by Admin | 5 May 2020 08:46 pm05
Bwana alimaanisha nini kusema “Hamtaimaliza miji ya Israeli hata ajapo mwana wa Adamu”
Tusome;
Mathayo 10:23 “Lakini watakapowafukuza katika mji huu, kimbilieni mwingine; kwa maana ni kweli nawaambia HAMTAIMALIZA MIJI YA ISRAELI HATA AJAPO MWANA WA ADAMU”
JIBU: Ukiusoma mstari huo kuanzia juu kabisa, yaani kuanzia mstari wa kwanza…Utaona ni Habari inayohusu tendo la Bwana Yesu kuwatuma wanafunzi wake kwenda kuhubiri injili katika miji ya Israeli…Na utaona alipowaagiza wakahubiri aliwapa na baadhi ya maagizo au masharti, kwamba wasichukue chochote na pia wawe wavumilivu kwa watakayoyapitia huko..Lakini mwishoni kabisa mwa maagizo tunaona Bwana anawaambia…“hamtaimaliza miji ya Israeli hata ajapo mwana wa Adamu”..
Sasa swali linalojitengeneza kwenye vichwa vyetu hapo ni kwamba…mbona Bwana Mitume walikuwa wameshaimaliza hiyo miji na Yesu bado alikuwa hajarudi?..ina maana mpaka leo injili haijasambaa kwenye miji yote ya Israeli ndio maana Bwana hajarudi mpaka leo?.
Jibu rahisi la swali hili tunaweza kulipata kwenye Habari kama hii hii katika kitabu cha Luka…Tusome,
Luka 10:1 “Basi, baada ya hayo Bwana aliweka na wengine, sabini, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenda kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe.
2 Akawaambia, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake.
3 Enendeni, angalieni, nawatuma kama wana kondoo kati ya mbwa-mwitu.
4 Msichukue mfuko, wala mkoba, wala viatu; wala msimwamkie mtu njia”
Tuvichunguze baadhi ya vipengele katika mstari huo wa kwanza ambavyo ndivyo vitakavyotupa dira ya kuelewa Habari nzima….katika mstari wa kwanza biblia inasema… “Bwana aliweka na wengine, sabini, AKAWATUMA WAWILI WAWILI WAMTANGULIE kwenda kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe”…Zingatia hilo neno “WAMTANGULIE”..Kama wewe ni mswahili mzuri utaelewa maana ya neno “kutangulia” ni nini…kutangulia maana yake ni mtu anakwenda mahali kisha wewe unafuata baadaye…yaani anawahi kufika kule kabla wewe kufika…hiyo ndiyo maana ya kutangulia…
Hivyo mstari huo una maana kuwa “hao wanafunzi sabini na wale 12 Bwana aliokuwa anawatuma kwenda huko katika miji ya Israeli hakuwatuma tu…huko wenyewe…bali Bwana aliwaahidi kwamba atawafuata, hivyo aliwatuma tu kama wamtangulie.”
Ili kuelewa vizuri tafakari tena kamfano haka… “Umemwagiza mfanyakazi wako atangulie asubuhi na mapema sehemu ya kazi kuendelea na kazi, na ukamwambia hatamaliza kazi zote kabla ya wewe kufika hapo ofisini, maana yake utafika kabla hata hajamaliza kazi zote”.. Ndicho Bwana alichowaambia wanafunzi wake, kwamba huko wanakwenda naye pia atakuja kabla hawajaimaliza miji yote ya Israeli (Hilo ni neno la Faraja)…Na kweli aliiungana nao baadaye hakuwaacha yatima…
Sasa kuna jambo moja la kujifunza hapo…Kwamba Desturi ya Bwana ilikuwa hafiki mahali kabla ya kutuma kwanza wajumbe wake wakamtengenezee njia…Maana yake kabla ya yeye kuja mahali anatuma kwanza watumishi wake wakahubiri injili..Ndivyo alivyofanya kwa Yohana Mbatizaji…yeye alitumwa kumtengenezea Bwana njia na kuiandaa mioyo ya watu kabla Bwana mwenyewe hajaanza kuhubiri..ili atakapoanza kuhubiri vile Bwana atakavyohubiri visiwe ni vitu vigeni sana kwa watu wake.(kasome Yohana 10:41-42, na Luka 1:17).
Utaona sehemu zote kabla Bwana hajaenda mahali huwa anatuma wanafunzi wake kwanza na baadaye anaungana nao.. (kasome Luka 9:52-54, Marko 14:12-18, Marko 11:1-4)..
Ndugu Mpendwa hata sasa, Bwana bado anatuma watu wake kuitengeneza njia yake…Umesikia injili mara ngapi?, kila mahali upitapo, mtaani, kwenye magari, mashuleni, unapofanyia kazi?..lakini unadharau kwasababu labda anayekuhubiria umemzidi kipato, au umemzidi elimu, au umri?..Lakini lisikie hili neno ambalo Bwana Yesu alilisema..
Marko 9:37 “Mtu akimpokea mtoto mmoja wa namna hii kwa jina langu, anipokea mimi; na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma”
Hako katoto unakokadharau sasa, huyo uliyemzidi elimu, pengine na kipato…huyo ambaye hata maandiko hawezi kuyatamka vizuri na anakuhubiria utubu umgeukie Mungu lakini unamchukulia unavyojua wewe…Bwana Yesu ambaye sasa hivi yupo mbingu za mbingu anamheshimu, siku ile tutaonyeshwa tumemkataa yeye Dhahiri.
Bwana atusaidie.
Kama bado hujampa Yesu Kristo Maisha yako, tupo ukingoni sana mwa siku za mwisho, ambapo ghafla tu unyakuo utapita na watakatifu watatoweka….waliobaki hawatasikia tena usumbufu wa mahubiri wanayohubiriwa sasa..watakuwa wamefungua jalada lingine la maisha..na watakatifu vivyo hivyo..Kwahiyo sio wakati wa kukaa nje..Mlango wa Safina unakaribia kufungwa, waasherati,walevi, wezi, watukanaji, watazamaji picha chafu mitandaoni, wanaokula rushwa, na wanaofanya kila aina ya machafuko biblia inasema sehemu yao itakuwa ni katika lile ziwa la moto. Ingia leo ndani ya Safina ya Yesu, wokovu unapatikana bure.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
Wewe u nabii yule akajibu la!..swali huyu ‘nabii yule’ ni nani?
JE! WEWE NI MWAKILISHI MWEMA?
Kwanini Bwana alisema Hakuna aliye mwema ila mmoja?
Kwanini Bwana alisema Hakuna aliye mwema ila mmoja?
Habari ile ya Pilato kuchanganya zile damu za wayahudi na pamoja na dhabihu zao,(Luka 13) ilihusu nini?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/05/05/hamtaimaliza-miji-ya-israeli-hata-ajapo-mwana-wa-adamu/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.