ubatizo wa maji mengi..Kama vile Maji ya farakano yalivyotumika katika Agano la kale kutakasa, katika Agano jipya yanatumika maji ya ubatizo.

Katika Agano la Kale, ilikuwa hata kugusa tu maiti, mtu tayari ameingia Unajisi, hivyo ilimpasa akafanye utakaso kwanza kabla ya kuingia katika kusanyiko la Bwana..

Hesabu 19:11 “Mtu agusaye maiti ye yote atakuwa najisi muda wa siku saba;

12 naye atajitakasa kwa yale maji siku ya tatu, na siku ya saba atakuwa safi; lakini kama hajitakasi siku ya tatu, ndipo na siku ya saba hatakuwa safi.

13 Mtu awaye yote agusaye maiti wa mtu aliyekufa, asijitakase, yuatia unajisi maskani ya Bwana; na mtu huyo atakatiliwa mbali na Israeli; maana, hayo maji ya farakano hayakunyunyizwa juu yake, atakuwa najisi; unajisi wake ukali juu yake bado”.

Na kulikuwa pia na sheria kali  kwa mtu ambaye atakataa kujitakasa kwa kujiosha katika mji yaliyoamriwa. Ambayo ni maji ya farakano (Au maji ya Utakaso kwa jina lingine).

Tunasoma hayo katika..

Hesabu 19:20 “Lakini mtu atakayekuwa najisi, naye hataki kujitakasa, mtu huyo atakatiliwa mbali katika mkutano, kwa sababu amepatia unajisi mahali patakatifu pa Bwana; hayo maji ya farakano hayakunyunyizwa juu yake; yeye yu najisi”. 

Katika Agano jipya, watu wote ambao hawajampa Yesu Kristo maisha yao, au kwa lugha rahisi HAWAJAOKOKA!..Hao ni watu najisi mbele za Mungu…Hivyo hawastahili hata kumwabudu Mungu katika hali walizopo, hawastahili hata kumsogelea Mungu wala kuuliza  kitu chochote kutoka kwake..Watu wengi sana hawalijui hilo…

Soma..

Ezekieli 14:3 “Mwanadamu, watu hawa wametwaa vinyago vyao na kuvitia mioyoni mwao, nao wameweka kwazo la uovu wao mbele ya nyuso zao. Je! Ni laiki yangu niulizwe na wao katika neno lo lote?

4 Basi sema nao, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Kila mtu wa nyumba ya Israeli atwaaye vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake, na kumwendea nabii; mimi, Bwana, nitamjibu neno lake sawasawa na wingi wa sanamu zake”

Na wala hawawezi kumwomba Mungu wala kumtolea sadaka..kwasababu ni Najisi…

kumbu.23:18 “Usilete ujira wa kahaba, wala mshahara wa mbwa, katika nyumba ya Bwana, Mungu wako, kwa ajili ya nadhiri yo yote; kwani haya ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako, yote mawili”

Ni kitu gani kinachowafanya wawe Najisi?

Jibu Ni dhambi zilizomo ndani yao ndizo zimewafanya wawe NAJISI, machoni pa Mungu…Biblia inasema katika..

Marko 7:21 “Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati,

22 wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu.

23 Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi”

Unaona?..Dhambi ndizo zinazomtia mtu unajisi mbele za Mungu..Na Watu najisi hawawezi kumsogelea Mungu hata kidogo..Na watu najisi ni watu wote watendao dhambi, (yaani ambao hawajaokoka)...watu wote wenye chuki, wasengenyaji, waasherati, wezi, wavaaji vimini, suruali, nguo fupi na zilizo nusu uchu, wote wajipakao wanja, lipstick, na kuvaa wigi n.k...Mungu huwa anajificha uso wao wasimwone, maombi yao yanakuwa hayajibiwi…Kwakuwa ni Najisi mbele za Mungu.

Biblia inasema…

Isaya 59:1″ Tazama, mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia;

2 lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.

3 Kwa maana mikono yenu imetiwa unajisi kwa damu, na vidole vyenu vimetiwa unajisi kwa uovu; midomo yenu imenena uongo, ndimi zenu zimenong’ona ubaya”

Sasa watu wa Agano la kale walitakasika kwa kuoshwa kwenye maji…Lakini sisi watu wa Agano jipya wanatakasika kwa kuoshwa kwenye kijito cha Damu ya YESU. Kijulikanacho kama KIJITO CHA UTAKASO.

Katika kijito hicho cha utakaso, Mtu atazama na kuoshwa katika hicho na unajisi wake wote unaondoka..

Sasa Mtu anaoshwaje ndani ya hicho kijito cha utakaso?

Kwanza kwa kutubu: kutubu maana yake ni kukiri kwamba ulikuwa mkosaji na hivyo umeamua kugeuka na kuacha kufanya uliyokuwa unayafanya…Hicho kinafananishwa na kitendo cha kuvua nguo zako zote kabla ya kuingia kuoga  kwenye kijito chochote kile.

Pili: Unajitosa kwenye kijito cha Utakaso..Kijito hicho ni Ubatizo wa Maji mengi ..Yaani baada tu ya kutubu, hatua inayofuata ni kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi… Kumbuka ubatizo sahihi sio wa kunyunyiziwa maji, au sio wa utotoni wala sio wa Baba, mwana na Roho Mtakatifu..Ubatizo sahihi ni wa kuzamishwa mwili wote katika maji mengi sawasawa na Yohana 3:23.. na katika jina la YESU KRISTO sawasawa na (Matendo 2:38).

Kwa kuzama katika kijito hicho..Kwa nje utaonekana kama umezama kwenye maji ya ubatizo lakini katika Roho utaonekana umezama katika kijito cha damu ya YESU.. Kuzamishwa mwili wote katika maji mengi ni ishara inayoonesha umezamishwa roho yako katika kijito cha damu ya Yesu kiletacho utakaso…Na hivyo dhambi zako zote zitakuwa zimeondolewa kwa tendo hilo..Na hautahesabika kuwa najisi tena mbele za Mungu.

Matendo 2:38 “Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu”

Je umeoshwa leo dhambi zako zote?..

Je unastahili kumsogelea Mungu? au je wewe ni najisi?..Kama bado hujachovya kwenye hicho kijito cha utakaso  unasubiri nini?..Tubu leo mwambie Bwana Yesu  leo nakuja mbele zako, mimi ni mkosaji, naghairi mabaya yangu yote leo,..Naomba unisamehe dhambi zangu zote…..Nakuomba unipokee sawasawa na Neno lako lisemalo kwamba “wote wajao kwako hutawatupa nje kamwe”..Nakuomba unipe neema ya kukujua wewe siku zote za maisha yangu. Amen.

Ukiwa umeomba hivyo au hata zaidi ya hivyo..Basi fahamu ya kuwa Mungu si mwongo..Ameshakusamehe haijalishi dhambi zako zilikuwa ni nyingi kiasi gani..

Sasa hatua inayofuata ni ya MUHIMU SANA. Nenda katafute Ubatizo sahihi kwa hali na mali..Umejifunza hapo juu, maana ya kijito cha Utakaso..Kitafute hicho kwa hali na mali…Kama unafahamu mahali unaweza kupata huduma hiyo ya ubatizo fanya hivyo haraka, maana shetani hapendi kuona unakwenda mbinguni…Na kama hufahamu basi unaweza kuwasiliana nasi kwa namba hizi +255789001312 tutakuelekeza mahali karibu ni ulipo..ambapo unaweza kupata huduma hiyo.

Bwana akubariki sana..

Kumbuka Biblia inasema katika..1Wathesalonike 4:7 “Maana Mungu hakutuitia uchafu, bali tuwe katika utakaso”.

Na tena Inasema…

Waebrania 10:10 “Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu”.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Maran atha!


Mada Nyinginezo:

JE! UMEBATIZWA UBATIZO SAHIHI?

ROHO HUTUOMBEA KWA KUUGUA KUSIKOWEZA KUTAMKWA!

Nini maana ya kusali kwa kupayuka payuka?

UWE MWAMINIFU HATA KUFA.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/12/05/kijito-cha-utakaso/