NGUVU YA MSAMAHA

by Admin | 17 January 2020 08:46 am01

Karibu tujifunze mambo yafuatayo; Nguvu ya msamaha ipo wapi? Biblia inaposema achilieni nanyi mtaachiliwa ina maana gani?Je kumpeleka mtu polisi au mahakamani ni kutokusamehe?

Neno Msamaha, halina tofauti sana na Neno ‘kuachilia’ au ‘kufungulia’. Unapomsamehe mtu aliyekukosea ni sawa na umemwachilia huru katika moyo wako. Huna naye deni tena, anakuwa anatoka katika kifungo cha moyo wako. Na kila mwanadamu anapaswa awe na huo uwezo wa kusamehe..Kwasababu msamaha ni ufunguo wa kitu kikubwa sana katika maisha.

Ingawa kwa akili za kawaida za kibinadamu ni ngumu kusamehe. Lakini ukiwa Mkristo(uliyeoshwa kwa damu ya Yesu Kristo na kufanyika kiumbe kipya) ni rahisi kusamehe. Na msamaha ule unaohusisha vitu ambavyo ni vigumu kusamehe huwa ndio unamaana kubwa sana na unafaida kubwa zaidi kuliko ule wa vitu vidogo.

Nguvu ya Msamaha upo katika Mistari ifuatayo.

Luka 6:36 ‘Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.

37 Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa.

38 Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa’

Hapo anasema ‘achilieni’….Faida za kuachilia ni nini?..mbele kidogo anasema ‘nanyi mtaachiliwa’. Ikiwa na maana kuwa unapomsamehe mtu na wewe umeweka deni mahali fulani la kusamehewa…kwa kipimo kile kile na uzito ule ule uliomsaheme mtu…Na wewe unalo deni la kusamehewa kwa kiwango hicho hicho mahali fulani..wakati fulani.

Wengi wetu hatujui au hatuna taarifa kuwa kuna Mungu juu anayeyatazama maisha..Ukishaikosa au kupungukiwa na hiyo Imani basi ni ngumu sana kuyaishi maneno ya Mungu. Siku zote kumbuka Mungu yupo juu anatutazama, kila tendo, kila neno na kila tukio tulifanyalo..na yeye hasahau, wala hasinzii, wala hapumziki..Kwahiyo kila kitu tukifanyacho kiwe kibaya kiwe kizuri anakirekodi na kila kitu kina mshahara wake..Vingine mishahara yao ni hapa hapa duniani na vingine ni kule katika ulimwengu ujao.

Ufunuo 22:12 ‘Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo’.

Kwahiyo kama ulitukanwa na hujasamehe…Na wewe pia hujasamehewa matusi ya siri uliyoyatoa moyoni mwako dhidi ya mwingine. Haijalishi unayakumbuka au huyakumbuki…mbele za Mungu hayajasahaulika hata moja.

Tusome tena mfano ufuatao wa mwisho.

Mathayo 18:21 ‘Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba?

22 Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.

23 Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake.

24 Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi.

25 Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile deni.

26 Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia.

27 Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni.

28 Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia akamkamata,akamshika koo,akisema Nilipe uwiwacho

29 Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia.

30 Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni.

31 Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka.

32 Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi;

33 nawe, je! Haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe?

34 Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote.

35 Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake’.

Umeona…Nguvu ya msamaha ipo kwenye vile unavyovisamehe…Unapomsamehe mtu 100 basi na wewe unastahili kusamehewa 100..Kadhalika unaposamehewa vitu 100 na wewe una deni la kusamehe vitu 100.

Hakunaga short-cut ya kupokea msamaha…bila kusamehe, hakikisha unasamehe kwanza ili na wewe pia usamehewe…Bwana Yesu alisema hivyo katika…

Mathayo 6:14 “Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi.

15 Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu”.

Sasa utauliza hata mtu akinidhulumu vitu vyangu vyote nimsamehe?…Ndio msamehe..hiyo ni kwa faida yako binafsi…Utakuwa umemwachia Mungu wako deni kubwa la yeye kukurehemu wewe sawasawa na jinsi ulivyomsamehe mwingine…Ukumbuke huo mfano hapo juu.

Sasa swali lingine linakuja…Je kumpeleka mtu polisi au mahakamani ni kutomsamehe?

Yapo mazingira ya mtu kupelekwa polisi au mahakamani…ambapo sio dhambi.

Kwamfano imetokea mwizi kakuibia na umemfahamu, na ulipojaribu kumwendea ukakuta kakificha kile kitu au kashakitumia na hataki kukiri kwamba yeye ni mwizi wala kutubu…Mtu kama huyo moyoni unamsamehe kabisa kwa moyo wote…lakni pia anapaswa akashtakiwe kwa watu wa karibu au polisi ili asiendeleze wizi huo kwako na kwa wengine. (Kwa kufanya hivyo Sio dhambi) na hautahesabika kama hujamsamehe mbele za Mungu.

Kadhalika kama umedhulumiwa mali yako isivyo halali na kuna nafasi ya kuirudisha, pambana kuirudisha kwa hekima…Mfuate aliyeichukua mwambie akurudishie akikataa na kuna nafasi ya kumshtaki..mshataki ili aogope akurudishie na ili siku nyingine asirudie kufanya hivyo kwako au kwa wengine…Lakini akija kwako na kutubu na kukiri kwamba ni kweli kakudhulumu lakini mali ile kashaitumia na hana tena..na anatubu mbele zako…hapo huna budi kumsamehe asilimia zote na kumkumbatia. Hupaswi kwenda kumshtaki, kwasababu kashakiri kosa lake. Unapaswa umsamehe kabisa. (Ukikumbuka siku zote kwamba nguvu ya msamaha ipo katika kusamehe).

Ukiwasamehe waliokuudhi, Bwana atakusamehe uliyomuudhi…Ukiwasamehe waliokudhulumu…Bwana atakusamehe dhuluma ulizozifanya ndogo ndogo hata kama huzikumbuki…Ukimsamehe mtu aliyekuudhi siku moja na wewe utamuudhi mwingine na Bwana atampa moyo wa kukusamehe wewe.

Ukimsaheme mtu anayetamani kusamehewa na wewe, siku moja na wewe utasamehewa na mtu ambaye ungetamani akusamehe.

Mithali 16:7 “Njia za mtu zikimpendeza Bwana, Hata adui zake huwapatanisha naye”.

Bwana akubariki.

Usisahau tena “nguvu ya msamaha ipo katika kusamehe”

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii 0789001312


Mada Nyinginezo:

SAMEHE KUTOKA NDANI YA MOYO WAKO.

UMUHIMU WA KUOMBA MSAMAHA.

DHAMBI ISIYO NA MSAMAHA.

Kwanini pale Bwana Yesu alichukua hatua ya kumsamehe dhambi kwanza kabla ya kumponya yule mtu mwenye kupooza?(Marko 2).

UWEPO WA BWANA HATA KATIKATI YA MATESO.

DUNIANI MNAYO DHIKI.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/01/17/nguvu-ya-msamaha/