UMUHIMU WA KUOMBA MSAMAHA.

UMUHIMU WA KUOMBA MSAMAHA.

Jambo ambalo watu wengi hawafahamu ni kuwa ndani ya mtu kuna kitu kinachoitwa DHAMIRI.. Hichi ndicho kinachomshuhudia mtu kuwa alichokifanya ni sahihi au sio sahihi hata kama jambo hilo litaonekana mbele za watu ni jema, ikiwa ni baya, basi ndani ya moyo wake mtu huyo dhamira yake yenyewe tu itamshuhudia kuwa alichofanya sio sahihi, au kama kitendo alichokifanya ni sahihi, basi dhamira yake vilevile itamshuhudia hivyo hata kama ulimwengu mzima utasema alichokifanya ni kibaya.

Sasa mtu anapofanya kosa, labda tuseme labda kamtukana ndugu yake, au katoka nje ya ndoa kisirisiri, au kaiba, au kamsengenya mwenzake, au kamsababishia mwenzake jambo baya pengine kamwambukiza ugonjwa wa ukimwi kwa makusudi, moja kwa moja ndani ya moyo wake mtu huyo, Dhamiri yake inamshuhudia kafanya kitendo baya…

Hivyo siku ile ya mwisho Mungu ataihukumu dhamira yake.

1Timotheo4:1 “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;

2 kwa unafiki wa watu wasemao uongo, WAKICHOMWA MOTO DHAMIRI ZAO WENYEWE;”

Dhamiri yako inakushuhudia kabisa umefanya makosa.

Wengi wetu tunaogopa tuomba msamaha, bali tunatafuta njia mbadala ya kujisafisha..

Mimi sio mfuatiliaji wa mambo ya siasa lakini linikutana na jambo moja nikajifunza, kama wewe ni mfuatiliaji wa Siasa utakumbuka kuna kipindi baadhi ya wabunge na mawaziri walimzungumzia vibaya Mheshimiwa Raisi, na sauti zao zikarekodiwa na kusikiwa karibu kila mahali nchi nzima..

Lakini baadhi yao, walipoona kuwa walichokifanya sio sahihi, walijisalimisha wenyewe na kwenda kumfuata Raisi ikulu kumwomba msamaha..Na mmojawapo akakiri mwenyewe na kusema tangu ule wakati mambo hayo yalipojulikana hakuwa na Amani kabisa, hata usiku usingizi alikuwa hapati, lakini sasa anasema baada ya kumwona Raisi na kumwomba  msamaha, ile amani yake yote imemrudia tena..

Unaona hapo? Kilichokuwa kinamtesa ndani ya nafsi yake ndio hiyo dhamiri ambayo pengine hata wewe inakusumbua leo hii, Dhamiri yake ilikuwa inamshuhudia kuwa alichokifanya kweli sio sahihi, hivyo moja kwa moja hakwenda kutafuta njia mbadala ya kujisafisha, kwa namna yoyote ile, kama  angefanya vile basi ile hali ya kuhukumiwa bado ingeendelea kubaki ndani yake, haijalishi watu nchi nzima itamwona ameonewa..Hivyo njia pekee ilikuwa ni kwenda kuomba msamaha.

Vivyo hivyo na wewe pengine umefanya jambo unajua kabisa sio sahihi,..na dhamiri yako inakushuhudia, nataka nikuambie usikawie kuomba msamaha, ikiwa ulimkosea mzazi wako basi mfuate na kumwomba msamaha, ikiwa ulimkosea rafiki,au bosi, au jirani, mke wako, mume wako au Mungu  mwenyewe kwa kufanya dhambi za makusudi mbele zake basi usikawie kuomba msamaha,..

Kwasababu faida ya kwanza utakayoipata kwa kuomba msamahani ni kuwa utakuwa  HURU na kujihisi AMANI nyingi. Ipo sauti inaweza kukwambia ndani yako Aaah! Yule hatakusamehe, au aah! Yule atakuona wewe ni mnyonge!!..Nataka nikuambie hakuna mtu ambaye akiona mtu amejishusha mbele zake na kumwomba masamaha asimuhurumie Yule mtu, hakuna…Hata kama ni wewe ukiona mtu ambaye siku moja alikusema vibaya akaja kwa upole na kukiri kuwa alikukosea, akaomba msamaha kwa dhati kabisa, ukamchukia mtu huyo haiwezekani..Kwanza ndivyo utakavyompenda zaidi..Sasa na wewe usiogope kwenda kuomba msamaha..fanya haraka kabla hujafa katika hali hiyo.

Pia Mungu anataka kitendo cha kuomba msamaha kiwe sehemu ya maisha yetu mbele zake,..Na ndio maana hata katika ile sala ya Baba yetu..utaona tunasema Utusamehe dhambi zetu, kama nasi tunavyowasamehe waliotukosea.

Mathayo 6:9 “Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje,

10 Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.

11 Utupe leo riziki yetu.

12 Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu.

13 Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. [Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.]”

Hivyo usiogope kuomba msamaha.

Ubarikiwe.


 

Mada nyinginezo:

SAMEHE KUTOKA NDANI YA MOYO WAKO.

RACA.

TOBA IGUSAYO MOYO WA BWANA.

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

FAIDA ZA MAOMBI.

EPUKA KUTOA UDHURU.


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments