USIMZIMISHE ROHO.

by Admin | 13 March 2020 08:46 pm03

1Wathesalonike 5:18 “Shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu. 19 MSIMZIMISHE ROHO;”

Roho Mtakatifu anafananishwa na moto…Wakati ule wa Pentekoste Roho aliposhuka juu ya wale watu..alishuka mfano wa ndimi za moto…Hakushuka kama ndimi tu, bali kama ndimi za moto.. Maana yake ni kwamba Roho Mtakatifu anafananishwa na moto kwa tabia zake.

Sasa maana ya ndimi za moto ni nini?…Maana yake ni katika vinywa vyao zilitoka lugha zenye kuchoma kazi zote za Adui…Ndio maana muda mfupi tu baada ya tukio lile, wale mitume waliposimama na kuwashuhudia watu, walichomwa mioyo yao kwa namna isiyokuwa ya kawaida, na siku hiyo hiyo wakatubu watu elfu tatu na kubatizwa.

Matendo 2:1 “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja.

2 Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi.

3 Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.

4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.

Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu.

6 Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.

7 Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya?

8 Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo?”

Tukienda mpaka mstari wa 37 unasema..

“37 Walipoyasikia haya WAKACHOMWA MIOYO YAO, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.

40 Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi.

41 Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka WATU WAPATA ELFU TATU.”.

Unaona? Hapo walichomwa mioyo yao?..sasa kilichowachoma ni nini…ni maneno ya moto yaliyokuwa yanatoka katika vinywa vya wale mitume walipokuwa wanawahubiria, siku zote walikuwa wanaishi na wakina Petro lakini maneno yao yalikuwa hayawachomi, lakini siku hii ya Pentekoste baada ya kupokea ndimi za moto..Maneno yao yakawa na uwezo wa kuchoma nia za Adui shetani ndani ya mioyo ya watu na kuwafanya waitii Injili. Hiyo yote ni kutokana na Roho waliyempokea na si kingine.

Hali kadhalika ndimi hizi hizi za moto walizozipokea Mitume ambazo kwa maneno yale machache tu siku ile waliweza kuwavuta watu wengi kwa Kristo takribani elfu 3…Ndio moto huo huo ambao wakiomba kitu kwa Mungu wa mbingu na nchi Mungu anawasikia na kuwajibu haraka zaidi kuliko wangekuwa hawana roho..Kwasababu ndimi hizo hizo zinaingia mpaka kwenye moyo wa Mungu na kwenda kumshawishi Mungu kwa kuugua kusikoweza kutamkwa na hivyo kupokea majibu kwa haraka sana..(Kumbuka neno ndimi ni wingi wa neno ULIMI, na ulimi ni neno linalowakilisha Lugha/usemi)..

Hivyo Usemi uliovuviwa Roho Mtakatifu unakuwa ni usemi wa moto. Kwahiyo mtu yeyote mwenye Roho Mtakatifu anapoomba iwe kwa kunena kwa lugha au isiwe kwa kunena kwa lugha, ule usemi wake mbele za Mungu unakuwa kama ni moto..unapenya mpaka kwenye vilindi vya moyo wa Mungu na kumshawishi kwa namna isiyoelezeka..hiyo ndiyo maana ya lile neno linalosema “Roho hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa (Warumi 8:26)”.

Maana yake ni kwamba tunapoomba tukiwa na Roho Mtakatifu lugha zetu hizi mbele za Mungu haziendi kama za watu wengine wa kawaida bali zinakwenda zikiwa zimejazwa nguvu mara nyingi zaidi za kuushawishi moyo wa Mungu kuliko tunavyoweza kuelezea..Kama tu vile mtu mwenye Roho Mtakatifu anavyohubiri, hatatumia nguvu nyingi kumshawishi Yule mtu aokoke..bali yale maneno yake yatakwenda kama moto wa Roho kuugua ndani ya Yule mtu kwa namna isiyoweza kutamka, na hatimaye Yule mtu kukata shauri kuokoka.

Lakini sasa huyu Roho Mtakatifu anaweza kuzimishwa..na ndio biblia inatuambia hapo.. “Msimzimishe Roho”..Maana yake ule moto wa Roho ndani ya mtu unazima. Maneno yake yanakuwa hayana nguvu tena ya kumbadilisha mtu, wala yanakuwa hayana nguvu tena kuushawishi moyo wa Mungu kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.

Mtu anapofikia hali kama hii ambapo “Roho kashazima ndani yake”…atalazimisha kutumia nguvu zake za kimwili na hekima yake ya kibinadamu na kila mbinu kumshawishi mtu amgeukie Mungu na atashindwa..

1Wakorintho 2:4 “Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu,

5 ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu”.

Hali kadhalika maombi yake siku zote yatakuwa sio ya kuushawishi moyo wa Mungu..

Sasa ni mambo gani yanayomzimisha Roho ndani ya Mtu?

Jambo la kwanza ni kuudharau msalaba na kumfanyia Jeuri Roho Mtakatifu kwa kulidharau Neno lake…Neno lake linaposema hivi, na ndani ya moyo wako Roho Mtakatifu anakushuhudia kabisa kwamba jambo hili kulifanya sio sawa,..lakini wewe unalipuuzia, unadharau au unaonyesha jeuri mbele yake unafanya yale yasiyompendeza..hapo ule moto ambao pengine ulikuwa umeshaanza kuwaka ndani yako unazima ghafla.

Waebrania 10:29 “Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, NA KUMFANYIA JEURI ROHO WA NEEMA?”

 2.Pili unapompinga Roho Mtakatifu kwa matendo yako..Kumpinga maana yake hukubaliani na kile anachokisema..Kwamfano biblia inasema.. “Waefeso 5.18 Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho;”..Na wewe unasema maana yake sio hiyo bali ni nyingine, na huku unaendelea kujihalalishia ulevi..hapo unampinga Roho Mtakatifu..Au biblia inaposema..

“1Timotheo 2:9 Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;

10 bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu.”…

Na wewe unasema maana yake sio hiyo bali ni nyingine..hapo unapingana na Roho Mtakatifu na hivyo upo hatarini kumzimisha Roho.

Matendo 7:51 “Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo”.

Ili tufanikiwe katika kila kitu hapa duniani, tunamhitaji Roho Mtakatifu..Huyo ni kama moto, akizimika ndani yetu hakuna chochote tutakachoweza kufanya..hata maombi yetu yatakuwa ni bure mbele za Mungu..Na kama tayari kashazima ndani yetu suluhisho la kuurudisha ule moto wake ni kutubu na kuanza kumtii Roho Mtakatifu, na kutompinga wala kulidharau Neno lake.

Kama hujampa Yesu Kristo maisha yako basi mpe leo, ulitii Neno lake wala usiudharau msalaba kwani ni kwa faida yako, tubu leo kwa kumaanisha kuziacha dhambi zote ulizokuwa unazifanya, na nenda kabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa na kwa jina la YESU, na Roho Mtakatifu atashuka juu yako kama moto.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

Je! hizi roho saba za Mungu ni zipi? na je zinatofautiana na Roho Mtakatifu?

MAFUNDISHO YA MASHETANI

KWANINI AWE PUNDA NA SI MNYAMA MWINGINE?

SIKUJA KULETA AMANI DUNIANI, BALI MAFARAKANO.

JINSI ROHO MTAKATIFU ANAVYOWAFUNULIA WATU MAANDIKO.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/03/13/usimzimishe-roho/