by Admin | 9 April 2020 08:46 pm04
Shalom, Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe daima..
Karibu tuzidi kujifunza maneno matakatifu ya Mungu, Na leo tutaona kwa ufupi habari ya mtu mmoja anayeitwa Absalomu mwana wa Daudi naamini lipo jambo utajifunza ndani yake..
Huyu Absalomu alikuwa ni mmojawapo wa wana wengi wa Daudi, isipokuwa yeye alikuwa anabeba kitu kingine cha ziada ambacho kilikuwa kinamtofautisha na wana wote wa Daudi waliokuwa katika enzi yake ya kifalme.
Biblia inatueleza Absalomu, alikuwa ni kijana mzuri sana (kwa lugha ya kiingereza labda tunaweza tukasema Handsome), sio tu katikati ya ndugu zake, bali pia katika Israeli nzima ndivyo walivyomwona, hakukuwa na kijana aliyekuwa mzuri kama yeye, kuanzia utosi wa kichwa chake, mpaka uwayo wa miguu yake, wanasema hakuna mwanadamu asiye na mapungufu, lakini huyu Absalomu yeye hakuwa na upungufu wowote katika mwili wake. Kila kiungo chake cha mwili kilionekana kizuri na cha kuvutia, na alisifiwa na kila mtu..
Na Zaidi ya yote, biblia imezitaja hizo nywele zake, inasema, alikuwa na nywele nzuri nzito, ambazo alikuwa hawezi kuziacha Zaidi ya mwaka mmoja bila kuzinyoa vinginevyo vitamlemea sana, embu tusome kidogo..
2Samweli 14:25 “Basi katika Israeli wote hapakuwa na mtu hata mmoja mwenye kusifiwa kwa uzuri wake kama huyo Absalomu; tangu nyayo za miguu yake hata utosi wa kichwa chake hapakuwa na ila kwake.
26 Naye aliponyoa kichwa, (basi mwisho wa kila mwaka hunyoa; na kwa sababu nywele zilikuwa nzito kwake, kwa hiyo akanyoa;) hupima nywele za kichwa chake shekeli mia mbili kwa uzani wa mfalme.”
Unaona, ukisoma hapo utaona nywele hizo alikuwa akishazinyoa zilikuwa zinakwenda kupimwa kwenye uzani wa mfalme, na inapatikana shekeli mia mbili ambayo ukiigeuza kwa vipimo vya kisasa ni Zaidi ya kilogramu 2.. Unaweza kutengeneza picha uzito wa kilo mbili ulikuwa unamlemea kichwani pake kama asipokata nywele zake baada ya mwaka mmoja..
Ili kuelewa vizuri, wanasema mtu wa kawaida ambaye amebahatika kuwa na nywele nyingi na zinazokuwa, akaziacha mwaka mzima, ili uzito wake uweze kufikia ule wa nywele za Absalomu kwa mwaka, basi itahitaji wachukuliwe watu kama yeye thelathini (30) kwa mwaka, kisha zichanganywe ndipo zitafikia uzito wa nywele za Absalomu ndani ya mwaka mmoja..
Hivyo unaweza kuona jinsi gani mtu huyu alipewa umbile la kipekee sana, na uzuri wa tofauti, nywele zenye utofauti sana lakini tunaposoma biblia tukumbuke kuwa siku zote biblia inapotaja umbile Fulani la mtu, basi tujue kuwa lina sehemu Fulani ya kusimamia katika habari husikia mbeleni,.. Hivyo kutajwa kwa sifa za nywele za Absalomu, ni wazi kuna mahali litatumika huko mbeleni..
Hivyo ukipata muda wako binafsi wa utulivu unaweza kuzisoma habari zake, kwa urefu na jinsi alivyokuwa, (2Samweli 13-18 )lakini kwa ufupi ni kuwa Absalomu, Japokuwa alikuwa na uzuri na umbile la kipekee na maneno ya kuvutia ambayo yaliweza kuifanya Israeli yote wampende mpaka kutaka kumfanya awe mfalme, lakini moyo wake ulikuwa ni tofauti na watu walivyokuwa wanamdhania..
Kwanza alikuwa na lengo la kuudondosha ufalme wa baba yake Daudi kinyume chake ili yeye atawale na Zaidi ya yote alikuwa anamtafuta baba yake ili amuue, pili alikuwa radhi hata kulala na Masuria 10 wa baba yake ili kuwaonyesha watu kuwa hampendi, japokuwa baba yake hakuwahi kumfanyia ubaya wowote..Na tatu alikuwa radhi kumuua ndugu yake, ambaye alilala na Dada yake, wala hakumsamehe..
Kwahiyo Absalomu, alikuwa ni mwovu, wala hakuwa mtu mwema, licha ya kuwa alikuwa ni mzuri na mwenye ushawishi wa maneno kwa watu.
Sasa ukizidi kusoma habari utaona alipokusudia kumwangamiza baba yake(Daudi), baada ya kumfukuza kwenye kiti cha enzi, aliondoka kwenda msituni yeye pamoja na jeshi kubwa la Israeli nyuma yake..Biblia inatuambia vita ilikuwa vikali sana katika msitu ule mkubwa sana.. Na unajua jinsi misitu ilivyo, vichaka vizito na miti ya Kamba Kamba za miiba inakuwa ni mingi sana, na inakuwa ni rahisi mtu kunaswa katika vichaka hivyo kama hutakuwa mwepesi..
Sasa kutokana na msitu ule kuwa mzito sana, biblia inasema watu waliokufa kwa uzito wa msitu ule, walikuwa ni wengi kuliko waliokufa kwa upanga.. Na huko huko lipo jambo ambalo Absalomu naye alikutana nalo embu tusome kwa ufupi..
2Samweli 18:6 “Hivyo watu wakatoka waende nyikani ili kupigana na Israeli; na vita vikatokea ndani ya msitu wa Efraimu.
7 Watu wa Israeli wakapigwa huko mbele ya watumishi wa Daudi, kukawa na maangamizo makuu huko siku ile, ya watu ishirini elfu.
8 Kwa maana vita vilienea huko juu ya uso wote wa nchi; na siku ile huo msitu ukala watu wengi kuliko wale walioliwa na upanga.
9 NA KWA BAHATI ABSALOMU AKAKUTANA NA WATUMISHI WA DAUDI. NAYE ABSALOMU ALIKUWA AMEPANDA NYUMBU WAKE, NA YULE NYUMBU AKAPITA CHINI YA MATAWI MANENE YA MWALONI MKUBWA, HATA KICHWA CHAKE KIKAKWAMA KATIKA MWALONI HUO, AKANYAKULIWA JUU KATI YA MBINGU NA NCHI; NA YULE NYUMBU ALIYEKUWA CHINI YAKE AKAENDA MBELE.
10 Basi mtu mmoja akaona hayo, akaenda akamwambia Yoabu, akasema, tazama, mimi nalimwona Absalomu ametundikwa katika mwaloni.
11 Naye Yoabu akamwambia mtu yule aliyempasha habari, Je! Wewe umeona haya; Mbona, basi, hukumpiga hata nchi papo hapo? Nami ningalikupa fedha kumi na mshipi.
12 Yule mtu akamwambia Yoabu, Kama ningalipata fedha elfu mkononi mwangu, hata hivyo singalinyosha mkono wangu juu ya mwana wa mfalme; kwa maana mfalme masikioni mwetu alikuagiza wewe, na Abishai na Itai, akisema, Angalieni sana mtu awaye yote asimguse yule kijana, Absalomu.
13 Na tena, kama ningaliitendea roho yake kwa hila; (wala hapana neno lo lote liwezalo kufichwa mbele ya mfalme); ndipo wewe mwenyewe ungalijitenga.
14 Ndipo Yoabu akasema, Siwezi kungoja na kusema nawe hivi. Akachukua vyemba vitatu mkononi mwake, akamchoma Absalomu moyoni, alipokuwa akali hai katikati ya ule mwaloni.
15 Kisha vijana kumi, waliomchukulia Yoabu silaha zake wakamzunguka, wakampiga Absalomu, na kumwua.
Utaona, hapo Absalomu, alipopita sehemu moja, biblia inasema kichwa chake kikakwama, kwenye mti mmojawapo, na yule farasi aliyekuwa chini yake akazidi kuendelea mbele, hivyo yeye akabakia pale pale amening’inia. Sasa, biblia inaposema kichwa inamaanisha eneo la nywele kwa ujumla wake, Ni kwamba zile nywele nyingi za Absalomu zilikwama kwenye vijiti vya miti, zikajisongorotesha pale, kwa namna ambayo asingeweza kuzifumua, akabakia tu anani’ngia nia tu pale kwa maumivu.. alikaa pale muda mrefu akijaribu lakini alishindwa kutoka mpaka mauti ilipomfika kwasababu ule uzuri wake ndio ulikuwa kitanzi chake..
Ndugu, hata sasa, watu wengi hawajui kuwa kile kinachowafanya wavutie, au wapendwe ndani yao ndio kitakuwa kitanzi chao baadaye ikiwa hawatasimama katika mstari wa wokovu.. Ikiwa ni mali zako zinakupa kiburi kumbuka yale maneno ya Bwana, Ni rahisi kwa ngamia kupenya katika tundu la sindano… Ikiwa ni urembo wako wewe binti, unajiona sasa huna haja ya Mungu bado wewe unavutia, una umbile zuri, kila mwanaume akikuangalia anakutamani, wakati utafika huo huo uzuri wako utakuwa kitanzi kwako, utanasa mahali ambapo hutatoka, na adui yako shetani atakumaliza kirahisi mbele ya macho yako ukiona kama ilivyokuwa kwa Absalomu, na ukajikuta katika lile ziwa la moto,..Vivyo hivyo na mambo mengine yote.
Huu ni wakati sasa wa kumtazama Kristo, na kuomba rehema kwake, kama na wewe umedanganywa na mojawapo ya hayo mambo, uzuri wako na utanashati wako. Tubu umgeukie Mungu, ili Mungu akurehemu na kukupa uzima wa milele. Nyosha njia yako kwa kuliamini na kulitii Neno la Mungu.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
UCHAWI WA BALAAMU.
USIPOWATAMBUA YANE NA YAMBRE, KATIKA KANISA LA KRISTO, UJUE UMEPOTEA.
USIPOWATAMBUA YANE NA YAMBRE, KATIKA KANISA LA KRISTO, UJUE UMEPOTEA.
KUTAKUWA NA MATETEMEKO YA NCHI, NJAA NA TAUNI.
NIMEOKOKA, ILA MUNGU NDIYE ANAYEJUA NITAKWENDA WAPI.
KWANINI YESU KRISTO NI WA MUHIMU KWETU SASA?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/04/09/angalia-uzuri-wako-usigeuke-kuwa-kitanzi-chako/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.