by Admin | 24 December 2019 08:46 pm12
Njia za Mungu hazichunguziki, Mariamu akutana na Elisabeti..Elisabeti katika uzee wake aliambiwa atapata mimba, wakati ambao kizazi kimeshanyauka. Je! Ni nini tunaweza kujifunza hapo?.
Nakusalimu katika jina kuu la Emanueli, Bwana wetu YESU KRISTO.
Wakati tukiwa katika kipindi hichi cha Krisimasi na kufunga mwaka. Napenda tufunge kwa kuwatazama wanawake hawa wawili Mariamu na Elisabeti. Wanawake hawa wanawakilisha makundi mawili ya Watoto wa Mungu ambao wapo tayari kupokea baraka zao hivi karibuni.
Kama tunavyojua walikuwa ni wanawake waliokuwa wanamcha Mungu, mmoja alikuwa ni mzee sana, na mwingine alikuwa bado ni kijana mdogo. Lakini cha ajabu ni kuwa kila mmoja alipokea ripoti ambayo ilikuwa ni kinyume na matarajio yake.
Elisabeti katika uzee wake aliambiwa atapata mimba, wakati ambao kizazi kimeshanyauka, na mayai ya uzazi hayapo, wakati ambapo mawazo ya kuwa na mtoto kichwani yameshafutika, Anachosubiri ni kifo tu, lakini ghafla anapokea ripoti kutoka kwa malaika Gabrieli kuwa atazaa mtoto mwanamume, na sio tu mtoto ilimradi mtoto bali mtoto ambaye atakuwa mkuu sana Luka 1:15).
Tukirudi upande wa pili wa Mariamu, yeye naya akiwa bado binti mdogo tu, ndio kwanza amechumbiwa..Akiwa bado hata hajamkaribia mwanamume, hata mawazo ya kuwa na mtoto hayajaingia kichwani mwake. Lakini tunaona hapa yeye naye anapokea ripoti ya ghafla kutoka kwa malaika yule yule Gabrieli kuwa atapata mimba. Naye atazaa mtoto, naye si mtoto ilimradi mtoto tu, bali atakuwa mfalme mkuu, ambaye ufalme wake utakuwa hauna mwisho.
Mariamu apolisikia hivyo hakukawia, alifunga safari kwenda kwa Elisabeti kuusikiliza ushuhuda wake, huku naye pia akiwa na ushuhuda wa kumweleza wa kwake.. shauku ilimjaa sana..
Jaribu kufikiria walipokutana walianza kuzungumza maneno gani..Mmoja atasema, nilidhani mpaka nitakapokutana na mwanamume ndio nitapata ujauzito, mwingine atasema, nilidhani wakati nilipokuwa na mwanamume, wakati ambao mayai yangu yakiwa tumboni ndio ningepata ujauzito..Lakini sasa wakati ambapo hatukutegemea hapo ndipo Mungu alipotuonekania..
Hata wewe leo ambaye umeokoka, unaweza ukajiona bado ni mchanga, bado ni mdogo Mungu kukutimizia malengo yako, unaweza ukadhani mpaka Bwana anitumie katika kazi yake ni lazima ufikie umri wa makamo, Au mpaka ufanikiwe ni lazima uwe umemaliza shule kwanza, au umefanya kazi miaka kadhaa, au umefikisha umri fulani.. Nataka nikuambie ondoa mawazo hayo kichwani kwako ikiwa wewe ni mtoto wa Mungu…
Njia za Mungu hazichunguziki, Mariamu hakuwahi kufikiria kuwa angewahi kubeba ujauzito kabla ya kukutana na mwanamume..Lakini iliwezekana kwasababu Gabrieli alimwambia hakuna linaloshindikana kwa Mungu..(Luka 1:37)
Vivyo hivyo na wewe. Neema hiyo Bwana anaweza akaishusha juu yako, ni nani ajuaye itakuwa katika huu mwaka unaonza 2020, atakuwa tayari ameshakupigisha hatua kubwa katika utumishi wako?, katika huduma yako?..ukawa msaada kwa wengi.. Kama ulikuwa nawe ni Tasa, Bwana akakupatia mtoto kama Elizabeth…Na Katika Maisha yako pia?, ukawa na nyumba yako mwenyewe, ukawa na biashara zako mwenyewe? Angali bado ni mdogo, angali hujasoma, angali bado hujaoa au hujaolewa? ..Lakini hiyo yote ni kama utakuwa katika mstari wa kutembea katika mapenzi ya Mungu..
Vilevile mwingine unaweza ukajiona, muda umeshakwenda sana, umri umesogea, ukiangalia kile ulichokuwa unakiongojea kwa muda mrefu hakijakufikia kwa wakati, mpaka sasa hujapiga hatua inayoonekana kwa macho, bado huna kwako, bado kula ni kwa shida..Ukiangalia hata useme ukaanze kutafuta bado utakuwa umechelewa, ni kama vile umeshajikatia tamaa kila kitu..Nataka nikuambie hata Elisabeti alidhani hivyo katika uzee wake, lakini wakati ulipofika wa yeye kupata mimba ya shujaa wa Imani aliyeitwa Yohana Mbatizaji ambaye Bwana Yesu alimshuhudia kuwa katika uzao wa wanawake hakuwahi kutokea aliye mkuu kama yeye, yaani kwa namna nyingine hata akina Musa, na Eliya na manabii wote hakuna hata mmoja aliyemzidi kwa ukuu Yohana Mbatizaji kule mbinguni..
Vivyo hivyo na wewe uliyeokoka ambaye kwa muda mrefu unaona kuna utasa katika huduma yako au biashara yako, au kazi yako..Ni nani ajuaye kipindi hichi ndicho Mungu anatungisha mimba hiyo ya mafanikio yako. Na mpaka mwaka kesho unaisha unakuwa umeyafikia malengo na kuvuka hata Zaidi ya matarajio yako?
Wagalatia 4:27 “Kwa maana imeandikwa, Furahi, wewe uliye tasa, usiyezaa; Paza sauti, ulie, wewe usiye na utungu; Maana watoto wake aliyeachwa pekee ni wengi Kuliko wa huyo aliye na mume”.
Lakini hiyo yote inakuja ikiwa upo katika mstari ulionyooka wa kuyatenda mapenzi ya Mungu kama alivyokuwa Elisabeti biblia inavyosema alikuwa mtu wa Haki, akienenda katika amri zote za Mungu bila lawama (Luka 1:6).
Lakini kama upo nje ya Kristo. Usitegemee miujiza ya Mungu kama hii kuja katika Maisha yako..Ni vizuri ndugu uumalize mwaka wako na Bwana, Ili ukifungua mwaka mpya, Bwana naye aanze na wewe.. Na akishaanzana na wewe, anaanzana na wewe kweli kweli Kama vile tulivyoona hapo juu, njia za Mungu hazichunguzi, unaweza kusema bado sana, kumbe ni wakati wenyewe..Unaweza kusema nimechelewa kumbe ndio wakati wa kufarijiwa
Unachopaswa kufanya ni kuyasalimisha Maisha yako kwa Bwana..Na hiyo inakuja kwa kutubu kwa kumaanisha kabisa kuacha dhambi zako zote bila kubakisha hata moja, kama ulikuwa ni mlevi leo hii unasema basi, kama ulikuwa ni mzinzi leo hii unasema inatosha, kama ulikuwa unaishi na mke au mume ambaye si wako leo hii unaaacha, kama ulikuwa unatapeli watu unasema sitaki tena mambo hayo nataka nianze mwaka wangu upya na Bwana..Na hutubu kwasababu unataka uwe na gari au nyumba..unatubu kwasababu umeona maisha yako yanamhitaji Yesu Kristo, na hayatoshi bila yeye.
Sasa ikiwa utakuwa umefanya hivyo kwa moyo wako wote, na umemaanisha kumgeukia Kristo kikweli kweli fahamu kuwa Mungu atauona moyo wako, na akishauona umegeuka basi yeye mwenyewe atakuwa ameshakusamehe na atakuwa na jukumu la kukuvuta kwake Zaidi kwa nguvu ya ajabu sana..Atakuvika uwezo wa kipekee wa kufanyika mwana wa Mungu ,(Yohana 1:12) Na uwezo huo ndio utakaokufanya uweze kuyashinda yale yaliyosalia yaliyokuwa magumu kuyashinda na kudumu katika wokovu.
Vilevile ukishafanya hivyo ili kuukamilisha wokovu wako, tafuta kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamwishwa katika maji mengi (Yohana 3:23) na kwa jina la YESU KRISTO sawasawa na Matendo 2:38, Na baada ya hapo Roho Mtakatifu atakuwa na wewe daima, Mpaka siku ya kufa kwako, ikiwa unyakuo utakuwa bado haujapita. Na baraka zote hizo ambazo Mungu anazileta nje ya matarajio yetu kwa Watoto wake wote wampendao zitaachiliwa na juu yako wewe uliyeokoka.
Bwana akubariki sana. Tafadhali “Share” na wengine ujumbe huu.
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Shalom.
Mada Nyinginezo:
Mungu anasema hatagharikisha dunia na maji tena,.Kwanini watu wanasema dunia itaangamizwa?
Sanduku la Agano lilikuwa linawakilisha nini katika Agano jipya?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/12/24/mariamu-akutana-na-elisabeti/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.