KWANINI MUNGU ALIMTUMIA MUSA KWA VIWANGO VILE?

by Admin | 25 January 2020 08:46 am01

Shalom, Karibu tujifunze Neno la Mungu. Lipo swali ambalo tunaweza tukajiuliza siku ya leo, ni kwanini miujiza yote ile mikubwa namna ile Mungu alimtumia musa kuifanya na si mtu mwingine?…Licha ya kuwa ulikuwa ni mpango wa Mungu kuwaokoa wana wa Israeli kwa mkono hodari lakini pamoja na hayo ipo siri nyingine ambayo tunaweza kujifunza kwa Musa ambayo tukiijua na sisi basi Mungu atafanya kazi na sisi katika viwango vingine vya juu zaidi…

Mwanzoni kabisa wa huduma ya Musa, tunaona Mungu hakujidhihirisha kwake kwa njia ya wazi, ikiwa na maana kuwa hakumwona malaika, wala nabii, wala hakusikia sauti yoyote ikimwambia Njoo! Musa nataka nikutume., alichoona tu ni muujiza, kama na sisi tunavyoona leo hii miujiza ya wazi.. na hiyo ndio inayotupa uthibitisho kuwa wito wa Musa hakuwa wa kipekee sana kama wengi wetu tunavyodhani..

Kama unadhani kuona kijiti kinaungua halafu hakiteketei ni muujiza mkubwa zaidi ya unayoona leo hii roho za wafu zinafufuliwa kwa jina la Yesu kutoka mautini, jifirie mara mbili tena…

Lakini biblia inatuonyesha tabia ambayo Musa alikuwa nayo, pindi alipouona muujiza ule tu, hakupita kando, badala yake, moyo wake uliguswa sana, akasema muujiza huu hautanipita mpaka nijue maana yake ni nini, na ni nani aliyeweza kufanya maajabu makubwa kama haya..Ndipo Musa akasogea karibu..Embu jaribu kutengeneza picha akiwa pale akikitazama ki-mti kile cha kijani, kwa butwaa, akikiangalia mara mbili mbili, pengine anajiuliza kichwani, huyu aliyeweza kufanya hivi bila shaka atakuwa ni mkuu sana kwa maajabu na uweza, laiti ningemjua ningemng’ang’ania nisingemwacha….

Sasa wakati akiwa anafikiria hivyo na anataka kukaribia karibu zaidi ili azidi kuchunguza anachokiona ni macho yake au la! saa hiyo hiyo Mungu akaanza kuzungumza naye na kumwambia Musa,usikaribie mahali hapa, maana unaposimama ni nchi takatifu…..Tusome..

Kutoka 3:1 “Basi huyo Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu.

2 Malaika wa Bwana akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea.

3 Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei.

4 Bwana alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa.

5 Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu.”.

Kama tunavyojua sote baada ya hapo, ni nini kilitokea katika huduma ya Musa..Mungu alimtumia kwa ishara na miujiza isiyokuwa ya kawaida kwa kipindi chote..

Lakini tujiulize, Ni kwanini Mungu hakuzungumza naye moja kwa moja tangu mwanzoni na kumpa huduma ile kubwa, mpaka akaruhusu kwanza ageuke?

Ni kwasababu Mungu alikuwa anapima kujali kwake kwanza..Na ndio maana akatanguliza kwanza ule muujiza mdogo wa kijiti kuteketea, ili aone kama Musa atauthamini kwa kutaka kujua maana yake au La! ..Na laiti kama Musa asingeuthamini, na kupita zake kuendelea na mambo yake ya uchungaji kamwe Mungu asingekuwa na habari na Musa..maisha yangeendelea kama kawaida tu, kama vile hakuna chochote kilichotokea.

Mungu huwa anawaza na kusema, ikiwa muujiza mdogo kama huu hauthamini, atauthamini vipi nikija kumpasulia habari huko mbeleni, atathamini vipi siku nikijifunua kwake kama nguzo ya moto huko mbeleni?, atathamini vipi wakati nawashushia mana kutoka mbinguni? Atathamini vipi siku nikiyowatolea maji mwambani?.

Lakini Musa alithamini madogo yale, na Ndio maana Mungu alimtumia Musa katika makubwa pia.

Hata sisi ni kwanini Mungu hasemi na sisi au hatembei na sisi katika viwango vingine? Ni kwasababu hatuithamini miujiza ile midogo anayoipitisha mbele yetu sasa.. Tunaona ni kawaida tu..Musa hakuona kawaida….Kama Musa leo hii angeona wafu wanafufuliwa, tujiulize angemshangaa Mungu kwa viwango gani?..Je! yale Mungu anayotutendea ambayo tunaona kabisa ni miujiza mikubwa, Je yanatutafakarisha usiku na mchana, na kutufanya tumshangae Mungu na kumshukuru daima mpaka kumpa Mungu aone sababu ya kutufanyia na makubwa zaidi ya hayo? Je! yale tunayoona wengine wanatendewa na Mungu, na tunaona kabisa ule ni muujiza, Yule kaponywa, Yule kafunguliwa, Yule kaokolewa, Je hayo yanatuingia mioyoni mwetu kiasi cha kwamba yanatugeuza na kutufanya tumshangae Mungu kwa kipindi kirefu au tunayapuuzia tu?

Nataka nikuambie tukiyathamini hayo tunayoona leo hii kama madogo, na kuyatafakari sana, na kumsifu Mungu kwa ajili ya hayo, tuwe na uhakika kuwa tutafungua milango ya kuoiona miujiza mikubwa isiyokuwa ya kawaida katika Maisha yetu, au katika huduma zetu. Kama Mungu alimtumia Musa anaweza kututumia na sisi pia kudhihirisha utukufu wake kwa wasio mjua.

Lakini leo tukiyapuuzia, tujue kuwa hatutafika popote,..Tuthamini haya madogo tunayoyaona kwanza, na ndipo hayo makubwa mengine Mungu atuzidishie..tujifunze kwa mababa hawa waliotutangulia tufanikiwe..

Ubarikiwe.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii 0789001312


Mada Nyinginezo:

KWANINI DAUDI ALIKUWA NI MTU ALIYEUPENDEZA MOYO WA MUNGU?

Nifanye nini ili niwe na uhakika nikifa naenda mbinguni?

MIILI YA UTUKUFU ITAKUWAJE?

FAHAMU ZA WATU HUWA ZINAONDOLEWA NA NINI?

Kwanini Mungu hakumuua Nyoka, akamwacha Hawa ajaribiwe katika bustani ya Edeni?

“Ninyi ni chumvi ya dunia” Andiko hilo lina maana gani?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/01/25/kwanini-mungu-alimtumia-musa-kwa-viwango-vile/